Aina ya sera, matumizi ya umma huchangia maendeleo kiuchumi

Muktasari:

  • Hali ya uchumi huathiri nyanja nyingine za maisha kama vile siasa, jamii hata usalama. Yapo mambo mengi yanayochangia maendeleo ya kiuchumi kwa kila nchi.

Kati ya mambo yanayojadiliwa zaidi duniani ni maendelo ya uchumi ambayo ni muhimu kwa kila mtu, kaya, taasisi, nchi na ulimwengu kwa ujumla.

Hali ya uchumi huathiri nyanja nyingine za maisha kama vile siasa, jamii hata usalama. Yapo mambo mengi yanayochangia maendeleo ya kiuchumi kwa kila nchi.

Kati ya mambo haya yenye mchango ni aina ya sera za uchumi katika nchi husika. Sera hizi ni zile za fedha na kodi. Hali ya uchumi pia hutegemea aina ya matumzi ya umma yanayofanywa.

Sera

Sera za fedha ni muhimu katika kuchochea na kusisimua uchumi kwani huhusisha riba inayotozwa na taasisi za fedha kwenye mikopo inayotolewa. Sera pana za fedha huwa na riba ndogo kwa wakopaji.

Riba ni bei ya mkopo inayolipwa na mkopaji. Inapokuwa chini, hurahisisha ukopaji kwa ajili ya uwekezaji na matumizi ya kawaida. Yote haya ni afya kwa kuchochea na kusisimua uchumi.

Ili kuwa na riba ndogo mambo kadhaa ni muhimu. Haya ni pamoja na sera pana za fedha kutoka kwa mamlaka ya fedha katika nchi husika. Kwa Tanzania kwa mfano, mamlaka hii ni Benki Kuu (BoT). Sera pana hupunguza riba inayolipwa na benki za biashara zinapokopa kutoka Benki Kuu ili nazo zikopeshe wateja wao.

Nchini, mwanzoni mwa mwaka jana riba ilipunguzwa kutoka asilimia 16 hadi 12. Agosti mwak ahuo huo, riba ilishuka tena kutoka asilimia 12 hadi tisa.

Pia mamlaka za nchi huweza kuongeza fedha katika mzunguko. Zote hizi ni hatua za kisera kuhakikisha upatikanaji wa mikopo na kwa riba ndogo. Hata hivyo riba ndogo pekee haitoshi kushawishi wakopaji kukopa. Yapo mambo mengine ambayo lazima yaambatane na riba ndogo ili kusisimua na kuchochea uchumi. Baadhi ya mambo haya yanaainishwa hapa.

Sera za kikodi

Kwa lugha rahisi, kodi ni makato yanayofanywa na mamlaka husika kutoka kwenye mauzo na kipato. Zipo aina nyingi za kodi kama vile ya mapato, ya ongezeko la thamani au ya zuiyo.

Kodi ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato ya nchi yanyaotumika kugharimia bidhaa na huduma za umma kama vile afya, elimu, maji, ulinzi, usalama na miundombinu ya usafiri na uchukuzi.

Kiwango cha kodi hutegemea sera za nchi ambazo zinaweza kuwa za kupanua uchumi au za kuufanya usinyae. Sera za kupanua uchumi huwa chache za zenye viwango vidogo.

Idadi ndogo na aina chache za kodi huchochea na kusisimua uchumi. Hii ni kwa sababu sera za aina hii hubakiza kiasi kikubwa cha fedha mikononi mwa walipa kodi ambao ni pamoja na kampuni, taasisi, kaya na watu binafsi.

Kwa kadiri fedha nyingi zinavyobaki mikononi mwa mwa wananchi kwa maana ya aina chache na viwango vya chini ndivyo uchumi unavyoweza kuchochewa na kusisimuliwa kwa haraka.

Kinyume cha sera pana ni sera zinazominya uchumi. Hizi ni sera banifu za kikodi pamoja na mambo mengine, huwa na viwango vikubwa na aina nyingi za kodi.

Pamoja na kodi, ruzuku ni muhimu katika kutekeleza sera za kodi katika upana wake. Ruzuku ni fedha inayotolewa na Serikali kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho. Ruzuku huchochea na kusisimua uchumi.

Hivyo, kama mamlaka zinataka kuimarisha uchumi na kuufanya kuwa endelevu ni vema zikatumia sera za kodi za kuupanua uchumi.

Matumizi

Kati ya mbinu za kusisimua na kuchochea shughuli za uchumi za uzalishaji bidhaa na huduma ni matumizi ya sekta ya umma inayojumuisha Serikali kuu na zile za mitaa.

Matumizi haya yanajumuisha shughuli za maendeleo na kawaida. Shughuli za kawaida ni zile za uendeshaji wa ofisi wa kila siku, mishahara ya watumishi, semina na safari mbalimbali.

Shughuli za maendeleo ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya aina zote kama vile barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege. Kinachofanya kuchochewa na kusisimka kwa uchumi kupitia matumizi ya umma ni uingizaji wa fedha kwenye mzunguko.

Popote duniani, Serikali ni miongoni mwa walaji wakubwa wa huduma na bidhaa hivyo kadri inavyozidi kutumia ndivyo inavyochochea na kusisimua uchumi kwa kuongeza fedha katika mzunguko. Sehemu ya fedha hizi ni zile zitokanazo na kodi.

Serikali inapotumia hulipa watu na kampuni na kuchochea matumizi hivyo kuhamasisha uzalishaji, kuchochea ajira, kuimarisha kipato na matumizi ya wananchi kwa ujumla. Ni muhimu kwa Serikali popote duniani kutumia kwa umakini ili kufanikisha hili.

Sekta binafsi

Kama ilivyo kwa Serikali, matumizi ya sekta binafsi nayo ni muhimu kwa uchochezi wa uchumi. Sekta binafsi ni pana ikihusisha ya ndani na ya nje; rasmi na isiyo rasmi; ndogo, ya kati na kubwa.

Matumizi ya sekta binafsi katika uwekezaji wa upanuzi wa vitega uchumi hulazimisha ajira kutokea katika minyororo mingi na mirefu ya thamani na mafundo yake.

Ajira hizi huleta kipato ambacho huchochea na kusisimua uchumi kupitia ununuzi wa huduma na bidhaa mbalimbali. Hivyo ni muhimu kuwapo kwa mazingira rafiki, wezeshi na ya kuvutia kwa sekta binafsi kukua na kusisimua uchumi.