Magufuli: Hii ndiyo sababu ya kumteua Mpina

Muktasari:

  • Pia alisema alikuwa akiwahamasisha wananchi wa jimbo lake kutochunga mifugo yao kwenye hifadhi.

Meatu/Dar. Rais John Magufuli ametaja sababu ya kumteua Luhaga Mpina kuwa waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwamba ni kwa kuwa anatoka kwenye jamii ya wafugaji.

Pia alisema alikuwa akiwahamasisha wananchi wa jimbo lake kutochunga mifugo yao kwenye hifadhi.

Mbali ya Mpina, Rais Magufuli alidokeza kuwa alimteua naibu waziri kutoka Mtwara na katibu mkuu kutoka umasaini ambako kote huku kuna ufugaji na uvuvi.

Rais Magufuli alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi katika ziara yake ya kikazi mkoani Simiyu.

Akiwa katika Kijiji cha Mwandoya, Jimbo la Kisesa wilayani Meatu, Rais alisema alimpa uwaziri Mpina ili akatekeleze sheria.

Alimsifu waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Kisesa akisema anafanya kazi nzuri.

“Mchawi mpe mtoto akulelee. Nilimpa uwaziri ili akatekeleze sheria ya uvuvi. Mmeniletea mchapakazi, anatekeleza sheria,” alisema Rais Magufuli.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri Mpina alizungumzia tatizo la tembo kuvamia na kuharibu mashamba ya wananchi na kutishia usalama wao.

Pia, aliomba wilaya hiyo kuwa halmashauri na kujengewa barabara kwa kiwango cha lami ambayo itaunganisha jimbo hilo na wilaya nyingine za jirani.

Akijibu maombi hayo, Rais Magufuli alisema suala la kuanzisha halmashauri ya Kisesa halitawezekana kwa sasa kwa sababu kuna hesabu zake.

“Tukianza kugawa halmashauri, kila jimbo litataka kuwa halmashauri. Jambo hili ni zuri lakini inawezekana siyo kwa sasa.

“Tuache tushughulike kwanza na barabara, maji na hospitali. Ngoja tufanye haya muhimu zaidi. Tumbane mkurugenzi wa Halmashauri ya Meatu afanye kazi ili watu wa huku nao wanufaike,” alisema Rais Magufuli.

Kuhusu hoja ya tembo kuvamia makazi, Rais alisema amelichukua suala hilo na Waziri Mpina pamoja na mawaziri wenzake wanaohusika watajadiliana namna ya kutatua changamoto hiyo.

“Tembo tunawahitaji, mazao tunayahitaji, wananchi tunawahitaji, lakini tutalishughulikia,” alisema.

Aidha, Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo kuhakikisha kilomita tatu za barabara katika Wilaya ya Meatu zinajengwa haraka iwezekanavyo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake.

Akiwahutubia wananchi wa Meatu, Rais Magufuli alishangaa kuona barabara hiyo haijakamilika na kumtaka waziri huyo kutafuta fedha kokote ili mchakato wa ujenzi ifikapo mwezi ujao.

“Nataka kuona mkandarasi ameanza kazi. Nataka kuona kilomita tatu nilizoahidi zinakamilika mwaka huu. Siwezi nikatoa ahadi halafu isitekelezwe wakati niliowateua wapo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema; “Najua watasema wanafanya upembuzi yakinifu na usanifu, unafanya upembuzi gani kwenye kilomita tatu wakati barabara inajulikana unapita wapi. Kachukueni contractor (mkandarasi) yeyote aanze kazi.”

Mtazamo wake kuhusu uzazi

Akizungumzia masuala ya uzazi, Rais Magufuli aliwahimiza Watanzania kuchapa kazi kwa bidii na kuendelea kuzaliana kwa wingi wakiwa na uhakika wa chakula.

Alisema hayo alipokuwa akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Meatu wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa majengo uliofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA).

Alisema yeye si muumini wa kupunguza uzazi na akiwa mwananchi ana uwezo wa kuzalisha, haoni sababu ya kuambiwa asizae.

“Kinachotakiwa ni kwa Watanzania kuchapa kazi ili watoto utakaowazaa uwalishe. Wale ambao hawafanyi kazi, wavivu ndiyo watakaopanga uzazi. Wakati mwingine uzazi unakataa, utazaaje wakati una njaa?” alisema Rais Magufuli huku wananchi wakiangua vicheko.

Alitolea mfano wa nchi moja ambayo asilimia 60 ya watu wake ni wazee wa kuanzia miaka 60 hadi 100 akisema ilikuwa na sera ya kuzaa mtoto mmoja lakini sasa wanapata shida na vijana hawataki kuzaa.

“Watu wameingizwa mawazo ya ajabu ya uzazi wa mpango na kupangiwa mambo ya kufanya na watu wa mataifa mengine.

“Limeni, fanyeni kazi. Ukiwa na chakula cha kutosha zaa. Taifa lisipokuwa na watu wa kufanya kazi, Taifa hilo halipo. Tunahitaji nguvu kazi ya Taifa letu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Serikali haitatoa chakula cha bure kwa yeyote atakayesema ana uhaba akirejea maneno ya Biblia yasemayo, “Asiyefanya kazi na asile.”

Aliwataka wakazi wa Meatu kulima kwa bidii ili wajenge nchi yao badala ya kusubiri wageni.

Katika hotuba yake aliyokuwa ‘akichomekea’ lugha ya Kisukuma, Rais Magufuli aliwataka wakazi wa Meatu kufikiria kufuga kisasa ili wanufaike na mifugo yao.

Aliwataka watumie mifugo yao kujiondolea umaskini badala ya kuona fahari wakati wanaishi maisha duni.

“Ukiwa na ng’ombe wengi, uza wachache, jenga nyumba ya bati, jenga rambo la mifugo yako, hayo ndiyo maendeleo,” alisema Rais Magufuli huku akiiagiza Wizara ya Mifugo kujipanga kutumia rasilimali hizo.

Akizungumzia hospitali ya Wilaya ya Meatu, Rais Magufuli alisema Serikali iliamua kuongeza bajeti ya idara ya afya kwa sababu ya kukabiliwa na changamoto nyingi hasa ya uhaba wa dawa.

“Kila nilipokuwa ninakwenda nakuta wananchi wanalalamikia upungufu wa dawa na wahudumu, sasa tumeamua kuimaliza kero hii, wananchi muwe na amani,” alisema Rais.

Alisema wafanyakazi wa sekta ya afya wanafanya kazi kubwa na nzuri, hivyo wanastahili kupandishwa madaraja hasa kwa wale wanaostahili kusudi malalamiko ya kutopandishwa madaraja yaliyokuwapo awali, yaishe.