Maeneo sita janga la elimu nchini Tanzania

Muktasari:

  • Hii ni mara ya pili, kwa Rais huyo wa Awamu ya Tatu kuzungumzia mustakabali wa sekta hiyo kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ameibua mjadala kuhusu elimu nchini akisema kuna janga na kushauri kuitishwa mdahalo wa wazi, utakaoshirikisha makundi yote ya jamii ili kujadili suala hilo.

Hii ni mara ya pili, kwa Rais huyo wa Awamu ya Tatu kuzungumzia mustakabali wa sekta hiyo kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

Novemba 11, 2017, akiwa katika kongamano la wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Rais Mkapa alisema Tanzania haijaweka msukumo katika kutafakari upya mfumo wa elimu.

Machi 18 mwaka huu akiwa katika hafla ya kumuaga Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idris Kikula, Rais Mkapa alisema kuna janga katika elimu. “Kwa nini ukisoma orodha ya shule zetu za sekondari kwenye ufaulu wao katika 10 bora unaweza kuwa na uhakika nane si za Serikali ni za watu binafsi? Kama Serikali ndio mhimili mkuu wa elimu, kuna kasoro gani?” Alihoji.

Alisema ni vyema ukaitishwa mdahalo wa uwazi utakaoshirikisha makundi yote na kusikia maoni badala kuwaachia wanataaluma wanaoegemea kwenye ujuzi.

Akizungumzia matatizo ya elimu na mipango ya Serikali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Ave Semakafu anasema kwamba Serikali inatambua changamoto zilizopo na tayari imeanza kuchukua hatua.

“Tukitaka kuwa wakweli, vitu vikubwa vimefanyika, ukifika shule yoyote ukikuta P4R ujue ni miundombinu mipya, pili tumeanza kufanya ukarabati wa shule kongwe, zote zilikuwa zimechoka lakini sasa hivi unakuta sura nyingine, pia tunahakikisha elimu haitolewi bila kuzingatia taratibu,” anasema.

Tatu, Dk Semakafu anasema wizara imefanya tathmini ya ubora wa vyuo vikuu na kufungia baadhi huku ikidhibiti udanganyifu wakati wa usajili na kwamba mkakati wao wa muda mrefu ni kuhakikisha kila mkoa unakua na chuo cha ufundi.

Pamoja na ufafanuzi huo, uchambuzi wa kitakwimu, maoni ya wadau yenye mifano vyote vinathibitisha elimu ni janga huku mapendekezo yaliyojikita katika maeneo sita yakitolewa.

Lugha ya kufundishia mgogoro

Aliyekuwa naibu Katibu Mkuu Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch anasema lugha sahihi ya kufundishia ni janga.

“Mfumo ulitakiwa kutumia lugha ya asili kufundishia chekechea hadi darasa la tatu na Kiswahili kuanzia la nne hadi la saba. Watalaam wa elimu wanashauri mtoto afundishwe kwa lugha ya asili kwa ngazi hiyo, Kiswahili kiwe sehemu ya somo. Akiingia kidato cha kwanza ndiyo atumie Kiingereza. Lakini kwa sasa mwanafunzi darasa la tatu hajui kutamka hata kuku kwa Kiswahili, anamaliza la saba hajui Kiswahili vizuri wakati huohuo anakutana na lugha nyingine ya Kiingereza kidato cha kwanza,” anasema Oluoch.

Utafiti wa mwaka 2015 wa Asasi ya Twaweza, unaonyesha watoto wanane kati ya 10 (asilimia 81) hawawezi kusoma hadithi ya Kiingereza ya kiwango cha darasa la pili, wengine saba kati ya 10 hawana uwezo wa kufanya kwa usahihi hesabu za kuzidisha za darasa la pili.

Uzalishaji duni wa wakufunzi

Oluoch pia anasema Tanzania haina chuo chochote cha kuzalisha wakufunzi ambao ni walimu wa walimu katika shule za umma. Anasema kinachofanyika ni Serikali kupangia wahitimu wa vyuo vikuu, ambao hawana uzoefu kwenda kufundisha vyuo vya ualimu.

“Unamchukua mhitimu wa UDSM akafundishe walimu Chuo cha Butimba, hajawahi kuwa mwalimu, hajui kuandaa ‘scheme of work’, hajui saikolojia ya mwanafunzi, sasa huyo atamfundisha nini mwalimu?

“Huo ni mgogoro, ilitakiwa Serikali ichambue walimu wenye umahiri, wakawaandae kwa miezi kadhaa kabla ya kuwapa jukumu la kuwa wakufunzi,” anasema.

Kinachosikitisha zaidi, Oluoch anasema wanafunzi wanaopata daraja la tatu na la nne ndio huchukuliwa katika vyuo vya ualimu, hali inayosababisha kufundishwa upya masomo kabla ya kufundishwa mbinu za kufundisha.

