Diamond wa sasa kawa mwepesi sana...

Muktasari:

Kupambana na WCB katika vita ya mitandaoni inatakiwa kujipanga sana. Wako wengi wamejitoa mhanga na hawataki kusikia chochote kibaya kuhusu WCB. Leo hii mwanadada mmoja mnyonge kasimama nao na wametulia. Wameshindwa.

‘Vita’ na Hamisa Mobetto ameshindwa. Ameshindwa kifamilia, mtaani na huko mitandaoni. Kila mtu yuko nyuma ya Mobetto. Hamisa kawa mkubwa sana kwa boko alilotoa Diamond mwenyewe, familia na ‘team’ yake. Hii siyo WCB tuliyoizoea miaka michache nyuma.

Kupambana na WCB katika vita ya mitandaoni inatakiwa kujipanga sana. Wako wengi wamejitoa mhanga na hawataki kusikia chochote kibaya kuhusu WCB. Leo hii mwanadada mmoja mnyonge kasimama nao na wametulia. Wameshindwa.

Mobetto ameikamata Instagram kama kalamu ya wanja wake akipaka nyusi zake. Anaichezea anavyotaka. Ana mashabiki wengi ambao wanampenda, wanamhurumia na zaidi wako tayari kwa lolote kumlinda na fujo za kima chochote.

Ni Diamond kafanya Hamisa awe pale alipo. Kama lengo ni ashuke, adharaulike, apuuzwe na kutoweka kwenye ramani, hali imekuwa tofauti. Amempaisha na sasa Hamisa ni ‘brand’ kubwa kuliko ‘vicheche’ kibao vya mjini. Anaanza Hamisa kwanza kabla yao kwa kila kitu.

‘Madem’ wa mjini wenye kupendwa zaidi mitandaoni, namba moja Hamisa, mbili Hamisa, tatu Hamisa. Kuanzia nne na kuendelea anza kuwapanga unaowajua wewe. Ule mtiti wa Wema ambao ulimtetea bila kujali baya au jema alilotenda, hivi sasa umehamia kwa Hamisa mara mbili zaidi.

Diamond kamjenga bila kupenda au kwa kupenda. Kwa sababu hapangi mipango yake vizuri. Ndo maana kipindi hiki ‘kiki’ zake zinapuuzwa ka kuwa hazipangwi vizuri. Sikushangaa Hamisa kuwagaragaza yeye, wapambe na familia yake kwa tukio ambalo yeye Hamisa alitakiwa anywe sumu.

Kashfa ya “uchawi’ ni nzito. Ilikuwa inammaliza jumla bila chenji. Lakini walio nyuma ya Hamisa wameifanya kuwa nyepesi na yenye maisha mafupi kama funza. Tumeshaisahau ndani ya muda mfupi. Tukio lenye uzito wa Mlima Kilimanjaro limekuwa dogo.

Akili kubwa iliyo nyuma yake imegeuza kashfa kuwa pesa. Badala ya kujifungia ndani na mashavu kuloa chozi, Hamisa hivi sasa anatengeneza pesa anavyotaka kwa kuteuliwa kuwa balozi wa bidhaa kadhaa, kupata mialiko na kusherehesha shughuli kubwa ikiwa ni pamoja na tukio la Miss Tanzania.

Huyu si Diamond wa miaka michache iliyopita. Huyu wa sasa anazidi kupanda ngazi akionekana kuzungukwa na akili ndogo. Anahitaji akili yenye uzito sawa na pale alipo hivi sasa. Wasaidizi wameelemewa kifikra. Hawawezi tena hata ‘bato’ dogo la Hamisa.

Mameneja wako ‘bize’ kuwaondoa watu wa muhimu kwa Diamond, badala ya kuwahifadhi. Kifesi kaondoka, leo hatuoni picha za kiwango kile. Hakuna staa aliyekuwa na picha kali kumzidi Diamond nchi hii. Rudisha kumbukumbu nyuma.

