UCHAMBUZI: Kwa nini serikali imeona hoja mapenzi ya jinsia moja tu?

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Amerika na Ulaya, Jestas Nyanmanga. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Mbunge wa Tarime Viji-jini, John Heche, amekiita kitendo cha serikali cha kugusia map-enzi ya jinsia moja kama “propaganda” iliyokusudiwa kuwaficha wananchi kuu-juwa ukweli wa jambo lenyewe. Akiandika katika ukurasa wake wa Twitter, Heche ameitaka serikali kujibu “hoja zote zinazosababisha nchi ikose sifa za kupata misaada kama zamani

Hatua ya Bunge la Umoja wa Ulaya (EU) kutoa azimio kuhusu Tanzania kwa kile bunge hilo imetaja kuwa ni kutokana na kukithiri kwa ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini, imeibua mjadala huku maoni kinzani yakiendelea kusikika kati ya wale wanaoliunga mkono na wale wanaolipinga.

Bunge hilo linaloundwa na wajumbe 751 kutoka nchi wanachama 28 za EU lilitoa azimio hilo la pamoja Alhamisi ya wiki iliyopita ikiitaka serikali ya Tanzania ifanyie kazi malalamiko yanayohusu hali ya uzorotaji wa haki za binadamu na uhuru wa kiraia nchini.

Azimio hilo lililobeba mapendekezo 15, limeitaka serikali ya Tanzania kujitafakari katika namna inavyoshughulikia suala la haki za binadamu na kuitaka ilinde mafanikio madogo yaliyokwisha fikiwa na Tanzania katika eneo la kuheshimu haki za kiraia kwa wananchi wake.

Pamoja na kunakiliwa kwa serikali, azimio hilo pia limetumwa kwa mashirika mengi ya kimataifa yenye uhusiano na Tanzania. Mpaka wakati wa kuandika makala haya, serikali haijatoa majibu rasmi kuhusu azimio hilo huku waziri mwenye dhamana na mambo ya nje, Dk Augustine Mahiga akiliambia gazeti hili wiki iliyopita kwamba hayuko tayari kujibu chochote kwa sasa kwani anasubiri maelekezo kutoka kwa Raisi John Magufuli.

Hoja za azimio lenyewe

Wabunge hao wa Umoja wa Ulaya, pamoja na mambo mengine, wameitaka serikali kuondokana na sheria, sera pamoja na vikwazo vingine vyote vinavyozuia uhuru, maendeleo kamili ya watu, na ambazo haziendani na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu.

Miongoni mwa sheria na vikwazo hivi ni pamoja na vile vinavyominya haki ya watu kujikusanya pamoja kwa malengo ya kisiasa na haki za akina mama na wasichana za kuishi maisha mazuri yasiyo ya bugudha huku wakiitaka serikali ibadilishe msimamo wake na kuwaruhusu wasichana wenye ujauzito kuendelea na masomo.

Kufuatia taarifa za uwepo wa kesi zilizohusisha mashambulio dhidi ya waandishi wa habari, watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, watetezi wa haki za binadamu na viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani, azimio hilo lenye kurasa sita limeagiza kufanyika kwa uchunguzi huru katika matukio hayo ili wahusika wake waweze kuwajibishwa kisheria.

Wabunge hao kwa umoja wao pia wameitisha kufanyika kwa marekebisho ya baadhi ya vifungu katika Sheria ya Makosa ya Mtandao, Kanuni za Maudhui Mtandaoni na sheria zingine kandamizi ili kuhakikisha uhuru wa watu kujieleza.

Haijawahi kutokea

Hii ni mara ya kwanza kwa bunge hilo la EU kuwahi kutoa azimio kuhusu Tanzania tangu kuanzishwa kwake mnapo mwaka 1993. Wadadisi wa mambo wanabainisha kwamba hatua hiyo inaashiria umakini wa umoja huo, ambao unajumuisha mataifa yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani kama vile Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Italia, katika mahusiano yanayozidi kuchafuka kati yake na Tanzania.

