MAONI YA MHARIRI: Staha izingatiwe Operesheni Sangara

Kuna mjadala ulioliteka Taifa letu kwa siku kadhaa sasa. Ni mjadala utokanao na kitendo cha baadhi ya maofisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuingia katika mgahawa wa Bunge jijini Dodoma na kupima urefu wa samaki wanaodaiwa kuwa walivuliwa katika Ziwa Victoria kwa njia haramu.

Kuanzia wabunge hadi viongozi wa Bunge, kilio chao ni namna maofisa hao walivyoendesha kazi hiyo ya upimaji wakisema kilichofanyika ni dharau kwa mhimili huo nyeti kwa Taifa.

Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Job Ndugai sio tu maofisa hao hawakuomba kibali cha kuingia na kufanya kazi katika eneo la Bunge, lakini upimaji haukuzingatia sheria, staha na taratibu za kiafya.

Ni tukio la aina yake kutokea katika mazingira ya mhimili huo wa nchi ambalo hata hivyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alilazimika kuomba radhi.

Tunatambua kuwa hivi sasa wizara hiyo inaendesha Operesheni Sangara inayolenga kuzuia vitendo vya uvuvi haramu vilivyokithiri katika maeneo mengi nchini, lakini kazi hiyo haina budi kufanywa kwa kuzingatia sheria na ustaarabu.

Kuwapima kwa kutumia rula samaki waliokwishapikwa tena kwa mikono iliyo wazi kulikofanywa na maofisa hao wa Serikali ni jambo ambalo limezua maswali mengi. Kama alivyosema Spika Ndugai kwamba watu wananunua samaki kwa kilo na hawanunui kwa futi.

“Halafu samaki mwenyewe kapikwa, amekwisha kuwa kitoweo, sasa hii sheria ya kupima kitoweo! Itabidi hizi sheria tuzisome sana, yaani samaki mbichi amevuliwa huko atafika Dodoma kwa muda gani, bado urefu ni uleule? Wapimaji wale wa wizara wanapima mikono haina hata glovu, mikono wazi, wanashikashika,” alikaririwa Spika Ndugai akisema bungeni juzi.

Hivi sasa katika maeneo mengi nchini wananchi hasa wanaotumia samaki kama kitoweo wana hofu inayotokana na Operesheni Sangara. Watu wana hofu ya kununua samaki au kuwabeba wakiamini wanaweza kukumbwa na rungu la kipimo.

Hatudhani kuwa Operesheni Sangara imekuja kuibua hofu na sintofahamu kwa wananchi. Mei mwaka huu, Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ilihoji utekelezwaji wake ikisema umegubikwa na ubabe, vitisho na viashiria vya rushwa.

Ifike mahali watendaji serikalini wajifunze kutokana na makosa ya zamani, kwa nini kila kunapokuwapo operesheni fulani hakukosi kuwapo manung’uniko na hata vilio?

Sio tu Operesheni Sangara ambayo nayo sasa inalalamikiwa, huko nyuma tumewahi kushuhudia operesheni kadhaa ambazo pamoja na dhamira njema ziliishia kuibua matatizo zaidi kwa wananchi na hata Taifa.

Tunasisitiza kuwa pamoja na nia njema ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Serikali kwa jumla katika kudhibiti vitendo vya uvuvi haramu, uendeshaji wa operesheni hii hauna budi kujali miiko ya kisheria, staha na ustaarabu wa Kitanzania.

Kwa sasa na hata baadaye, tunahitaji operesheni ambazo utekelezwaji wake utawagusa na kuwakosha Watanzania wengi zaidi, badala ya kila siku kubuni operesheni zinazoacha majeraha na vilio kwa wananchi.