Majaliwa awataka ma-DC kuzifanyia tathmini mali za halmashauri

Muktasari:

  • Ametoa kauli hiyo leo Agosti 17, 2018 mkoani Tabora

Tabora. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa wilaya nchini kushirikiana na madiwani katika halmashauri zao kufanya tathmini ya mali zote zinazomilikwa na halmashauri vikiwemo vibanda vya biashara ili kujiridhisha kama viwango vinavyotozwa vinalingana na hali halisi ya uchumi kwa sasa.

Amesema licha ya tathmini hiyo kuwawezesha kufahamu viwango vinavyotozwa, pia itasaidia halmashauri kubaini watu wa kati ambao wanawatoza wafanyabiashara fedha nyingi na kuilipa halmashauri fedha kiduchu, jambo linalochangia kuikosesha Serikali mapato inayostahili.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Agosti 17, 2018 wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya mji wa Nzega na wa halmashauri ya Wilaya ya Nzega pamoja na madiwani katika ziara yake ya kikazi wilayani Nzega, Tabora.

Ametoa agizo hilo baada ya mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe kuomba Serikali iingilie kati mgogoro uliopo baina ya halmashauri na wafanyabiashara kuhusu mradi wa vibanda vya biashara katika eneo la Soko Kuu la Nzega.

Amesema vibanda  hivyo vimejengwa na wafanyabiashara katika ardhi ya halmashauri kwa makubaliano ya kulipa kodi.

Uongozi wa halmashauri ya Mji wa Nzega uliamua kupitia upya mkataba wa mradi huo kwa sababu ulikuwa hauinufaishi, hivyo ilianzisha mpango wa maboresho ambapo ilibaini kuwepo kwa watu wa kati waliokuwa wakiwatoza wafanyabiashara zaidi ya Sh 150,000 kwa mwezi na kuilipa halmashauri  Sh30,000 kwa mwezi.

Pia, ilibaini baadhi ya wamiliki wa awali wa vibanda waliviuza kwa wafanyabiashara wengine kwa bei kubwa bila ya kuishirikisha halmashauri na ilivyotaka kuvichukua ili wafanyabiashara waendelee kuwa wapangaji kwa lengo la kuondoa mtu wa kati, ndipo ulipoibuka mgogoro wa umiliki wa vibanda hivyo.

Waziri Mkuu amesema migogoro ya aina hiyo huwa haiishi kwa wakati katika maeneo mengi kwa sababu baadhi ya vibanda hivyo vinamilikiwa na wakuu wa idara, madiwani na baadhi ya watumishi katika halmashauri husika, jambo linalozikosesha halmashauri mapato.

Pia, amezishauri halmashauri zinazomiliki vibanda vya biashara hususani kwenye maeneo yenye migogoro watumie leseni za biashara zinazofanyakazi kwa kuzitambua na kuingia mikataba na wamiliki wake ili kuondoa uwepo wa mtu wa kati.

Waziri Mkuu pia amewataka watumishi wa umma wanaomiliki vibanda vya biashara kwenye eneo hilo watoe taarifa za umiliki wao ili kuondoa mgongano wa kimaslahi pindi wanapokuwa kwenye vikao vya kujadili namna bora ya kuipatia ufumbuzi migogoro ya vibanda vya biashara vinavyomilikiwa na halmashauri katika maeneo yao.