Mbali ya ubora kwenye upigaji picha, pia alikuwa fundi wa maneno ya kiswahili. Diamond alipotaka kunyoosha watu, kwenye ‘kapsheni’ zake mitandaoni Kifesi alihusika. Hivi sasa lugha zile hazipo tena,. Posti zake hazina uzito tena. Naye amekuwa mtu ‘yeyote yule’.

Kuna tofauti wakati wa Kifesi na sasa. Kuna picha ilipigwa ikimuonesha Diamond amebinuka kashika ardhi kwa mkono mmoja. Bonge moja liililotembea sana mitandaoni. Mpaka MTV Base wakaitumia wakati wa tuzo zao. Haikuwa bahati mbaya ni kazi ya Kifesi.

Kazi ya Kifesi ilifanya picha zake kutawala kila sehemu. Ilikuwa ngumu kuzikwepa kwa sababu zilikuwa bora. Hiyo ilifanya awe maalum na kuweka tofauti ya msanii na Diamond. Alijitenganisha na wenzake kwa ubora, lakini leo anajitenganisha na watu waliomfanya awe bora.

Leo akitokeza hadharani hana tofauti na wasanii wengine wa kawaida. Alifanya mahojiano Clouds baada ya sakata la mtoto wake na Hamisa. Hali akijua kabisa anarushwa hewani na mitandaoni, alivaa shati na suruali kama mwalimu wa nidhamu wa Shule ya Msingi ya Mtakuja. Huyu si Diamond wa siku zote.

Aliyefanya awe bora kimavazi hayupo tena. Q Boy Msafi, kazi yake pale WCB ilikuwa kumtengeneza Diamond muonekano wakati anapojitokeza hadharani. Taswira yake ikawa bora zaidi ya wasanii wengi Afrika. Diamond huyu wa leo anaonekana kakama kafubaa kwa stress za Zari.

Q Boy Msafi, kama ilivyo kwa Kifesi, aliondoka kwa kesi ya kibwege. Uzito wa kesi na uzito wa majukumu yake, mwenye akili timamu anaishia kushangaa kwanini menejimenti iliacha dogo aondoke. Diamond si yule aliyetikisa msiba wa Steven Kanumba pale Vatican City Sinza.

Anahangaika na misuko kichwani na matenge mwilini. Anavaa pajama kwenye shughuli za usiku na vikuku mguuni. Hajui avae vipi ili kuteka macho ya watu. Kwa sababu hakuna mtu wa kufanya kazi aliyoifanya Q Boy Msafi.

Katika mastaa wazito kimuonekano Afrika, Diamond alikuwa nafasi za juu kuliko mastaa wengi sana. Kuanzia mavazi mpaka mitindo ya nywele. Alivaa kulingana na aina ya tukio tofauti na sasa.

Alichokuwa akifanya Q Boy ni kujua aina ya tukio. Kama linahusu Coca Cola basi pamba zitakuwa na wekundu wekundu. Kama shughuli ya kibiashara basi suti na tai nyembamba kama Pep Gaurdiola zitahusika. Lakini hii leo, inaonekana hakuna wa kufanya kazi hiyo.

Tumeona hivi majuzi akiwa Marekani, anaingia na ‘traki suti’ kikaoni na mabosi wa YouTube. Kamwe Q Boy asingeruhusu kaka yake achemke namna hiyo. Alikuwa anajua anachofanya ndiyo maana Chibu akawa pale juu. Hakuwahi kuchemka kimavazi na muonekano.

Q Boy na Kifesi walifanya mastaa kibao wajue umuhimu wa wasaidizi. Chibu alionekana mwehu kuzunguka na kundi la watu, wengi hatukujua. Ni kama uwepo wa Mwarabu Fighter, ulifanya Chibu awe tofauti na Fid Q kama si Stamina na Roma pale wote wanapojitokeza hadharani.