Uamuzi huo wa bunge hilo unakuja kufuatia tamko lililotolewa, Oktoba mwaka huu, na EU likibainisha mzozo wake na Tanzania kutokana na kile ilichokitaja kuwa ni “kulazimishwa kuondoka” kwa mwakilishi wake nchini, Roeland van de Geer.

Nchi wanachama wa EU kwa sasa zipo katika majadiliano na serikali katika kujaribu kurejesha mahusiano yao kufuatia mtikisiko unaoendelea kutokea baina ya pande mbili hizo huku nchi zingine kama vile Denmark ikitangaza kuondosha msaada wa takribani dola milioni kumi za Marekani (Sh22.9 bilioni).

Ni katika mazingira kama haya ambapo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amenukuliwa na vyombo vya habari wiki hii akisema kwamba nchi inapita kwenye kipindi kigumu kutokana na wafadhili kupunguza kutoa misaada.

Akiongea katika mkutano kati yake na watoa huduma za serikali katika kukusanya mapato, Dk Mpango alisema kwamba hali hiyo inatokana na wanaotoa misaada kuambatanisha masharti mengi ambayo ameyaita ya “hovyo.”

Moja katika ya masharti hayo ya “ovyo” ni pamoja na lile linaloitaka Tanzania kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja kitu ambacho Mpango amenukuliwa akisema “nchi haiwezi kukubaliana” nacho.

Azimio pekee halitoshi

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Wananchi (Cuf) Ismail Jussa azimio hilo la Bunge la Ulaya ilikuwa ni kitu cha kutegemewa kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni ambayo yamekuwa yakitokea nchini.

Jussa anasema hii inatokana na ukweli kwamba kuna mambo yameshakubalika kimataifa kama tunu za pamoja, kama vile demokrasia na haki za binadamu, ambazo kila mmoja katika jumuiya ya kimataifa anategemewa kuziheshimu na kuzifuata.

“Ni kile kile ambacho sisi ndani ya nchi tumekuwa tunakiomba lakini serikali imekuwa ikitupuuza,” anasema Jussa.

Zitto Kabwe, ambaye ni kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, ameliita azimio la bunge la EU kama “malalamiko halali kutoka kwa chombo cha kimataifa, ambacho kimekuwa ni rafiki yetu kihistoria, kuhusu uminywaji wa haki za msingi katika nchi yetu.”

Zitto anabainisha kwamba suala la kufanyia kazi mapendekezo yaliyomo kwenye azimio au la ni la serikali kuamua lakini hiyo haibatilishi msingi wa hoja zenyewe zinazopendekezwa na azimio.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk Vincent Mashinji anasema kwamba azimio hilo limekuja kwa kuchelewa sana kwani lilitakiwa lije mapema zaidi.

“Sisi kama chama tunaliunga mkono azimio hili,” anasema Dk Mashinji. “Lakini azimio tu halitoshi. Linatakiwa lifuatiwe na usimamizi endapo kama serikali itaamua kulipuuza na kuendelea kukiuka haki za binadamu.”

Serikali ikae chini na EU

Lakini, kwa mujibu wa mhadhiri wa masuala ya diplomasia kutoka Kituo cha Mahusiano ya Kigeni (CFR) Profesa Kitojo Wetengere anasema kwamba azimio hilo halipaswi kuungwa mkono na yeye binafsi analipinga kwa nguvu zote.

Profesa Wetengere anasema kwamba Tanzania ni nchi huru yenye mila na desturi zake zinazoongoza ufanyaji wa mambo tofauti.

“Ni nani ana umiliki wa maana ya haki za binadamu? Nani anamiliki maana halisi ya uhuru wa vyombo vya habari? Utagundua kuwa hakuna mtu mwenye umiliki huo. Kila mtu yupo huru kuyapa maana maneno haya kulingana na mila na desturi anazozisimamia pamoja na mazingira ya nchi husika,” anasema.

Hata hivyo, Profesa Wetengere ameishauri serikali ione ni jinsi gani inaweza kufanya mazungumzo na EU ili kuweka sawa mambo. “Kuna umuhimu wa kukaa na kuongea. Serikali inahitaji kueleza kwa nini inafanya kile inachofanya. Si kukubali masharti, bali kuongea na kujadiliana ili kufikia maelewano.”

+255 716 874 501