Maelezo ya shahidi yaibua mvutano kortini

Watuhumiwa wa kesi ya mauaji ya Erasto Msuya wakiingia katika chumba cha Mahakama Kuu mjini Moshi jana huku mtuhumiwa mmoja akisaidiwa kutembea baada ya kuugua tumbo ghafla akiwa mahabusu. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

Baada ya shahidi wa 13 Elirehema Msuya kumkubalia wakili wa utetezi Majura Magafu kukabidhi nyaraka za maelezo katika Mahakama hiyo kama ushahidi wake, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali Kassim Nassir uliweka pingamizi kupinga maelezo hayo.

Moshi. Mvutano wa kisheria umeibuka katika Mahakama Kuu mjini hapa kuhusu nani anayetakiwa na nani asiyetakiwa kutoa nyaraka za shahidi wa 13 katika kesi ya mauaji ya bilionea Erasto Msuya.

Baada ya shahidi wa 13 Elirehema Msuya kumkubalia wakili wa utetezi Majura Magafu kukabidhi nyaraka za maelezo katika Mahakama hiyo kama ushahidi wake, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali Kassim Nassir uliweka pingamizi kupinga maelezo hayo.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa shahidi huyo hakuiomba Mahakama kuchukua maelezo hayo kama ushahidi wake bali aliyeomba yapokewe kama kielelezo ni wakili Magafu.

Wakili Nassir ambaye anaiwakilisha Jamhuri alidai kuwa Magafu hana uwezo wa kutoa nyaraka mahakamani, badala yake anayepaswa kutoa nyaraka hizo ni shahidi pekee.

Baada ya pingamizi hilo, wakili Magafu aliiambia Mahakama kuwa pingamizi lililotolewa na upande wa mashtaka halina mantiki, hivyo litupiliwe mbali kwa sababu halina miguu ya kisheria na akaomba ushahidi huo upokewe.

Akitoa uamuzi, Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo alisema upande wa mashtaka hawakuwa wakimsikiliza wakili Magafu wakati akifanya mahojiano na shahidi huyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sharifu Mohamed, Shaibu Jumanne, Musa Mangu, Jalila Zuberi, Karimu Kihundwa, Sadiki Mohamed na Ally Mussa.

Yafuatayo ni mahojiano ya shahidi wa 13, Elirehema Msuya yakiongozwa na wakili Kassim Nassir.

Wakili Nassir: Unafanya shughuli gani?

Shahidi: Udereva

Wakili Nassir: Unafanyia wapi?

Shahidi: SG Resort Lodge.

Wakili Nassir: Iko wapi?

Shahidi: Sakina.

Wakili Nassir: Tarehe 6/8/2013 ulikuwa wapi?

Shahidi: Hotelini.

Wakili Nassir: Siku hiyo ilikuwaje?

Shahidi: Baada ya kutoka mjini kwenye kufanya manunuzi ya hotelini, saa 4:30 asubuhi nilimkuta marehemu (Msuya) anaongea na simu.

Wakili Nassir: Yeye na nani?

Shahidi: Alikuwa kwenye swimming pool (bwawa la kuogelea) na mtu mmoja.

Wakili Nassir: Wewe ulikuwa unafanya nini wakati huo?

Shahidi: Nilikuwa nimesimama kwenye parking (eneo la kuegesha magari).

Wakili Nassir: Nini kiliendelea?

Shahidi: Waliendelea na maongezi na baada ya muda walielekea hotelini.

Wakili Nassir: Kabla ya kwenda hotelini aliongea na huyo mtu kwa muda gani?

Shahidi: Kama dakika 20.

Wakili Nassir: Kutokea ulipokuwa umesimama na pale walipokuwa wamekaa kulikuwa na umbali gani?

Shahidi: Sio mbali.

Wakili Nassir: Walikuwa wanasemaje?

Shahidi: Walikuwa wakitazamana.

Wakili Nassir: Baada ya kuelekea hotelini ilikuwaje?

Shahidi: Walipita pale parking (eneo la kuegesha magari) nilipokuwa nimesimama.

