Madai ya wakulima yageuka kaa la moto

Muktasari:

Viongozi hao wa Chama cha Msingi cha Ushirika Jaribu (Amcos) kilichopo Kijiji cha Kitumbi Nkuya, wilayani Kilwa wamepewa wiki mbili kueleza sababu za kutowalipa wakulima fedha zao za mauzo ya korosho msimu uliopita.

Kilwa. Madai ya Sh5 milioni ya wakulima wa korosho yamegeuka kaa la moto kwa viongozi na watendaji wa chama cha ushirika wilayani hapa.

Viongozi hao wa Chama cha Msingi cha Ushirika Jaribu (Amcos) kilichopo Kijiji cha Kitumbi Nkuya, wilayani Kilwa wamepewa wiki mbili kueleza sababu za kutowalipa wakulima fedha zao za mauzo ya korosho msimu uliopita.

Mkuu wa wilaya hiyo, Christopher Ngubiagai, alitoa muda huo alipozungumza na wanakijiji hao kwenye mkutano wa hadhara.

Agizo hilo linatokana na wananchi kuwasilisha malalamiko kwake kwamba wanadai Sh5 milioni za mauzo ya korosho walizouza kwa mfumo wa stakabadhi ghalani msimu wa 2015/16.

“Nawapa siku 14 mnipatie maelezo na sababu zinazowafanya msilipe fedha za wakulima hawa, sipo tayari kuona wanahamasishwa wazalishe korosho kwa wingi, huku viongozi na watendaji wa vyama mkijinufaisha,” alisema Ngubiagai.

Alisema iwapo hataridhishwa na maelezo yao, ataagiza Polisi wilayani hapa wafanye kazi ya kuwakamata, kuwafungulia mashtaka na kuwafikisha mahakamani.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa wito kwa wakulima kuupokea mfumo wa malipo kupitia benki kwa kuwa utawahakikishia usalama wao na fedha zao.

Alisema lengo la Serikali ni jema kwa kuwa mfumo wa malipo uliopo sasa wa kubeba na kusafirisha fedha unahatarisha usalama wa wasafirishaji wanaolazimika kuzipeleka kwenye vyama vya msingi.

Awali, mkulima Hemedi Ally kwa niaba ya wenzake alilalamika kuwa viongozi na watendaji wa Amcos wamekuwa chanzo cha wananchi kuuchukia mfumo mzima wa malipo ya stakabadhi ghalani.

Alisema wanakatishwa tamaa ya kuzalisha korosho kwa kuwa hawanufaiki wao bali viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi na watendaji wao ambao wanawadhulumu.

Licha ya kuwapo madai hayo, kwa mara ya kwanza wakulima mkoani Mtwara wameuza korosho kwa mnada na kupata bei kubwa ya Sh3,670 kwa kilo moja ya zilizo ghafi badala ya Sh2,400 za msimu uliopita.

Mnada huo wa wazi ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita wilayani Masasi.