Majaliwa aalika wageni wake Dom

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Alisema hayo jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kwenda Dodoma, wakati akipokea msaada wa maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10 kutoka Kampuni ya Huawei, Ubalozi wa Pakistan na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN).

Dar/Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amehamia rasmi Dodoma na kuwaalika wanaotaka kumuona kumfuata makao makuu ya nchi.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam muda mfupi kabla ya kwenda Dodoma, wakati akipokea msaada wa maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10 kutoka Kampuni ya Huawei, Ubalozi wa Pakistan na Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN).

“Natumia fursa hii kuwaaga wananchi wa Dar es Salaam, nawashukuru kwa michango yao ya maafa ya tetemeko la Kagera. Leo nahamia rasmi Dodoma ambako shughuli za Serikali zitakuwa zikifanyika huko. Hata michango ya maafa haya nitaipokelea Dodoma,” alisema Majaliwa.

Uchangiaji wa jana ulikusanya Sh190 milioni na Kampuni ya Huawei kupitia Balozi wa China, ilitoa Sh60 milioni huku ubalozi wa Pakistan ukitoa Sh80 milioni na AKDN Sh50 milioni.