Wakili Nassir: Baada ya hapo?

Shahidi: Erasto Msuya aliniita uko wapi kaka? Nikamwambia niko huku parking (eneo la kuegesha magari). Aliniambia washa gari, nikamwambia langu au lako? Niliwasha gari langu nikasogea karibu na marehemu (Msuya).

Akaniambia nimpeleke mgeni wake stendi ya mabasi Arusha kisha nimpandishe Coaster (basi) za Moshi.

Wakili Nassir: Nini kiliendelea?

Shahidi: Marehemu (Msuya) alimwambia huyo mtu ahakikishe anamhimiza ndugu yake wamalize hiyo biashara asubuhi.

Wakili Nassir: Baada ya hapo ilikuwaje?

Shahidi: Alimwambia sawa brother (kaka).

Wakili Nassir: Wakati marehemu (Msuya) akiwa anamwambia maneno hayo wewe ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa karibu yao.

Wakili Nassir: Baada ya hapo nini kiliendelea?

Shahidi: Aliingia kwenye gari, nilipofika stendi huyo rafiki yake akaniambia nimwache pale pale hakuna shida.

Wakili Nassir: Baada ya hapo ikawaje?

Shahidi: Nilirudi hotelini.

Wakili Nassir: Huyo mtu aliyekuwa na marehemu siku ile ukiambiwa umuonyeshe utamkumbuka?

Shahidi: ndiyo.

Wakili Nassir: Huyo mtu ana mwonekano gani?

Shahidi: Macho mekundu, uso mpana, alikuwa si mrefu wala mfupi na alikuwa mwembamba kidogo.

Wakili Nassir: Kabla ya tarehe 6/8/2013 ulishawahi kumwona?

Shahidi: Sikuwahi kumwona.

Wakili Nassir: Ulishawahi kuwa na ugomvi naye?

Shahidi: Hapana.

Wakili Nassir: Nini kiliendelea baada ya wewe kumpakiza kwenye gari yule aliyekuwa na marehemu siku ile.

Shahidi: Nilirudi hotelini, tarehe 7/8/2013 alinipigia simu akaniambia anataka Sh1 milioni hivyo nikaichukue kwa meneja kisha nitoke nje nitamkuta mtoto wake wa kike aliyemwagizia aje kuchukua kisha tukaelekea Philips na zile fedha.

Wakili Nassir: Baada ya maagizo hayo?

Shahidi: Nilimpa Sh1 milioni yule mtoto wake tulipofika pale Philips, kisha nikarudi hotelini muda kidogo marehemu aliingia.

Wakili Nassir: Nini kiliendelea?

Shahidi: Aliingia akapaki gari lake kisha akanipa simu, charger ya simu pamoja na kipimo cha kupimia mawe ya madini kisha akaingia uwani. Kabla hajatoka uwani alikuja mtoto wake akiwa na gari aina ya Range Rover akapaki na muda kidogo marehemu alitoka.

Wakili Nassir: Mtoto wake anaitwa nani?

Shahidi:Glory.

Wakili Nassir: Nini kiliendelea?

Shahidi: Alinipa funguo za gari akaniambia nimpe zile fedha Sh1 milioni, charger na kipimo cha madini.

Wakili Nassir: Ulifanyaje?

Shahidi: Nilimpa vitu vyote.

Wakili Nassir: Baada ya hapo nini kiliendelea?

Shahidi: Aliniambia anaenda KIA kufanya biashara.

Wakili Nassir: Ilikuwaje?

Shahidi: Aliondoka na ile Range Rover.

Wakili Nassir: Nini kilitokea mkiwa mjini?

Shahidi: Nilipigiwa simu na Rama kuwa Erasto Msuya amepigwa risasi huko KIA Mijohoroni.

Wakili Nassir: Baada ya huo ujumbe ulifanya nini?

Shahidi: Nilirudi hotelini nikakuta watu wanalia wanasema Erasto Msuya kapigwa risasi.

Wakili Nassir: Nini kiliendelea?

