Kama “slogans” za kisiasa ni maendeleo tungekuwa mbali

Muktasari:

  • Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete akili-hutubia Bunge Maalumu la Katiba, aliwaambia wajumbe kwamba wakifan-ya kazi nzuri na kutengeneza Katiba mpya, majina yao yataandikwa kwa kalamu ya dhahabu kwenye kumbu-kumbu za Taifa letu.

Tanzania tuko mstari wa mbele wa kutunga “Slogans”. Naweza kuzitaja chache, lakini ziko nyingi; “Kilimo kwanza”, “Matokeo makubwa sasa”, “Uwazi na Ukweli”, “Hapa kazi tu”, “ Kasi mpya...”, “Kasi na viwango”, “Matokeo Makubwa sasa”. Nimeacha kutaja za mwanzo kabisa za “Uhuru na Umoja”, “Mvua za kwanza ni za kupandia” na “Chakula bora shambani”.

Mara nyingi “Slogans” zinafanya kazi nzuri katika uchochezi. Ninatumia neno zuri hapa, si kwa maana ya “uzuri” bali kwa kutaka kueleza “mafanikio” ambayo mtu anakuwa amelenga kwa kuanzisha uchochezi. Ni kiasi gani “Slogans” hizi zimechangia kulijenga Taifa letu Tanzania ni jambo la kufanyia utafiti.

Kuna ukweli kwamba wakati wa kupigania uhuru wa nchi yetu na miaka michache baada ya uhuru “Slogans” nyingi zilichangia kujenga Taifa na kuleta mabadiliko katika fikra mfano “Tanu yajenga nchi”, “Ubepari ni unyama” na “Mvua za kwanza ni za kupandia”, lakini “Slogans” za leo ni siasa na maneno ya kutafuta “Ulaji”.

Kitu kinachochanganya wengi wakati huu tunapohitaji kwa nguvu zote Katiba mpya ya Taifa letu ni msemo huu ulioibuka wa “Tanzania Kwanza”, je msemo huu nao ni “Slogan” kama zingine ambazo tunaziimba kama kasuku na kushindwa kuingiza kwenye matendo ujumbe unaobebwa na “Slongans” hizo?

Mara nyingi “Slogans” zinatumika kwa mambo ya kiimani. Makanisani na hasa haya makanisa ya “Kisasa”, “Slogans” kama vile “Simba wa Yuda”, “Chini ya mwamba” , “ ni kwa neema” na mengine mengi yameleta mafanikio makubwa kwenye makanisa hayo, hasa kwa kuwajaza waumini wengi ambao “Slogans” hizo zinawalewesha kiasi cha kuingiza mkono kwenye mifuko yao na kutoa fedha zote ili kukamilisha “Slongan” yenye nguvu kubwa isemayo “ Toa ndugu, toa ndugu ulicho nacho wewe Bwana anakuona hadi mfukoni mwako”.

Wanatoa bila kuuliza; fedha zinakwenda wapi? Zitafanya nini, maana wanakuwa wamelishwa “Slogan za nguvu” kwamba majina yao yataandikwa kwa kalamu ya dhahabu kule mbinguni.

Tunawasikia watu wengi wakisema kwamba wakati wa kutengeneza Katiba mpya, tuweke tofauti zetu pembeni na kutanguliza “Tanzania kwanza”. Ili kukwepa hatari ya kujiingiza kwenye “Slogans” wakati wa kuandika Katiba yetu mpya ni lazima kufafanua kwa kina pasi na shaka, “Tanzania kwanza” ni kitu gani? Tuna maana gani tunaposema tulitangulize Taifa letu? Na kwamba hakuna mtaalamu zaidi ya mwingine juu ya “Tanzania kwanza”.

Tulimsikia Rais Mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete akilihutubia Bunge Maalumu la Katiba, akiwaambia wajumbe wa Bunge hilo kwamba wakifanya kazi nzuri na kutengeneza Katiba mpya, majina yao yataandikwa kwa kalamu ya dhahabu kwenye kumbukumbu za Taifa letu. Ni maneno kama yale ya wahubiri wa dini hizi za kisasa ni maneno ya kuwalewesha watu na kuwafanya wajione wako peponi, wakati bado wako hapa duniani na wana kazi ngumu ya kutengeneza Katiba. Rais, aliwaimbia wajumbe hao wimbo mzuri wa kuwahadaa, wakati anawajaza hoja za CCM za kutunga Katiba ya serikali mbili na matakwa mengine mengi ya chama hicho tawala.

Kuandikwa kwa kalamu ya dhahabu kwa kuyasigina mawazo ya Watanzania, ndiyo kuijenga Tanzania kwanza? Tutafakari kwa pamoja na kushirikiana kutengeneza Katiba ya Taifa letu. Tanzania ni yetu sote, hakuna mwenye haki zaidi ya mwingine. Hivyo ni bora kuichana chana hiyo “Slogan” ya “Tanzania kwanza”.

Padre Privatus Karugendo

+255 754 6331 22