Ubunifu kuboresha huduma za fedha ufike vijijini

Muktasari:

  • Kwa kutambua kuwa uchumi endelevu unategemea sekta imara ya fedha, wadau hawa wamekuwa mstari wa mbele kutu-mia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kufikisha huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na benki, taasisi za fedha na kampuni za simu kuboresha huduma za fedha, wataalamu wanasema mikakati inahitajika kuwafikia wananchi wengi waliopo vijijini.

Kwa kutambua kuwa uchumi endelevu unategemea sekta imara ya fedha, wadau hawa wamekuwa mstari wa mbele kutu-mia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kufikisha huduma kwa wananchi wengi zaidi.

Wakati takwimu za Mfuko wa Kuen-deleza Huduma za Fedha Tanzania (FSDT) zikionyesha kuwa ni asilimia 17 tu ya Watanzania wanatumia huduma za fed-ha nchini, mbinu kadhaa za kupunguza changamoto zilizopo inatekelezwa.

Pamoja na hayo yote, mchumi na mha-dhiri mwandamizi wa Chuo cha Biashara (CBE), Dk Dickson Pastory anasema benki zinahitaji kwenda vijijini waliko wananchi wengi zaidi.

Anasema ukiangalia kinachofanywa na benki za biashara pamoja na kampuni za simu ni kujitofautisha sokoni kwa wateja wale wale jambo ambalo haliongezi watu-miaji wa huduma hizo kwa kiasi kikubwa.“Bila benki, kampuni za mawasiliano haziwezi kutoa huduma za fedha. Wakala anahitaji kuweka fedha kufanikisha mia-mala ya wateja.

Benki zielekee vijijini, kuna watu wengi zaidi. Huko zitaongeza wateja kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Dk Pastory anasema kutokana na juhudi za kupeleka umeme vijijini (Rea) na uima-rishaji wa mtandao wa simu maeneo yasi-yo na mvuto wa biashara, wananchi wengi watashawishika kumiliki simu na kutumi ahuduma za fedha.

Ripoti ya nne ya FSDT iliyotolewa mwaka jana inaonyesha changamoto kadhaa zilizopo ambazo zinachangia wengi kutotumia huduma za fedha.

Miongoni mwa changamoto hizo ni elimu duni. Ripoti inaonyesha Watanzania wanane katika kila 10 wana elimu ya msingi au chini ya hapo hivyo taasisi za fedha kuhitaji umakini wa aina yake zinapoandaa bidhaa kwa ajili ya wananchi.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa robo ya Watanzania wote hawajui kusoma wala kuandikia Kiswahili huku asilimia tatu wakijua kusoma tu.

Hali ikiwa hivyo kwenye Kiswahili, takwimu zinaonyesha ni asilimia 27 pekee ya Watanzania wanajua kusoma na kuandika Kiingereza. Ripoti hiyo inaonyesha asilimia 66 hawajui kusoma wala kuandika ilhali huduma nyingi za fedha hutolewa kwa lugha hiyo.

“Ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi, taasisi za fedha ziangalie ni lugha ipi wateja wao wanapend akuhudumiwa nayo,” inashauri ripoti hiyo.

Licha ya elimu, ripoti hiyo inaonyesha wananchi wengi wanategemea kilimo kuingiza kipato. Kwa maana hiyo, wanapatikana zaidi vijijini zinakofanyika shughuli zao suala linalohitaji ama taasisi za fedha kufungua ofisi huko au kuhakikisha huduma zinafika kwa urahisi zaidi.

Zaidi ya theluthi mbili (asilimia 68) ya Watanzania, ripoti inasema wanategemea chanzo kimoja cha kipato. Wakati asilimia 41 wanategemea kilimo, asilimia 20 wanaendesha maisha kwa kufanya kazi za vibarua na asilimia 18 ni tegemezi kwa ndugu na jamaa zao. Ni asilimia 14 tu wanategemea biashara zao.

Ingawa wananchi wengi wanategemea kilimo kujiingizia kipato, wachache wanaimiliki kwa nyaraka zinazokubalika kwenye taasisi za fedha. Ripoti inaonyesha ni asilimia tatu pekee ya Watanzania wana hati za ardhi au nyumba wanazomiliki hivyo kukosa sifa za kukopesheka kwa kutumia dhamana hizo.

Kutokana na changamoto zilizopo, wananchi wengi hawapati huduma za fedha licha ya uwepo wa zaidi ya benki na taasisi 50 za fedha nchini.

Ripoti hiyo inaonyesha wananchi 22 katika kila 100 wanaoishi vijijini wanakaa zaidi ya kilomita tano kutoka zinapotolewa huduma za fedha hivyo kuwafanya wategemee zaidi simu za mkononi.

Wakati taarifa za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zikionyesha mpaka Juni kulikuwa na watumiaji milioni 41.8 waliosajiliwa, ripoti ya FSDT inabainisha wanaopata huduma za fedha kupitia simu hizo wameongezeka kutoka asilimia asilimia 50 mwaka 2013 mpaka asilimia 60 mwaka jana.

Katika kipindi hicho, matumizi ya huduma za fedha kwa ujumla yamepanda kutoka asilimia 58 mpaka asilimia 65. Ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hatua kadhaa zinachukuliwa na wadau wa sekta ya fedha.

Simu kufungua akaunti

Hivi karibuni Benki ya NMB imezindua mpango unaowaruhusu wateja wapya fursa ya kufungua akaunti kwa kutumia simu ya mkononi.

