Serikali kufanya tathmini mahitaji mita za luku

Muktasari:

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, Dk Merdard Kalemani amesema Serikali itafanya tathmini ya mahitaji ya mita za luku kabla ya kupiga marufuku uagizaji mita hizo kutoka nje ya nchi.

Amesema tathmini hiyo itafanyika kwa siku 90 kuanzia leo Jumamosi Machi 24, 2018 baada ya hapo hakutakuwa na uagizaji wa mita hizo kutoka nje kutokana na uzalishaji ulioanza kupitia viwanda vya ndani.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 24, 2018 wakati wa ziara katika kiwanda cha kutengeneza mita za umeme wa luku cha Baobab Energy System Tanzania (Best).

Kiwanda hicho kimeanza kutengeneza mita za aina hiyo Machi 15, 2018 kikianza na uzalishaji wa wastani wa mita hizo 1000 kwa siku zinazotumika kwa wateja wa kawaida.