Jokate, Hamisa Mobetto mambo safi

Jokate Mwegelo.

Muktasari:

  • Hamisa na Jokate walikuwa wakiripotiwa kipindi cha nyuma kutoelewana baada ya Jokate kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Diamond Platinumz wakati akijua fika Hamisa na mmiliki huyo wa lebo ya muziki ya WCB ni wapenzi.

Kama ulifikiri kuwa Hamisa Mobetto na mwanadada Jokate Mwegelo bifu lao halijaisha, utakuwa umekosea.

Hamisa na Jokate walikuwa wakiripotiwa kipindi cha nyuma kutoelewana baada ya Jokate kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamuziki Diamond Platinumz wakati akijua fika Hamisa na mmiliki huyo wa lebo ya muziki ya WCB ni wapenzi.

Si kwamba Hamisa na Jokate walikuwa wanavimbiana tu pindi walipokuwa wanakutana katika ishu zao za urembo, bifu lao lilienda mbali zaidi lakini baadaye liliishia kwenye njia ambayo ni nzuri ambapo mwaka juzi, Jokate aliwatumia warembo maarufu akiwemo Hamisa kwa ajili ya kutangaza nywele zake mpya zinazofahamika kama Malaika kupitia brand yake ya kidoti.

Sasa basi ikiwa wakazi wa Mwanza na mikoa ya jirani wameshuhudia onyesho la Miss Mwanza, siku hiyo kwa Hamisa na Jokate imekuwa neema kwao kukutana baada ya kuchaguliwa kuwa majaji.

Akizungumza na Mwananchi, Hamisa alisema amefurahi kuwa jaji wa shindano la Miss Mwanza kwa kuwa ni mzaliwa wa mji huo, hivyo atawatendea vyema washiriki.

Pia alisema amefurahiswa zaidi kuchaguliwa pamoja na Jokate kwani anategemea kujifunza mambo mengi ya urembo.

“Habari za kuwa na bifu na Jokate zilikuwa zinazungumzwa kitambo sana, ila ukweli ni kwamba mimi nimefurahishwa sana kuwa naye pamoja kama majaji kwani najua tuna mengi ya kufanya pamoja. Nategemea kujifunza zaidi kutoka kwake kwani mambo ya urembo yana ubunifu kila siku,” alisema.

Kwa upande wa Jokate, hakupatikana kuzungumzia suala hilo kwani hata alipopigiwa simu ili aweze kutoa neno kuhusiana na kukutana na Hamisa kwenye ujaji, simu yake ya kiganjani iliita bila kupokewa na baadaye kuzimwa.