Emmanuel Shadary, tumaini la Joseph Kabila DRC

Desemba 30, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ilifanya uchaguzi wa kihistoria kuchagua Rais ambaye atachukua nafasi ya Rais Joseph Kabila ambaye ameliongoza Taifa hilo tangu mwaka 2001 baada ya baba yake, Laurent Kabila kuuawa.

Rais Kabila alitakiwa kuondoka madarakani mwaka 2015, lakini aliendelea kubaki madarakani huku akieleza kwamba uchaguzi haikufanyika kwa sababu serikali yake haikuwa na fedha za kuandaa uchaguzi huo.

Hata hivyo aliendelea kupokea shinikizo kutoka kwa wananchi wake na jumuiya ya kimataifa wakimtaka aondoke madarakani kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo ili amani ya Congo iendelee kuimarika.

Watu walishangazwa na uamuzi wa Kabila kutangaza kuachia kiti hicho na kutangaza tarehe ya uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) ilitangaza wagombea na kuratibu na kusimamia uchaguzi.

Uchaguzi huo umehusisha wagombea wakubwa watatu katika siasa za DRC ambao ni Emmanuel Shadary ambaye ni mteule wa Rais Kabila kutoka chama tawala; Martin Fayulu kutoka Muungano wa Lamuka na Felix Tshisekedi kutoka chama cha UDPS.

Licha ya kwamba bado Tume ya Taifa ya Uchaguzi (CENI) haijatangaza matokeo ya urais, Shadary anapewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi kwenye uchaguzi huo ambao ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu.

Wachambuzi wa siasa za Congo wanasema kuondolewa kwa wanasiasa wenye nguvu kwenye uchaguzi huo kama vile Jean-Pierre Bemba na Moise Katumbi kunampa nafasi zaidi ya ushindi wa kiti cha urais.

Wanasema Fayulu na Tshisekedi wanaweza kugawana kura watakazozipata ambazo zitamfanya Shadary, chaguo la Kabila aibuke mshindi. Hata hivyo, CENI ndiyo yenye jukumu la kumtangaza mshindi katikati ya mwezi huu.

Shadary ambaye alizaliwa mwaka 1960 huko Kasongo, Mashariki mwa DRC, alianza kupata umaarufu wa kisiasa baada ya kuteuliwa na Rais Kabila kuwa Naibu Waziri Mkuu wa DRC wakati huohuo akiwa ni waziri wa Mambo ya Ndani.

Mwanasiasa huyo amekuwa mshirika wa karibu wa Rais Kabila kwa muda mrefu na Februari mwaka huu, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha PPRD, nafasi nyeti na ya juu ndani ya chama hicho ambacho kilianzishwa mwaka 2002.

Wanachama wa chama hicho walishtuka baada ya Shadary kutangazwa kuwa mgombea kwa sababu hakuna aliyedhani kwamba atapata nafasi hiyo. Kati ya wanasiasa kumi ambao walitarajiwa kupewa nafasi ya kugombea, jina lake halikuwemo.

Shadary ni msomi wa Chuo Kikuu cha Lubumbashi ambako alisoma shahada yake ya awali katika sayansi ya siasa na alihitimu mwaka 1987. Aliingia rasmi kwenye utumishi wa umma miaka ya 1990.

Mwaka 1997, alichaguliwa kuwa Naibu Gavana wa jimbo la Maniema na mwaka mmoja baadaye akawa Gavana wa jimbo hilo ambalo mama mzazi wa Rais Kabila anatoka.

Mwanasiasa huyo ambaye anasoma shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Kinshasa, alipewa jina la “Fanya Yatokee” baada ya kuongoza kusimamia makubaliano yaliyowezesha mabadiliko ya sheria kupitishwa na Bunge licha ya upinzani mkali.

Kama waziri wa mambo ya ndani, Shadary alifanikiwa kudhibiti maandamano ya mara kwa mara ya wananchi wakishinikiza kufanyika kwa uchaguzi ambapo alitumia polisi kukabiliana na waandamanaji hao.

Umoja wa Ulaya (EU) alimwekea vikwazo Shadary pamoja na viongozi wengine wa juu 15 kwa madai kwamba haki za binadamu zilikiukwa wakati jeshi la polisi likidhibiti maandamano ya wananchi mjini Kinshasa.

Vikwazo hivyo vinahusisha kufungiwa kwa pasi zao za kusafiria na mali wanazomiliki katika nchi wanachama wa EU. Umoja wa Ulaya ulipanga kuhuisha vikwazo hivyo, hata hivyo, Hispania ilipinga ikitaka Shadary aondolewe kwenye orodha ya waliowekewa vikwazo.

Mbali na kazi ya siasa, Shadary pia ni baba wa watoto watatu na mume wa Wivine, Paipo Ngweli. Yeye na familia yake wanaishi katika jiji la Kinshasa wakati akitekeleza majukumu yake kama waziri wa mambo ya ndani.

Wakati huohuo, Nehemie Mwilanya kutoka timu ya kampeni ya Shadary, aliviambia vyombo vya habari hivi karibuni kwamba ana uhakika kwamba Shadary ameshinda uchaguzi huo. Hata hivyo, Mwilanya hakutoa takwimu zozote kuthibitisha madai hayo.

“Kwetu sisi ushindi ni dhahiri,” alisema Mwilanya ambaye pia ni msaidizi wa Rais Kabila wakati akizungumza na vyombo vya habari.