Udhaifu katika ukaguzi

Oluoch ambaye ni mwalimu kitaaluma anataja hatua nyingine inayothibitisha janga kuwa ni kukosekana taasisi huru yenye mamlaka ya kisheria ya kukagua, kufungia na kutoa adhabu shule yoyote itakayokuwa chini ya viwango vya ubora wa elimu inayohitajika.

Anatumia mfano wa kisayansi wa pembe tatu ya elimu bora, ambao umekuwa ukitumiwa na mataifa yanayohitaji kufanikiwa katika sekta ya elimu. Pembe tatu hizo ni Taifa kuwa na taasisi ya elimu, taasisi ya kupima mitalaa na taasisi huru ya ukaguzi wa mitalaa.

“Tunayo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Baraza la Mitihani (Necta), ambalo linahusika na kupima mitalaa lakini hatuna taasisi huru ya ukaguzi itakayokuwa tofauti na idara inayosimamia ubora iliyo chini ya wizara, tunataka iwe huru kukagua na kufungia shule,” anasema.

Aibu ya wahitimu vyuoni

Programu Meneja wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Nicodemas Shauri anasema ipo aibu ya Taifa kuzalisha wahitimu wasio na ubora wa kushindana katika soko la ajira.

Ripoti ya Bazara la Vyuo Vikuu Afrika Mashariki (IUCEA) ya 2014, inaonyesha asilimia 61 ya wahitimu wa vyuo vikuu hawakuandaliwa kwa ajili ya ushindani wa soko la ajira baada ya kubainika kuwa na upungufu katika ujuzi unaohitajika.

“Mwanafunzi anapata shahada kwa ‘copy and paste’, kinachoshangaza hata vyuo vilivyotegemewa zaidi kuzalisha wataalamu vimebadilishwa na kuwa vyuo vikuu, mfano Arusha Tech, Moshi Tech kwa hiyo wataalamu wanaingia mtaani wakiwa watupu, wanakosa uwezo wa kujiajiri wenyewe, hili suala linahitaji mjadala wa kitaifa,’’ anasema Shauri ambaye pia ni mkufunzi wa elimu.

Anasema mazingira ya mwanafunzi kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu yanaakisi kuwa elimu ni janga.

Kufifia uzalishaji wanasayansi

Mwenyekiti wa Chama Cha Hisabati Tanzania (MAT/Chahita), Dk Said Sima anakiri elimu ni janga na juhudi za haraka zisipochukuliwa, taifa litaendelea kubaki maskini, akitolea mfano wa tatizo la ufaulu wa somo la hisabati kwa kidato cha nne.

Anasema kwa miaka 10 iliyopita, takwimu zinaonyesha ufaulu wa hisabati nchini ni chini ya wastani wa asilimia 20, tofauti na malengo ya asilimia 31 yaliyowekwa na Benki ya Dunia. “Mwaka 1975 ilikuwa ni asilimia 52, ikashuka hadi asilimia 20 ya sasa, maana yake Taifa litaendelea kuwa na upungufu wa watalaam katika fani za uhandisi, ukandarasi na nyinginezo, licha ya kukosekana takwimu lakini uhaba kwa sasa ni mkubwa katika fani hizo,” anasema.

Ushiriki mdogo wa mzazi

Sima anasema mzazi ana nafasi kubwa kufuatilia elimu ya mtoto lakini wazazi wengi wameshindwa kutumia nafasi hiyo badala yake wanaishia kuilalamikia Serikali.

“Mzazi au mlezi akiwa nyumbani anatakiwa kudhibiti muda wa mwanafunzi anavyoutumia lakini hata anapokwenda shule unafuatilia? Mfano mwanafunzi anasoma mbali, mzazi unatakiwa kufuatilia anafika shule? Je anasoma? Anazingatia vipindi? Ufaulu wake ukoje?

Katika mkutano wa wadau wa elimu ulioandaliwa mwaka jana na TenMet, meneja wa kitengo cha Uwezo kutoka Twaweza, Zaida Mgalla alisema wazazi wana nafasi kubwa kuhakikisha watoto wao wanafanya vizuri darasani na hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.

Alitolea mfano utafiti wa Uwezo wa mwaka 2015 ulionyesha asilimia 70 ya watoto wanaofaulu, ni wale ambao mama zao wamesoma walau elimu ya sekondari. Utafiti huo ulibaini asilimia 29 ya watoto ni watoro.

“Mtoto hadi anamaliza elimu ya msingi mzazi hujui chochote, ufaulu wa mwanafunzi unategemea ushirikiano wa kila mmoja,” alisema.

Ufuatiliaji hafifu wa mtoto shuleni pia umechangia ongezeko la mimba za utotoni.