Arusha inavyotambua mchango wa vyombo vya habari katika maendeleo

Muktasari:

  • Anasema vyombo hivyo ni zawadi ya Mungu na ni sehemu ya kupanua mtazamo kuhusu mambo mbalimbali katika maisha ya watu duniani.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis katika salamu zake Juni mwaka juu, amenukuliwa akielezea umuhimu wa vyombo vya habari, ikiwepo mitandao ya kijamii.

Anasema vyombo hivyo ni zawadi ya Mungu na ni sehemu ya kupanua mtazamo kuhusu mambo mbalimbali katika maisha ya watu duniani.

Katika utekelezaji wa majukumu ya serikali, vyombo vya habari hutumika kama kioo kuonyesha mazuri, mabaya na maoni ya wananchi.

Pamoja na majukumu yake ya kutoa elimu, kuburudisha, kuonya vyombo vya habari hutumika kama sehemu ya kuhifadhi kumbukumbu ya matukio mbalimbali.

Hivyo, taifa lolote linalotaka maendeleo endelevu ni muhimu kushirikiana na vyombo vya habari si tu kuandika habari za serikali bali pia kupata maoni mbadala.

Maoni mbadala husaidia kupatikana hisia za walio nje ya utawala na jamii, juu ya mwenendo wa viongozi na serikali yao.

Juni 14 mwaka huu, Mkoa wa Arusha uliandaa mkutano ulioshirikisha wanahabari zaidi ya 120 na viongozi wa taasisi za serikali na umma, kuelezea utekelezaji wa majukumu na changamoto zake.

Mpango huu ulioanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo unapaswa kuigwa na viongozi wa mikoa mingine kwa kuwa kukaa na vyombo vya habari kuelezea mafanikio, changamoto na kujibu maswali kunasaidia taasisi kujua yanayoendelea katika jamii na kuboresha utendaji.

Jambo hili, ingawa kuna baadhi wanaweza kulipokea kwa hisia tofauti, nionavyo mimi lafaa kupongezwa.

Jambo hili pia linaondoa uadui usio na sababu baina ya watendaji wa taasisi za serikali na vyombo vya habari, kwani mwisho makundi hayo hujikuta yana lengo bora kutaka amani na maendeleo.

Kwa Mkoa wa Arusha jambo hili lina umuhimu wa kipekee hasa kwa kuzingatia mchango wa mkoa kwa taifa. Arusha ni mkoa wa pili kwa kukusanya kodi kubwa serikalini, lakini pia unaoongoza kuingiza mapato ya kigeni kupitia sekta ya utalii.

Utalii ndio unaongoza nchini na kuingiza fedha za nyingi za kigeni na unachangia zaidi ya asilimia 18 ya Pato la Taifa. Hivyo, Arusha inapaswa kuwa na mazingira ya aina yake yenye kutoa fursa kwa vyombo vya habari kuchangia maendeleo.

Miongoni mwa mambo ambayo vyombo vya habari vinaweza kusaidia kushamirisha maendeleo, ni umuhimu wa mkoa kuwa na amani utulivu ili kuenzi ile sifa ya kuwa “Geneva ya Afrika”.

Kutokana na Arusha kuwa shwari mapato ya utalii yameongezeka, kutoka dola 1.7 bilioni mwaka 2012 hadi dola 2.2 bilioni mwaka 2017.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya Maliasili na Utalii, ongezeko la mapato hayo, linatokana na ongezeko la watalii, kutoka 1,077,058 mwaka 2012 hadi 1,327,143 mwaka 2017.

Hali hiyo imechangiwa na taasisi zote za umma, kushirikiana na wanahabari kutangaza vivutio vya mkoa huo. Ni wazi kwa ushirikiano huo wa vyombo vya habari uliendelea, mkoa huo utafanikisha mipango ya Tanzania ikiwamo ya kuendeleza viwanda.

Hivyo itoshe kutoa wito kwa mikoa mingine na serikali kwa ujumla kutambua mchango wa vyombo vya habari na kuvitumia kwa uwazi kwa faida ya Watanzania wote.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha 0754296503.