Saturday, June 30, 2018

Kazi zinazosigana na maadili zina historia ndefuAnko Kitime

Anko Kitime 

By ANKO KITIME

Katika siku za karibuni wimbi la nyimbo na video zimewaingiza wasanii kadhaa kwenye matatizo baada ya kuonekana haziendani na maadili ya jamii zetu.

Hakika kwa mwendo na taratibu zilizopo, hali hii itazidi kuongezeka. Hali hii siyo Tanzania peke yake, bali vijana kutoka pande zote za Afrika wanajiunga katika wimbi la kutunga nyimbo ambazo zinawaweka katika ugomvi na mamlaka mbalimbali.

Nchini Ghana, vituo kadhaa vya luninga ikiwemo GhOne Tv vimeikataa video ya wimbo Budum Budum ya msanii Vybrant Faya, hali ambayo imemfanya msanii huyo kulalamika kuwa hatua ni kali mno na wimbo wake usingekataliwa bali ungekuwa unapigwa usiku.

Wakati huohuo huko Nigeria, taasisi yake ya utangazaji imeupiga marufuku wimbo wa ‘Don’t Stop’ wa msanii Olamide kwa kudaiwa kuwa na maneno machafu na pia wasanii katika video hiyo walikuwa wakitumia ishara ambazo ni wazi ziliashiria mambo yasiyo na staha.

Wanamuziki wengine wa Nigeria waliowahi kukumbana na rungu la taasisi hiyo ni Wizkid, Phyno, Davido, Inyany na, Reminisce.

Bahati mbaya hawa ndio vioo vya wasanii wetu wachanga. Huko Kenya wimbo ‘Same Love Remix’ wa wasanii Art Attack na Nicole Francis Kutoto ulipigwa marufuku kwa kuhamasisha mapenzi ya jinsi moja.

Hata huko Uganda, msanii wa kike Jemimah Kansiime maarufu kwa jina la Panadol wa Basaja alijikuta akikumbana na mkono wa sheria kwa kuonekana kavunja sheria zinazokataza utupu hadharani kwa kutengeneza video ambayo alionekana kavaa nusu uchi iitwayo Ensolo Yange.

Waziri wa maadili wakati huo alitishia kumfunga jela miaka 10. Kundi la Urban Boyz la Rwanda liliwahi kujikuta kwenye matatizo kwa wimbo wa Ancilla. Wizara ya Michezo na Utamaduni iliamua kupiga marufuku usirushwe hewani na vyombo vya utangazaji.

Hii ni mifano michache ya hali ilivyo katika bara letu. Kati ya sababu zinazotajwa kusababisha hali hii ni ukosefu wa malezi mema kwa vijana wa Afrika, wazazi wakilaumiwa kwa upande mmoja kwa kuacha jukumu lao la kufundisha maadili stahili na Serikali nyingi zikipuuza wizara za utamaduni kwa kuona kuwa hazina tija, wakati ni zenye dhamana ya kulinda maadili.

Jambo hilo liliacha mwanya wa kuingia kwa kasi maadili mapya kupitia kisingizio cha utandawazi na kuathiri vijana wengi ambao sasa wanaona utamaduni wa Magharibi ndio utamaduni bora.

Wafanyabiashara wa kazi za sanaa wamechukua nafasi na kuwa walimu wa maadili mapya ili kupata masilahi, kwa maelezo kuwa aina ya sanaa hizi ndizo zenye soko kwa sasa.

Lakini pia ieleweke kuwa kutoa kazi ambazo zimekuwa zikikiuka maadili siyo jambo geni, pengine tofauti imekuwa ni sababu au kipimo cha nini ni kinyume cha maadili na pia ukubwa wa adhabu.

Adhabu ya kifungo kwa waliokiuka maadili ziliwahi kutolewa, tena bila kujali umaarufu wa msanii. Katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, mwaka 1978, Bendi ya TP OK ilitoa nyimbo mbili zilizokuwa tungo za Franco Luambo Makiadi aliyekuwa kiongozi na mwanamuziki maarufu. Mwanamuziki huyo alitoa santuri za nyimbo za ‘Helene’ na ‘Jacky’. Nyimbo hizo zilileta matatizo makubwa kwa Franco na alipatikana na makosa kadhaa.

Kosa la kwanza alilofanya ni kuvunja sheria iliyomlazimisha kila mwanamuziki kupitisha nyimbo zake kwenye kamati iliyokuwa ikizihakiki kabla ya kuzitoa. Umaarufu wa mwanamuziki huyo wakati huo pengine ulimfanya ajione yuko juu ya sheria, hakufuata taratibu hizo.

Kosa la pili ni kuwa maneno yaliyotumika katika nyimbo hizo yalikuwa ni matusi ambayo hata leo, miaka 38 baadaye nyimbo hizo bado zimepigwa marufuku.

Mwanasheria Mkuu nchi hiyo wakati huo, Kengo wa Dondo alipomuita na kumuuliza Franco kwa nini alitunga nyimbo chafu, alijitetea kuwa hazikuwa na tatizo lolote.

Ilipochukuliwa hatua ya kumwambia mama yake Franco asikilize nyimbo zile na kutoa mawazo yake, inasemekana Franco mwenyewe alisihi asizikilize. Pia kuna maelezo kuwa alisikiliza na kupigwa na butwaa, lakini hatimaye Franco alishtakiwa na kukutwa na hatia na kufungwa miezi mitatu na wanamuziki wake 10 akiwemo Simaro Lutumba.

Mara kadhaa Franco alikumbwa na adha ya kusigana na Serikali japo mara mbili alipata mikasa kutokana na sababu za kisiasa. Mwaka 1959, Franco alifungwa jela miezi miwili kutokana na uendeshaji mbaya wa gari. Wakati akiwa gerezani pia kuna mwanamuziki mwingine wa OK Jazz aliyekuwa mpiga tarumbeta. Wawili hao walitunga wimbo wa Mukoko uliozungumzia uhuru wao, wakiwa na maana uhuru kutoka gerezani. Baada ya kutoka gerezani na kuurekodi, Serikali ya kikoloni iliutafsiri kama wimbo uliokuwa unahamasisha uhuru, haraka sana ukapigwa marufuku usirushwe hewani wala kuuzwa.

Mwaka 1965, Rais wa Congo wakati huo Mobutu Seseseko aliamuru wapinzani wake watano wauwawe hadharani. Franco aliyeshuhudia mauaji hayo akarekodi wimbo ulioitwa Luvumbu Ndoki unaoweza kutafsiriwa kama ‘Mchawi Luvumbu’. Huu ulikuwa wimbo wa Kicongo uliokuwa ukiimbwa kumsimanga mtu aliyeua nduguze au watu wa karibu, na ulitokana na Chifu Luvumbu aliyekuwa akitoa kafara ndugu zake ili aweze kufanikiw.

Serikali ikitafsiri kuwa ule wimbo ulitokana na mauaji yaliyoamriwa na Mobutu. Franco aliwekwa kizuizini kwa muda na nakala za wimbo zikaanza kukamatwa.

-->