Waziri Mkuu amsimamisha kazi mwanasheria Misungwi

Muktasari:

Mwanasheria wa halmashauri hiyo anatuhumiwa kwa kutotimiza wajibu wake katika kesi iliyohusu deni la halmashauri 

Misungwi. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Alphonce Sebukoto kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuharakisha malipo ya fidia ya Sh279 milioni inayomilikiwa na kampuni ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Anthony Bahebe.

Majaliwa ambaye yuko kwenye ziara ya siku saba mkoani Mwanza amechukua uamuzi huo leo Februari 19 alipokuwa akizungumza na watendaji na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Misungwi.

Kabla ya kuwa diwani na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa halmashauri, Bahebe alikuwa akitekeleza mradi wa maji katika halmashauri hiyo wenye thamani ya zaidi ya Sh300 milioni kupitia kampuni yake ya Seekevim Company Ltd ambayo iliishtaki halmashauri.

“Wewe mwanahseria uliyeajiriwa kwa kazi ya kuitetea halmashauri hukutimiza wajibu wako katika shauri hili kwa sababu licha ya kusema mahakamani kuwa halmashauri haina pingamizi na madai hayo, pia uliharakisha malipo ya fedha hizo ulipokaimu nafasi ya mkurugenzi,” amesema Majaliwa na kuongeza:

"Utasimama kazi kuanzia leo kupisha uchunguzi na ikibainika kweli hukutekeleza ipasavyo majukumu yako, basi utumishi wako utaishia hapo hapo maana Serikali haiwezi kuvumilia kuendelea kuwa na watumishi wa aina hii.”

Waziri Mkuu ameonyesha mshangao kwa mwenyekiti wa halmashauri kuishtaki na kuidai fidia halmashauri anayoiongoza hadi kuchukua mamilioni ya fedha ambazo zingetumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Hata kama shauri hili lilifunguliwa kabla hajagombea udiwani na kuwa mwenyekiti; baada ya kushika wadhifa huu angetafuta utaratibu mwingine wa kulimaliza suala hili,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini fedha hizo zimelipwa haraka haraka kupitia akaunti binafsi kwenye moja ya matawi ya benki jijini Mwanza.

Ziara hiyo pia haijamwacha salama Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke baada Waziri Mkuu kutangaza kutuma timu maalum ya uchunguzi dhidi ya tuhuma za upotevu wa mamilioni ya fedha zilizotumwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Halmashauri ilipata Sh548 milion kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa daraja lakini zaidi ya Sh50 milioni hazijulikani zimefanya nini,” amesema Majaliwa.

Ametaja fedha nyingine ambazo hazijulikani zilipo na zitakazochunguzwa kuwa ni Sh325 milioni ambazo ni kati ya Sh665 milioni zilizotumwa kwa ajili ya miradi ya Rivemp unaosaidia uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya Bonde la Ziwa Victoria.

"Nitaleta watu kuchunguza fedha hizi ambazo zinadaiwa kubadilishiwa matumizi badala ya kutekeleza miradi iliyokusudiwa,” amesema Waziri Mkuu.