Shahidi: Meneja aliniambia tuwashe gari tuelekee KIA mimi na yule jamaa, tulipofika tukaambiwa twende Boma tulipofika kwenye hiyo zahanati tulikuta watu wamekusanyika wengi na marehemu (Msuya) akiwa ameshaingizwa ndani.

Wakili Nassir: Nini kiliendelea?

Shahidi: Tulikaa kidogo na kurudi hotelini.

Wakili Nassir: Baada ya mazishi nini kiliendelea?

Shahidi: Tuliendelea na kazi, baadaye kidogo nilipigiwa simu nahitajika Moshi mjini tarehe 7/10/2013.

Wakili Nassir: Uliambiwa unahitajika Moshi sehemu gani?

Shahidi: Kwa RCO (Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai)

Wakili Nassir: Sasa ikawaje baada ya kupata taarifa unahitajika Moshi?

Shahidi: Nilipofika Moshi niliambiwa nitamwona mtu ambaye nilimpeleka stendi tarehe 6/8/2013.

Wakili Nassir: Baada ya hapo?

Shahidi: Nilikuta watu wamepanga mistari.

Wakili Nassir: Je, ulimwona?

Shahidi: Ndiyo. Nilimshika bega, niliambiwa niandike maelezo yangu kuhusiana na huyo mtu.

Wakili Nassir: Je,ni yuleyule uliyemtambua mara ya kwanza?

Shahidi: Ni yuleyule.

Wakili Nassir: Yule bwana ulimpeleka stendi na gari gani?

Shahidi: Noah, nyeusi T108 BZC.

Wakili Nassir: Ulisema marehemu aliondoka na Range, unaweza kukumbuka namba za hiyo gari?

Shahidi: Ndio,T800 CKF.

(Mara baada ya kumaliza mahojiano hayo yalifuata mahojiano ya upande wa utetezi yakiongozwa na Wakili Hudson Ndusyepo)

Wakili Ndusyepo: Una elimu gani?

Shahidi: Kidato cha nne.

Wakili Ndusyepo: Shule gani?

Shahidi: Makumira Sekondari.

Wakili Ndusyepo: Ulimaliza mwaka gani?

Shahidi: 1992.

Wakili Ndusyepo: Ulianza kazi mwaka 2012 kweli si kweli?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili Ndusyepo: Kabla ya hapo ulikuwa unafanya nini?

Shahidi: Nilikuwa nachimba madini Mererani.

Wakili Ndusyepo: Uliajiriwa kama ndugu au mfanyakazi?

Shahidi: Mfanyakazi.

Wakili Ndusyepo: Kwenye parking (eneo la kuegesha magari) na swimming pool (bwawa la kuogelea) kuna umbali gani?

Shahidi: Siyo mbali sana.

Wakili Ndusyepo: Mbali na Erasto na huyo mgeni, kulikuwa na nani mwingine?

Shahidi: Hakuna.

Wakili Ndusyepo: Hapo swimming pool(bwawa la kuogelea) kulikuwa na nini?

Shahidi: Meza yenye mwavuli na viti viwili.

Wakili Ndusyepo: Unakumbuka hiyo siku huyo mgeni wake alikuwa amevaaje?

Shahidi: Kofia ya kapero.

Wakili Ndusyepo: Rangi yake alikuaje?

Shahidi: Mweusi.

Wakili Magafu: Ni mara ya ngapi kufika hapa mahakamani tangu kesi ianze?

Shahidi: Mara ya kwanza.

Wakili Magafu: Ulikuwa unazuiwa kuja hapa mahakamani toka kesi hii imeanza?

Shahidi: Sikuwahi kuzuiwa.

Wakili Magafu: Marehemu alikuwa bosi wako na ulikuwa unampenda? Kwanini hukuja mahakamani kesi ikiwa inaanza?

Shahidi: Shughuli zilikuwa nyingi.

Wakili Magafu: Siku ya tukio ulipata taarifa saa ngapi?

Shahidi: Kama saa saba hivi.

Kesi hiyo itaendelea leo.