Rais wa Zimbabwe aandaa kiama cha mafisadi

Muktasari:

Muda huo wa miezi mitatu utakapokuwa umeisha, serikali itaanza kuwakamata na kuwatia ndani wote ambao watakuwa hawajatekeleza agizo hilo na tutahakikisha wanashtakiwa kwa kuzingatia sheria za nchi.

Harare, Zimbabwe. Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ametangaza msamaha wa miezi mitatu kwa watu binafsi au mashirika waliofisidi fedha au mali kurejesha vinginevyo watakabiliwa na mashtaka.

“Serikali ya Zimbabwe imetangaza gazetini katika muda wa miezi mitatu waliohusika na vitendo vya uhalifu wa kiuchumi wanapaswa kurejesha fedha na mali na wala hawataulizwa maswali yoyote wala kufunguliwa mashtaka,” imesema taarifa ya Rais Mnangagwa ambaye ameanzisha juhudi za kufufua uchumi ulioharibiwa.

Msamaha huo, kwa mujibu wa tangazo hilo utaanza Desemba Mosi.

“Muda huo wa miezi mitatu utakapokuwa umeisha, serikali itaanza kuwakamata na kuwatia ndani wote ambao watakuwa hawajatekeleza agizo hilo na tutahakikisha wanashtakiwa kwa kuzingatia sheria za nchi,” alisema.

Mnangagwa, aliyeapishwa Ijumaa iliyopita kuchukua nafasi ya Robert Mugabe baada ya jeshi kuingilia kati, amesema katika operesheni waliyofanya wamegundua kwamba kiasi kikubwa cha fedha kimetoroshewa nje. Operesheni ya kijeshi iliyoshuhudiwa vifaru vikiranda mitaani na kuhitimisha utawala wa Mugabe ilisaidia kuchimbua “matukio kadhaa ambapo kiasi kikubwa cha fedha na mali vilipelekwa nje na watu binafsi au mashirika,” alisema.

“Vitendo hivyo viovu vimechangia pakubwa uhalifu wa kiuchumi dhidi ya Wazimbabwe na kamwe serikali ya Zimbabwe haitafumbia macho.”

Zimbabwe inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na katika miezi ya hivi karibuni mabenki yamebaki na kiasim kidogo au hakuna fedha kabisa.

Mnangagwa, 75, ameapa kupambana na ufisadi, kulinda uwekezaji wa kigeni, kutengeneza nafasi au fursa za ajira katika juhudi za kuujenga upya uchumi ulioharibika.