Magufuli aongoza maelfu kuomboleza askari wa JWTZ waliouawa DRC

Muktasari:

  • Kabla ya kuanza kutoa hotuba yake kwenye Uwanja wa Jamhuri, Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, aliwaomba wananchi kusimama kwa dakika moja kuwaombea askari hao waliouawa na kikosi cha waasi cha ADF.

Rais John Magufuli jana aliwaongoza maelfu ya Watanzania na wageni waalikwa waliohudhuria sherehe za miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania kuwaombea askari 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa na waasi huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Kabla ya kuanza kutoa hotuba yake kwenye Uwanja wa Jamhuri, Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu, aliwaomba wananchi kusimama kwa dakika moja kuwaombea askari hao waliouawa na kikosi cha waasi cha ADF.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres alisema juzi kuwa wanajeshi hao waliuawa katika kambi iliyopo Mashariki mwa Congo.

Katika shambulio hilo, askari wengine 44 walijeruhiwa, wanane kati yao wakiwa mahututi na wawili walipotea baada ya kambi yao kuvamiwa.

Mbali ya vifo hivyo, Oktoba mwaka huu, askari wawili waliuawa na waasi wakati wakilinda amani nchini humo. Askari hao ni Koplo Maselino Paschal Fubusi na Praiveti Venance Moses Chimboni. Wengine 12 walijeruhiwa katika shambulio hilo.

Mei 2015, askari wengine wawili waliuawa na wengine 13 kujeruhiwa baada ya msafara wao kushambuliwa kwa roketi na waasi.

Askari mwingine, Khatibu Mshindo aliuawa Agosti 2013 katika shambulio la bomu lililofanywa na waasi wa Kikundi cha M23 kwenye Mji wa Goma ulioko Mashariki mwa DRC.

Baada ya kupokea taarifa za tukio hilo usiku wa kuamkia jana, Rais Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, maofisa na askari wote wa JWTZ, familia za marehemu na Watanzania wote.

Alisema, “Nimeshtushwa na kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na mashujaa waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa majirani zetu DRC,” ilieleza taarifa hiyo.

Aliwataka Watanzania kuwa watulivu na kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua zinazostahili baada ya kutokea tukio hilo. Aliwaombea majeruhi wote wapone haraka ili waendelee na majukumu yao ya kawaida.

Mbali na Rais Magufuli, Spika wa Bunge, Job Ndugai alituma salamu za rambirambi kwa Waziri Mwinyi na Jenerali Mabeyo akisema, “Nimepokea kwa masikitiko taarifa hizi za kuuawa kwa askari wetu waliokuwa wanalinda amani huko DRC, hakika hili ni pigo kwa Taifa zima, naungana na Watanzania wenzangu kuwapa pole kwa msiba huo mzito, ninamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za wapendwa wetu mahala pema peponi.”

Spika ambaye pia amewaombea majeruhi wapone haraka, ametoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki waliopoteza wapendwa wao.

Kupitia kurasa wake wa Twitter Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameandika: “Natoa pole kwa familia za askari na Mkuu wa Majeshi ya Tanzania. Ni msiba mkubwa kwa Taifa letu na sote tuwe pamoja na familia na jeshi letu kwa wakati huu.”