Kama hawa wanalima,kufuga unasubiri nini?

Muktasari:

  • Kwa kutegemea pensheni hiyo pekee, bado wangeweza kuwa na maisha bora kwao na hata familia zao.

Wangeweza tu kuishi kwa kutegemea pensheni zao kama wastaafu wa nafasi za juu katika utumishi wa umma nchini.

Kwa kutegemea pensheni hiyo pekee, bado wangeweza kuwa na maisha bora kwao na hata familia zao.

Hata hivyo, wastaafu hawa akiwamo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na aliyekuwa Waziri Mkuu wake, leo ni wakulima wa kupigiwa mfano nchini.

Hawajataka kutegemea pensheni pekee, wamejiongeza na walifanya hivyo hata kabla hawajatoka kwenye utumishi.

Kwa mfano, Rais Kikwete sasa anasifika kwa kilimo cha mazao mbalimbali ikiwamo mahindi, mbogamboga, mananasi, ufuta, ufugaji wa nyuki na ng’ombe wa maziwa. Anaendesha miradi hii katika maeneo mbalimbali nchini kama kijijini Msoga anakoishi, Mkuranga, Miono, Kibindu Bagamoyo na Dakawa.

Amewahi kunukuliwa akisema kuwa anajipanga kuanzisha kiwanda cha maziwa na siagi kwa sababu ana ng’ombe zaidi ya 400.

Kikwete alianza kilimo mwishoni mwa miaka ya 1980 ambako inawezekana hakuwa hata na ndoto ya kuwa Rais wa Tanzania.

Kwa upande wake, Waziri Mstaafu Pinda yeye anajihusisha na shughuli za kilimo katika shamba lake lililopo kijiji cha Zuzu mkoani Dodoma.

Pinda anamiliki shamba la ukubwa wa ekari 60 hukua akiwa amepanda mazao mbalimbali, mifugo na kuzalisha gesi ya asili ya biogas.

Sio Kikwete na Pinda pekee, kuna wastaafu wengi wenye viwango vizuri vya pensheni, lakini wameamua kulima au kufuga.

Wengine bado wako kwenye utumishi iwe serikalini au sekta binafsi, lakini sasa wameelekeza nguvu kwenye kilimo na ufugaji, wewe nani usiwaige watu hawa?

Makala inahanikiza wasomaji kuanza sasa kufikiria na kujikita katika kilimo na ufugaji. Kumbuka msemo maarufu hivi sasa kuwa mabilionea hivi sasa wanatoka kwenye sekta ya kilimo. Kwa aliye ajiriwa na asiyeajiriwa, sekta ya kilimo na mifugo ni mahala mwafaka kwa mtu kuwekeza.

Wakati ni huu

Mkurugenzi wa Chuo cha Kilimo cha Canre Dk Aloyce Masanja, anasema hakuna haja kwa mwajiri kusubiri mpaka astaafu ndiyo aanze kulima huku akisisitiza kuwa wakati wa kufanya hivyo ni sasa.

Anasema wanachokosea waajiriwa wengi ni kuishi kwa kutegemea ajira pasipo kujua kuwa ajira zina mwisho.

“Ni vizuri kabla mtu hajastaafu aingie kwenye kilimo, kwa sababu kilimo hakimtupi mtu. Kinachowakwamisha wengi ni kulima bila ushauri,”anasema na kuongeza:

‘’Mwajiriwa anayesubiri kustaafu kisha aanze kilimo anaweza kuishia njiani, kwa sababu kilimo kina pilikapilika nyingi zinazohitaji mtu awe na nguvu.’’

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Mtaalamu wa rasilimali watu, Ramadhani Shabani

anasema kabla mtu hajastaafu kazi anatakiwa kujitengenezea mazingira ya kuwa mjasiriamali kwa kuwa ajira haitodumu milele.

Anashauri mwajiriwa aanze kitu cha kufanya tangu mapema, alimradi hakiathiri muda wake wa kazi.

“Anaweza akaanza biashara au hata kilimo ambacho wengi wao hukimbilia huko ili hata anapostaafu anajua wapi pa kuanzia. Huyu hawezi kufanana na yule anayesubiri kustaafu kisha aanze ujasiriamali,”anasema na kuongeza:

“Ukiangalia kwa haraka mtu anayestaafu anaweza kuwa na zaidi ya miaka 60. Kwa hiyo mtu huyu atahitaji kupumzika; zile pilikapilika za kutembea huku na kule kusimamia miradi mfano ya kilimo inakuwa ngumu.’’

Zingatia haya kabla hujaanza kulima

Unapohamasika kuanza mradi wa kilimo hasa kile cha kibiashara, unashauriwa kutokurupuka. Mtaalamu wa kilimo Ally Said anakushauri kuzuingatia mambo saba yafuatayo kama anavyoeleza katika maelezo yake

1-Utayari kuingia katika kilimo.

Kabla hujajiingiza katika kilimo uwe tayari wewe mwenyewe kuamua kuanza kufanya kilimo husika. Kwa maana nyingine, namaanisha uamuzi wako ya kuingia katika kilimo utokane na uchaguzi wako mwenyewe baada ya kuridhika kuwa kilimo kitaboresha maisha yako.

Utayari wako utakusaidia kuongeza ari na juhudi zaidi katika kazi yako na kukupunguzia uwezekano wa kukata tamaa njiani.

2- Uchanguzi wa kilimo kinachokufaa

Kabla ya kuingia katika kilimo, lazima kwanza ufanye uchaguzi wa kilimo gani ambacho utafanya. Katika uchaguzi lazima uchague kitu ambacho utakuwa tayari kukifanya bila kupata pingamizi la utayari wa kufanya kilimo hicho.

Ukichagua kilimo ambacho si sahihi kwako, tarajia changamoto nyingi katika kilimo chako hapo baadaye.

3-Utafiti na ushauri wa gharama juu ya kilimo ulichokichagua

Baada ya kufanya uchaguzi wako, inakupasa ufanye utafiti wa gharama utakazoweza kuzimudu katika kilimo chako. Hili litaendana na ushauri wa jinsi gani ya kufanya kilimo chako kiwe kwa gharama nafuu zaidi na pia mbinu za kukabiliana na changamoto.

4- Panga bajeti

Yakupasa kupanga bajeti yako kabla hujaanza kilimo, kwa kuangalia utafiti na ushauri wa gharama juu ya kilimo ulichokichagua.

5-Usimamizi mzuri

Wakulima tunasema uchungu wa kilimo aujuaye mkulima. Msemo huu unamaanisha uangalizi wako kwa ukaribu katika kilimo chako unahitajika zaidi kuliko kuwa mtu wa kuagiza pekee.

6- Tafuta ushauri wa utaalamu wa kilimo ulichokichagua.

Kabla hujaanza usisite kutafuta ushauri wa kitaalamu wa kilimo ulichokichagua.

7- Anza kilimo chako kwa uhakika

Baada ya kupitia hatua hizo juu, anza kufanya kilimo chako kwa uhakika zaidi, huku ukitambua kuwa kilimo ni biashara.

Sio lazima ulime, ufuge

Inawezekana hujavutika na kilimo kwa maana ya kuwa mkulima, lakini kumbuka una fursa bado ya kunufaika na utajiri uliomo kwenye sekta ya kilimo na ufugaji kwa kuuza pembejeo au hata kusomea kilimo kwa minajili ya kuja kuwa mshauri kwa wakulima.

Fursa nyingine pia ipo katika biashara ya mazao hasa yale ya chakula. Huu ni mwanya mwingine unaotumiwa na watu wengi kuuaga umasikini.