Magari manne ya mafuta yawaka moto

Muktasari:

Ni Rusumo mpakani mwa Tanzania na Rwanda

Ngara. Magari matano ya mizigo yameteketea kwa moto katika kituo cha forodha Rusumo Wilaya ya Ngara mkoani Kagera mpakani mwa Tanzania na Rwanda baada  ya gari la mafuta ya petrol kuligonga gari jingine na kupoteza mfumo wa breki.

Kwa mujibu wa shuhuda Chrispine Kamugisha amesema gari la mafuta lilikuwa likiingia katika lango la forodha Rusumo na kupoteza mfumo huo na baada ya kugonga lingine moto ulilipuka na kusababisha mengine kupatwa moto huo na hakuna juhudi yoyote ya kuzima moto kwa kuwa ni mkali.

Kamugisha amesema wananchi waliokuwa wakielekea makanosani wamesambaza taarifa za ajali hiyo na limefika jeshi la polisi kituo cha Rusumo na Kasulo kuondoa watu eneo la tukio huku madereva waliokuwa na magari eneo hilo wameyasogeza mbali.

"Eneo hili lina mteremko mkali kuingia sehemu ya maegesho kufanya clearing kwenye ofisi za hapa hivyo hakuna kinachofanyika kuzima  moto huo hivyo serikali ichukue hatua kuweka zimamoto kwa wilaya yetu," amesema Kamugisha

Matukio ya ajali ya magari katika kata ya Rusumo yamekuwa yakitokea mara kwa mara baada ya magari kupoteza mfumo wa breki katika barabara iendayo nchini Rwanda kutokana na miteremko mikali na kona nyingi ambapo husababisha vifo majeruhi na kuteketea kwa mali mbalimbali.

Kamanda wa polisi wilayani Ngara, Abeid Maige amethibitisha  kupokea taarifa za ajali hiyo na kwamba anaelekea huko baada ya wenzake kutangulia walio jirani na eneo.

Hata hivyo, mkuu wa wilaya ya Ngara, Luteni Kanali Michael amesema ukosefu wa zimamoto ni changamoto kubwa wilayani Ngara kutokana na matukio ya ajali ya moto kuongezeka na ombi lilishatumwa serikalini lakini utekelezaji wake haujafikiwa.