Alikuwa mpiga debe sasa ni msomi anayepigania ukombozi wa fikra

Muktasari:

  • Mshereheshaji Lawrence Mwantimwa (39) kutoka mtaa wa Simike mkoani Mbeya aliyekuwa mpiga debe katika kituo cha mabasi miaka 23 iliyopita, anakuwa miongoni mwa kundi la Watanzania waliotengua dhana hiyo.

Maisha hayana bahati mbaya. Kila unachokivuna kwa sasa kinategemeana na msingi uliouandaa kwa miaka kadhaa iliyopita. Baadhi ya wataalamu wa sayansi ya jamii wanaamini uamuzi binafsi unaweza kutengua dhana ya umaskini unaochagizwa na historia ya familia, wazazi au utawala.

Mshereheshaji Lawrence Mwantimwa (39) kutoka mtaa wa Simike mkoani Mbeya aliyekuwa mpiga debe katika kituo cha mabasi miaka 23 iliyopita, anakuwa miongoni mwa kundi la Watanzania waliotengua dhana hiyo.

Kwa sasa anaishi ndoto alizozipandikiza mwaka 1998, akiwa machinga baada ya kutamani kurudi shule ikiwa ni sehemu ya majuto yaliyotokana na utukutu uliokatisha masomo yake akiwa kidato cha pili katika Chuo cha Ufundi Mbeya mwaka 1994.

“Kwa sasa nina shahada mbili. Shahada ya Habari na Mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Tawi la Dar es Salaam (Tudarco) na Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT),” anasema.

“Haikuwa rahisi, niliamua kuugua ugonjwa wa kubadili maisha yangu…nafsi yangu ilikuwa na nguvu ya kusukuma akili na mwili ili kutekeleza hitaji hilo.”

Mwantimwa ni mmiliki wa kofia nne zinazosaidia kuingiza kipato cha zaidi ya Sh5 milioni kwa mwezi. Ni wakala wa kuagiza magari, mwalimu katika maisha ya ujasiriamali, mwanasiasa na mshereheshaji (MC) wa matukio mbalimbali kama vile harusi.

Katika simulizi yake, anasema haikuwa rahisi kuamua mwelekeo mpya wa maisha baada ya kupitia kipindi kigumu.

“Nilikuwa mtoto mtukutu, sikusikiliza wazazi na nilidhani naweza kuyatafsiri maisha kwa namna yoyote ile, nikaamua kuacha shule nikiwa mlevi wa pombe kali, mvuta sigara. Marafiki walionizunguka walikuwa chachu ya kuingia kwenye kazi ya upigadebe. Nilipiga debe pale Mbeya mjini kwa daladala za kwenda Kyela na Tunduma. Nilijulikana kwa jina la Konda Lure,” anasema Mwantimwa.

Anasema alionekana kijana asiyeaminika akiwa na umri wa miaka 17 na wazazi wake walikata tamaa ya kufuatilia hatima ya maisha yake.

Baada ya kuachana na upigadebe aliotumikia kwa miezi 18, aliamua kuwa machinga kabla ya kazi ya upiga picha harusini, akijitegemea mtaani huku akiwa na msukumo wa kubadili maisha yake ya ujana.

Safari ya shule

Mwaka 1998, Mwantimwa akiwa mpiga picha aliamua kuhamia jijini Dar es Salaam na kuishi Mabibo kwa mchungaji Iman Mwakyoma wa Kanisa la EAGT Magomeni Makuti, akifanya kazi ya kukata nyasi na kukamua maziwa ya ng’ombe huku akiwa na ndoto ya kufika elimu ya chuo kikuu.

“Mwaka 2001 nilianza kidato cha kwanza Sekondari ya Kijitonyama baada ya kuanza kujitegemea na rafiki yangu nikitumia kipato cha kupiga picha mtaani, niliendelea hadi nilipomaliza kidato cha sita Sekondari ya Air Wing, Gongo la Mboto. Nikaingia Chuo Kikuu cha Tumaini kwa daraja la tatu kwa msaada wa Godwin Gondwe aliyenilipia hadi fomu ya kujisajili. Baadaye nikajiunga tena OUT kwa shahada ya sheria,” anasema.

Mwantimwa anataja mambo manne yasiyoepukika kwa kijana anayehitaji kutoka ‘katika’ kimaisha. “Ukiona kijana analia maisha magumu hayo ni matokeo ya kukubali kufa maskini, ni lazima ujenge taswira ya maisha unayoyataka bila kujali utakutana na nini mbele yako,” anasema.

“Katika maisha usikubali kuona umechelewa kufanya maamuzi. Mimi nilifanya maamuzi ya kuanza kidato cha kwanza nikiwa na miaka 21, walimu walidhani mie ni usalama wa Taifa, nilifedheheshwa mtaani hadi shuleni, sikujali. Leo nina shahada mbili na maisha mapya nikiwa na miaka 39. Hata wewe unaweza kuamua pia,” anasema Mwantimwa.