Kuna mtu aliitwa Almasi Mzambele. Wengi wao hawamfahamu hasa mashabiki wa Diamond waliongia kwa mafuriko WCB. Huyu alikuwa bingwa wa kucheza na mitandao wakiwa na Kifesi. Wangekuwepo hii leo mchezo wa “uchawi’ wa Hamisa usingechezwa namna hii.

Hata ungechezwa, bado Hamisa na Team yake wasingefurukuta. Walijua lugha ya kutumia, kurasa muhimu mitandaoni za kuposti na zaidi muda sahihi wa kuanzisha mashambulizi. Waliobaki wameendesha kindezi na kuwatesa mama na dadaake Diamond.

Yawezekana mameneja wana sababu za kuwaweka kando watu wa mwanzoni. Walianza na Ruge wakamtenga na himaya ya Diamond. Ruge ndiye aliyetoa wazo la kumzawadia gari Gurumo wakati wa uzinduzi wa wimbo wa “Number One”.

Kwenye harakati za Diamond kupanda kileleni, Ruge alihusika kwenye michezo yote. Diamond sasa kawatanguliza Said Fella na Babu Tale mbele huku yeye akiwaongoza kwa rimoti. Wakaona wamekuwa wengi, wakamtenga Ruge na nafasi yake ya Kiingereza ikazibwa na Sallam.

Unawatengaje mameneja na uamuzi wa kuondoka kwa Zari? Ukifuatilia matukio ya kuondoka kwa watu muhimu pale WCB, lazima uwe na imani kuwa hata kuondoka kwa Zari ni mchezo kama wa Kifesi na wenzake. Ni kama dhambi Diamond kuzungukwa na watu wenye akili zaidi.

Ilikuwa rahisi kwa Zari kuona ‘maboko’ ya Diamond na kumuonyesha njia sahihi. Kitu ambacho hakipo sasa. Zari amekuwa mkosoaji mkubwa wa jinsi mambo yanavyokwenda pale WCB akiwa nje ya mbavu za Diamond.

Akiwa kando ya Diamond, aliponda kitendo cha Wasafi TV kuonyesha matukio na kuhoji familia ya Diamond tu. Kwamba kibiashara si nzuri. Kama aliishi namna hii basi ilikuwa lazima Zari atenganishwe naye. Akili kubwa haitakiwi Madale.

Mkubwa Fella kashindwa kusimamia Ya Moto Band kaacha itoweke kama Kifadulo. Kawaacha Chegge na Mh. Temba kama yatima wapambane na hali zao. Yeye yuko ‘bize’ Madale.

Babu Tale hayuko na Tunda Man, Keisha na wenzake, huku Madee akikomaa na Dogo Janja wake. Tale yuko ‘bize’ Madale, akijivisha mpaka usuluhishi wa hisia za Zarina Hassan ‘Zari’ kwenye kongosho za Diamond.

Unadhani Sallam ndo kichwa zaidi? Unakosea. Kama ni akili kubwa mbele ya Diamond mbona hatumii hiyo akili kwa Fid Q, ili naye achomoke na mchomoko mrefu zaidi? Sallam pia ni meneja wa Farid Kubanda “Fid Q’ na Ambwene Yessaya “AY’. Lakini katingwa na Madale.

Ni Mose Iyobo tu ambaye yupo tangu mchomoko wa kimataifa. Wote wameondoka kama si kuondolewa. Hata kama ni mke basi awe na upeo wa salon na vigodoro. Ukiwa na akili kubwa hiwezi kudumu pale Madale. Ile pesa inatazamwa na wengi.

Kwa mazingira haya lazima utajiuliza “hivi mameneja wa Diamond ni akili ndogo inayoongoza akili kubwa?” Kwa kiwango cha elimu yake, Diamond anahitaji akili mtambuka zaidi. Hii inayomzunguka sasa imegota kwenye ukuta wa baba mwenye nyumba Madale na Afrika Kusini.