Lima nyanya kisasa-1

Muktasari:

  • Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalolimwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo.

Nyanya ni zao la mboga linalolimwa sehemu nyingi duniani kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na pia kama zao la biashara. Nyanya ni aina ya mboga inayozalishwa kwa wingi sana duniani.

Kwa Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalolimwa na kuliwa kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu katika kila mlo.

Kulingana na umuhimu wa zao hili kama chakula na pia kama zao linalomwingizia kipato mkulima, kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wake.

Maeneo yanayolima nyanya

Inadhaniwa kuwa asili ya nyanya ni nchi ya Peru au Equador huko Amerika ya Kusini. Mmea huu ulianza kuzalishwa kama zao katika nchi ya Mexico na baadaye kusambaa katika nchi nyingine za ulimwengu. Nchi zinazolima nyanya kwa wingi duniani ni pamoja na Marekani, Italia na Mexico.

Kwa upande wa Afrika, nyanya hulimwa Malawi, Zambia na Botswana. Zao hili hulimwa pia katika nchi za Afrika Mashariki. Kwa upande wa Tanzania mikoa inayolima nyanya kwa wingi hasa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na biashara ni pamoja na Kilimanjaro, Arusha, Morogoro, Iringa, Tanga, Mbeya na Singida.

Mazingira yanayofaa kwa kilimo cha nyanya

Nyanya hustawi vizuri zaidi kwenye mazingira ya joto la wastani kuanzia nyuzi joto 18-27 sentigreti. Mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa ya ukungu kama vile Baka jani chelewa.

Udongo

Nyanya hustawi kwenye aina zote za udongo kuanzia udongo wa kichanga, mweupe wa tifutifu hadi udongo wa mfinyanzi, ili mradi uwe na mboji ya kutosha na usiotuamisha maji. Pia uwe na uchachu wa wastani yaani pH 6.0 hadi 7.0.

Mwinuko

Nyanya hustawi vizuri kutoka sehemu za mwambao hadi kwenye mwinuko wa mita 400-1500 kutoka usawa wa bahari; yaani nyanda za chini kati hadi za juu kutoka usawa wa bahari. Nyanya zinazopandwa nyanda za juu sana hukumbwa na mvua za mara kwa mara ambazo huambatana na magonjwa ya jamii ya ukungu; kama Bakajani chelewa.

Aina za nyanya

Kutokana na tabia ya ukuaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:

1.Aina ndefu: Aina hizi hufanya vizuri zaidi zinapopandwa ndani ya shamba kitalu (green house). Uvunaji wake ni wa muda mrefu. Zipo ambazo zinavunwa hata zaidi ya miezi sita. Mfano wa aina hizi ni ANNA F1, Tengeru 97, Marglobe (M2009).

2.Aina fupi: Mfano wa aina hizi za nyanya ni Tanya, Cal J, Mwanga, Onyx, Roma VF (nyanya mshumaa).

Aidha, kulingana na uchavushaji, nyanya zinagawanyika katika makundi mawili:

1. OPV (Open Pollinated Variety) - Hizi ni aina za kawaida

2. Hybrid - Chotara: Hizi ni nyanya zilizoboreshwa, aina hii zina mavuno mengi, kati ya hizo zipo aina fupi na ndefu.

Hata hivyo, katika karne hii ya 21, nyanya zinazopendelewa kulimwa zaidi na wakulima, ni zile zinazoweza kuvumilia magonjwa, zinazozaa sana na zenye ganda gumu, ili kufanikisha usafirishaji, na kuhifadhika kwa siku nyingi bila kuharibika mapema.

Imeandaliwa na Mogriculture ambao ni wataalamu wa kilimo na ufugaji. 0655-570-084 www.mogriculture.com