Juma Mgeni : Mpiga ala mahiri asiyevuma

Muktasari:

  • Huyu ni Juma Hamza, msanii wa kizazi kipya anayekimbiza kwa spidi ya juu ili kuendana na hali halisi ya jinsi upepo unavyovuma.

Katika Mtaa wa Mtoni kwa Mama Mere, yupo kijana mmoja ambaye wengi hudhani ni raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutokana na umahiri wake katika muziki na mwonekano.

Huyu ni Juma Hamza, msanii wa kizazi kipya anayekimbiza kwa spidi ya juu ili kuendana na hali halisi ya jinsi upepo unavyovuma.

Wakati akisoma Shule ya Msingi Mtoni alikuwa muimbaji na mtunzi wa mashairi hususani wakati wa sherehe na karamu mbalimbali shuleni hapo hadi alipohitimu mwaka 2007.

Juma ambaye mashabiki wae wanamtambua kama Mgeni, ni mmoja kati ya wasanii wachache wanaounda kundi la Hanscana Brandy, chini ya Fadhili Kondo kama meneja.

“Naimba na nina wasanii kibao ninaowashauri aina ya muziki na mpangilio wa mashairi kwenye biti.” anajinasibu.

Mgeni, kwa mara ya kwanza ameonekana katika wimbo wa msanii anayefanya vizuri nchini, Aslay. Kwenye wimbo wa Nibebe, kuna jamaa anayeonekana akipiga ala ya muziki ya violini.

Huyo ndiye Mgeni, tunayemzungumzia hapa.

Sauti yake na mpangilio wake wa mashairi kwenye kiitikio cha wimbo huo, umewavutia watu wengi hususan mashabiki na wapenzi wa muziki wa Bongo Fleva.

Anasema Aslay ni mmoja kati ya wengi wanaofahamu kazi za msanii huyo.

“Aslay ananifahamu. Nimeimba na wasanii wengi sana lakini kutokana na sababu moja au nyingine, siwezi kuwataja hapa maana kazi nyingi bado hazijatoka,” anasema Mgeni.

Vipi kuhusu uraia?

Mgeni anasema moja ya changamoto anayokumbana nayo ni kuonekana raia wa kigeni kitu ambacho hakipendi na wengine huwapa hofu ya kufanya naye kazi.

Hili limemgharimu kufanya jitihada za ziada ili kuwaridhisha watu kwamba yeye ni Mtanzania.

“Nyumbani ni Mafia wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Nimezaliwa hapo na wazazi wangu wakahamia Mbagala Kizuiani na baadaye hapa Mtoni jijini Dar es Salaam,” anaeleza Mgeni.Watu wanasema sura yangu kidogo ina mkanganyiko. Ni kweli baba yangu ana asili ya Zanzibar na inadaiwa kwamba baba yake naye alikuwa nusu muarabu. “

Mgeni, anasema baada ya kufanya kazi na baadhi ya wasanii wa kuimba na wandaaji, watayarishaji, wapo waliomfundisha namna ya kutumia baadhi ya ala kama vile violini, piano na mixer.

Hili limemsaidia kwa kumrahisishia kazi husasan wakati wa kujirekodi na kufanya mixing yeye mwenyewe.

“Nina uzoefu wa kutumia baadhi ya vyombo vya kutengeneza ala za muziki kama vile violini na hivi karibuni nitaanza kujifunza namna ya kuandaa muziki kwa kutumia tarakilishi,” anasema Mgeni.

Mgeni ambaye ni mtoto wa pili kwa Mzee Hamisi, anasema mara nyingi alikosa ushirikiano kwani wazazi wake hawakutaka ajiingize kwenye nyanja ya burudani.

“Nahisi pia hili limechangia sehemu kubwa kwangu mimi kujikokota katika kutoka kimuziki.”

Anamshuru mmiliki wa Vibes Records, Shirko, kwa moyo wake wa kumsaidia kufika alipo, bila ya kumdai malipo.

Changamoto

Kama ilivyo ada, hakuna kisichokuwa na changamoto. Siri ni namna ya kukabiliana nazo kwa njia ya busara.

“Changamoto zipo na nyingi kweli kikubwa ni kuzikubali na kutafuta namna ya kukabiliana nazo iwe kwa kusaidiwa au kupambana nazo kama jeshi la mtu mmoja,” anasema Mgeni.

Anasema kuimba na wasanii wakubwa hapa nchini kama vile Aslay ni mafanikio.

Pia, analaumu kufanya kazi ni wasanii kutengeneza nyimbo lakini humgomea kumshirikisha katika utengenezaji wa video, kitu ambacho anaamini kingemtangaza sana.

Anasema ingawa sio makubaliano lakini kama wangefanya hivyo ingemtangaza zaidi na kupanua soko.

“Kwangu sioni taabu sana hata nikimuandikia msanii mkubwa mashairi au tukaingia wote studio na hatimaye asinishirikishe kwenye video, cha msingi tu akidhi vigezo na taratibu tunazokuwa tumewekeana.”

Anasema ndani ya huu mwaka, atahakikisha anaachia kazi nyingi ambao zitakuwa habari ya mjini.

Tayari amerekodi kazi nyingi na kwa mujibu wa menejimenti yao, Hanscana Brand, hana mamlaka ya kusema ni lini ataanza kutoa kazi hizo.

“Ninachokifahamu ni kwamba kabla ya mwisho wa mwaka huu, Mgeni atakuwa tayari ameachia vitu vikali na vilivyokwenda shule,” anaeleza Mgeni.