Thursday, July 12, 2018

Unahitajika mwingiliano wa taasisi za utafiti kukuza ufanisi wa viwandaProfesa Honest Ngowi

Profesa Honest Ngowi 

By Profesa Honest Ngowi

Kati ya mambo makuu yanayosisitizwa na Serikali katika maendeleo ni kuwa na uchumi wa viwanda. Hili ni jambo zuri sana kwani litachangia uwezekano wa kuleta na kuongeza ajira, mapato ya Serikali, fedha za kigeni na kukuza sekta nyingine zinazofungamana na viwanda.

Sekta nyingine zina uwezekano mkubwa wa kuwa soko la bidhaa zitakazozalishwa viwandani huku zenyewe zikitoa malighafi kufanikisha uzalishaji.

Kwa ujumla, uchumi wa viwanda unaongeza uwezekano wa kukua kwa pato la Taifa na kupunguza umasikini hasa uliokithiri. Lakini, kati ya mambo muhimu kwa mafanikio ya uchumi wa viwanda ni utafiti.

Kwa lugha nyepesi, utafiti ni kufanya kisichofahamika kifahamike kwa kutumia mbinu za kisayansi. Utafiti unaweza kufanywa kwa marejeo ya taarifa na maandiko ya watafiti wengine ili kujua kilichofanywa na wengine katika eneo husika.

Njia nyingine ni kukutana na wadau wa jambo linalohusika na kuwauliza maswali kwa kutumia njia mbalimbali. Njia bora zaidi ya utafiti ni kuunganisha mbinu hizi mbili.

Utafiti unapaswa kutoa ufahamu na elimu mpya ambayo haikuwapo kabla ya kufanywa kwake. Utafiti unaweza kuwa mdogo, wa muda mfupi na wa kawaida au mkubwa, unaotumia muda mrefu na wa hali ya juu sana.

Utafiti na viwanda

Utafiti ni muhimu katika kuelimisha kuhusu mambo kadha wa kadha yanayohusu jamii. Katika uchumi wa viwanda, utafiti ni muhimu ili kuyafikia malengo yaliyowekwa.

Utafiti unasaidia kujua aina za malighafi zilizopo na zinazohitajika kwa maendeleo ya viwanda na namna ya kuzizalisha. Vilevile, unasaidia kujua ukubwa na aina ya masoko kwa bidhaa za viwandani na uwezo wa wananchi kununua bidhaa husika.

Uchumi wa viwanda Tanzania unalenga kuajiri watu wengi. Utafiti utasaidia kujua hali halisi ya suala hili kadri muda unavyokwenda.

Kufanikisha azma ya uchumi wa viwanda kunahitaji ubunifu katika kuunda na kuzalisha mambo muhimu yanayojumuisha mashine na vipuri vyake, mfumo wa uzalishaji, upokeaji na ufanyiaji kazi uchafu unaotoka viwandani.

Kwa ujumla wake, taasisi zinazofanya utafiti hazina viwanda. Hii ni kwa sababu shughuli kuu za taasisi hizi sio viwanda bali utafiti. Kwa upande mwingine, viwanda vingi hasa vidogo na vya kati havina utaalamu na idara za utafiti.

Hii ni kwa sababu shughuli za msingi za viwanda hivi ni uzalishaji wa bidhaa sio utafiti. Hivyo kunaweza kuwepo ombwe kati ya viwanda na taasisi za utafiti linalopaswa kuzibwa kwa kuunganisha taasisi za utafiti na viwanda.

Mwingiliano

Kuna haja kubwa ya utafiti kutoa mchango wake kwa maendeleo ya viwanda. Ili hili lifanyike ipo sababu ya msingi ya kuwa na mwingiliano kati ya taasisi za utafiti na viwanda.

Taasisi hizi hazipaswi kujitenga na viwanda na viwanda havipaswi kujitenga na taasisi hizi. Matokeo ya vinavyofanywa na taasisi za utafiti yanapaswa kuhabarisha uamuzi unaopitishwa viwandani.

Kwa maana hiyo, taasisi za utafiti zinapaswa kuzalisha na kufanya utafiti unazohitajika viwandani. Matokeo ya utafiti yanapaswa kukidhi mahitaji ya viwanda ambavyo wamikili wake hawana budi kuwataarifu watafiti kuhusu mahitaji waliyonayo.

Kusudi mwingilinao huu utokee ni lazima kuwepo ukaribu wa hali ya juu kati ya ulimwengu wa viwanda na wa utafiti. Ni lazima pande husika zizungumze lugha moja.

Bila kufanya hivyo matokeo ya utafiti yanaweza yasiwe sehemu ya vipaumbele vilivyopo viwandani. Utafiti usiotatua matatizo ya msingi ya jamii vikiwamo viwanda utakuwa na thamani na mchango mdogo katika uchumi.

Hivyo, mwingiliano kati ya taasisi za utafiti na viwanda ni muhimu kuhakikisha haufanywi tu ilmradi bali kwa nia ya maendeleo ya viwanda.

Ugavi na uhitaji

Ili kufanikisha mwingiliano unaotakiwa kati ya taasisi za utafiti na viwanda kuna haja ya kuunganisha ugavi na uhitaji wa utafiti pia.

Maana yake ni kuwa upande unaotafiti ndio upande wa ugavi. Huku ndiko walipo watafiti na taasisi zao katika upana wake. Upande wa uhitaji ni ule walipo walaji au wateja wa matokeo ya utafiti. Hivi ni viwanda na wamiliki wake.

Ili kinachozalishwa katika utafiti kiwe ndicho kinachohitajiwa na walaji ni lazima pande mbili husika zizungumze pamoja. Ni lazima kuwepo majadiliano na mashauriano kuhusu nini kifanywe kwa maendeleo ya kiwanda kimoja kimoja kimahususi na nchi kwa ujumla wake.

Katika uhalisia, viwanda vingepaswa kuwa na idara za utafiti. Idara hizi zingejikita kufanya utafiti mahususi kwa kiwanda husika kwa lengo la kutatua matatizo na mahitaji yaliyopo.

Kuwa na idara hizi ni ghali. Viwanda vingi vidogo na vya kati hata baadhi ya vikubwa haviwezi kumudu gharama hizi. Vitapenda kujikita katika biashara zake za msingi kuliko kuwa na idara za utafiti. Vitakapohitaji utafiti vinaweza kuajiri waatalamu wa muda mfupi kwa lengo hilo.

Njia nyingine bora ya kuwa na mwingiliano kati ya watafiti na viwanda ni kwa taasisi hizi kuuza matokeo yake sokoni. Katika hili, taasisi hizi huzalisha matokeo na kuyashikilia kabla ya kuyaweka sokoni.

Kama ni vifaa, huzalisha vichache vya majaribio kisha kuvijaribu. Vikionekana vinahitajika, huzalisha kwa wingi kadri ya mahitaji ya soko. Ili uuzaji utafiti ufanikiwe ni lazima taasisi zikidhi mahitaji ya soko.

-->