Maelezo ya Lissu yatua mahakamani

Muktasari:

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa, alidai kabla ya kuchukua maelezo ya Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, alimpatia haki za msingi ikiwamo kuwa na wakili wake John Malya.

Dar es Salaam. Askari kutoka Makao Makuu ya Polisi, Inspekta Nicholaus Mhagama ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa yeye ndiye aliyechukua maelezo ya Tundu Lissu anayeshtakiwa kwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jamhuri ya Muungano.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi kutoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa, alidai kabla ya kuchukua maelezo ya Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, alimpatia haki za msingi ikiwamo kuwa na wakili wake John Malya.

Pia alimjulisha kuwa tuhuma zinazomkabili ni kutoa maneno ya uchochezi na wakati akichukua maelezo yake alimuonyesha video iliyoonyesha alivyokuwa akitoa maneno hayo kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

“Wakati nikichukua maelezo ya onyo ya Lissu polisi, hakupinga kuhusu maneno aliyoyatamka na alisema ni kweli aliyatamka nikaendelea kuyaandika na nilipomaliza nilimpa ayasome; akayasoma na kusaini, mimi pamoja na wakili wake John Malya pia tukasaini,” alieleza shahidi huyo.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Wakili Kishenyi alimuonyesha nyaraka ya maelezo hayo ya onyo aliyoyatoa Lissu polisi, Mhagama aliyatambua akidai yana saini yake, ya mshtakiwa, ya wakili wa mshtakiwa na mwandiko ni wake.

Inadaiwa kuwa Juni 28, 2016 Lissu akiwa katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alitoa kauli za uchochezi kuwa “Mamlaka ya Serikali mbovu ya kidikteta uchwara inapaswa kupingwa kwa nguvu zote na kila Mtanzania na kwamba, utawala wa nguvu ukiachwa unaweza kupelekea nchi kuingia kwenye giza nene.”

Kesi imeahirishwa hadi Juni 22.