Kuhakikisha benki hiyo inawafikia wateja wengi zaidi kati ya zaidi ya Watanzania milioni 54.2 waliopo, NMB inawaruhusu wateja wake kutumia NMBApp kwa wanaotumia simu za kisasa au kupiga namba maalum kwa zile za kawaida.

Meneja mwandamizi wa bidhaa za dhamana, Stephen Adili anasema mpango huo utapunguza usumbufu uliokuwapo kwa mteja kwenda kwenye tawi kwa ajili hiyo.

“Huduma hii inapatikana kwa saa 24. Mteja anaweza kufungua akaunti muda wowote kutoka akiwa mahali popote. Namba ya simu ndiyo huwa namba ya akaunti,” anasema Adili.

Ikiwalenga zaidi wananchi wenye kipato cha chini na kati, NMB inatoa siku 90 kwa mteja aliyefungua akaunti kwa njia ya simu kuendelea kufurahia huduma akifanya miamala isiyozidi Shilingi milioni moja.

Na anaweza akaendelea kwa miamala ya mpaka Sh5 milioni lakini zaidi ya hapo atapaswa kupeleka taarifa zake kwenye tawi lolote la benki hiyo lililo jirani yake.

Miamala iliyoboreshwa

Kampuni za simu zinashindana kuboresha huduma zao za fedha. Kampuni ya Halotel ilikuwa ya kwanza kufanya mabadiliko yanayohamasisha huduma zake baada ya kuondoa gharama za kutuma fedha.

Ndani ya miezi miwili tangu kuzinduliwa kwa huduma hiyo, mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa Halotel, Mhina Semwenda anasema kumekuwa na ongezeko la wateja.

“Kwa sasa wateja wanatuomba tuongeze idadi ya mawakala. Unajua wateja wetu wengi wapo vijijini ambako mawakala wengi hawajafika. Kwa sasa tunao mawakala 55,000. Tunatarajia kuboresha huduma zetu kukidhi mahitaji ya wateja,” anasema Mhina.

Takwimu za TCRA zinaonyesha ongezeko la wateja wa Halopesa mpaka asilimia nne katika robo iliyoishia Juni kutoka asilimia tatu waliokuwapo robo ya Machi. Ndani ya kipindi hicho, wateja hao wameongezeka kutoka 547,181 mpaka 756,332.

Miongoni mwa changamoto ambazo zaidi ya wateja milioni 20.85 wa huduma za fedha kwa simu za mkononi waliopo ni kukosea kukamilisha muamala.

Mara kadhaa wateja hukosea namba hivyo fedha walizokuwa wanazituma kwenda kwa mtu mwingine ambaye hakukusudiwa.

Hili nalo limeshughulikiwa. Kampuni ya Tigo yenye takriban wateja milioni saba wa Tigopesa imeboresha huduma yake na sasa mteja aliyekosea kutuma fedha anaweza kusitisha muamala wa alioufanya na kupata fedha zake kwa wakati.

Ofisa mkuu wa Tigopesa, Hussein Sayed anasema baada ya kusikiliza mapendekezo yaliyotolewa wameboresha huduma hiyo ili kuwapa uhuru wa nafsi wateja wao.

“Kuna maalum umewekwa ambao mteja naweza kurudisha fedha aliyotuma kimakosa. Kuondoa uwezekano wa kufanya udanganyifu aliyetumiwa naye anapaswa kuthibitisha kurudishwa kwa fedha husika ili kumuhusu aliyekosea kurekebisha makosa aliyoyafanya,” anasema Sayed.

EAC

Maboresho ya huduma za fedha hayafanywi nchini pekee. Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo inayo mikakati kadhaa inayokusudia kupunguza gharama na kurahisisha miamala inayofanywa na wananchi kutoka kwa wanachama wake.

Ilikuondoa changamoto za kubadili fedha na kupunguza gharama za kutumia mashine za kutolea fedha (ATM), nchi za EAC zimekubaliana kufanya marekebisho ya sheria za fedha ili kushusha gharama za miamala inayofanywa na wananchi wanaotembelea nchi nyingine.

Mpango huo unaihusisha Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda. Wiki iliyopita, wawakilishi wa mataifa hayo walikutana jijini Mombasa, Kenya kuridhia kufanyika kwa utafiti utakaoruhusu wateja wa benki moja kutumia huduma za ATM za benki nyingine katika nchi jirani kwa gharama nafuu.

Utakapoanza kutekelezwa, mpango huo unatarajiwa kuongeza matumizi ya huduma za fedha kwa wananchi wa mataifa hayo.

Ofisa mtendaji mkuu wa Jumuiya ya Benki nchini Kenya (KBA), Habil Olaka anasema: “Ushirikiano wa kutumia miundombinu iliyopo utapunguza gharama za kila muamala jambo litakaloshuhudiwa na wateja wanaovuka mipaka ya nchi zao na kutembelea nchi jirani.”

Mpango huo uliridhiwa na magavana wa benki kuu za mataifa husika tangu Mei 2014 ili kufanikisha miamala kwa wakati kwa kutumia sarafu yoyote ya nchi wanachama lakini kikwazo ni sheria na sera za kuufanikisha.

Kwa sasa wateja wa EAC wanatozwa Dola 2.5 (Sh5,625) kila wanapotumia ATM iliyopo nje ya mipaka ya nchi zao lakini utakapoanza kutekelezwa mpango huo, gharama hizo zitapungua mpaka Dola 0.8 (Sh1,800) kwa kila muamala kwa wale watakaotoka nje au kuingia Tanzania, Kenya, Uganda au Rwanda.