Malalamiko ya Wazanzibari kukosa ajira kwenye Serikali ya Muungano

Salim Said Salim

Muktasari:

  • Wakati mwingine kelele hizi huambatana na matamshi yaliyojaa hasira na kauli ambazo ukizizingatia zinatoa tafsiri isiyopendeza juu ya mfumo mzima wa Muungano.

Kwa muda mrefu zimesikika kelele nyingi Zanzibar juu ya mfumo na utaratibu wa ajira katika idara na taasisi mbalimbali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Wakati mwingine kelele hizi huambatana na matamshi yaliyojaa hasira na kauli ambazo ukizizingatia zinatoa tafsiri isiyopendeza juu ya mfumo mzima wa Muungano.

Hii ndio iliyopelekea baadhi ya watu kusema ni vyema Muungano uwe wa Serikali moja badala ya mbili na wengine kutaka mfumo wa shirikisho utakaokuwa na serikali tatu.

Kelele hizi sio zinasikika kwa watu wa kawaida tu bali hata katika chombo muhimu na kinachoheshimika cha Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Ukipitia kumbukumbu za mijadala mbalimbali ya Baraza la Wawakilishi (BLW) utaona zipo kauli zilizotolewa mara nyingi zenye matamshi makali na shutuma nzito za kudai haki haitendeki katika utoaji wa ajira kwenye taasisi za Muungano.

Wapo watu ambao wanapotoa lawama huambatanisha na takwimu za ajira ili kuonyesha hali ilivyo.

Watu hawa wanasema ni kawaida kuona watu saba hadi 10 wanapochaguliwa kushika nafasi za uongozi katika taasisi za Muungano, unaweza kukuta wote ni kutoka Bara na hakuna hata mmoja wa Visiwani.

Panapotokea kuwapo mtu mmoja au wawili kutoka Zanzibar basi wapo wanaosema kwamba hao waliochaguliwa wajihesabu kama watu wenye bahati ya kuweza kupenya kwenye tundu la sindano.

Pia, kuna taasisi za Serikali ambazo tangu kuungana Tanganyika na Zanzibar zaidi ya miaka 50 iliyopita hazijawahi kuongozwa na watumishi kutoka upande wa Zanzibar.

Zipo hisia za hapa na pale kuwa ukisikia unafanyika usaili wa watu kuajiriwa basi mara nyingi utaratibu huo huwa kama danganya toto na kwamba wanaopata nafasi hizo huwa watoto wa wale wanaoitwa, Ibni Khuzaymat” na Ibni Ilyas”.

Mengi yamesemwa na mengi yameandikwa juu ya suala hili, lakini imekuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa au kuku kutakiwa kucheza msewe.

Wapo wanaosema hata nafasi za kugombea uongozi au kuteuliwa kushika nafasi hizo katika Serikali nazo hutolewa zaidi kwa misingi ya kifamilia na wazee wa watu hao ni nani.

Ukiangalia hata ndani ya BLW unapata hisia za kukubaliana na hoja hii. Kwa lugha nyingine watu wengi wanaopata nafasi hizo huwa watoto na jamaa za Ibni Khuzaymat na Ibni Ilyas na wenzangu mie hukosa.

Wengine huenda mbali zaidi na kusema sura hii ya haohao kufunguliana mlango kushika nafasi za juu za Serikali zinaonekana hata ndani ya Bunge.

Lawama za ajira kwa nafasi za uongozi ndani ya Serikali zilikuwa moja ya mada kuu ya maoni yaliyotolewa na watu wa Zanzibar wakati wa kukusanya maoni juu ya tume ya Katiba mpya.

Kwa bahati baya siku hizi hatusikii lolote juu ya mpango wa kuwa na katiba iliyotumia mabilioni ya shilingi katika matayarisho ya hatua mbalimbali.

Hivi karibuni imetangazwa kwamba sekretarieti ya ajira ya Jamhuri ya Muungano itatembelea Zanzibar kupata maoni ya wananchi juu ya fursa za ajira katika Serikali.

Huu ni uamuzi mzuri, lakini itakuwa vizuri zaidi kama hiyo sekretarieti itaifanya kazi hiyo kikweli kweli na si babaisha bwege au danganya toto.

Ufanisi wa kazi ya hiyo sekretarieti utaonekana kwa hatua zitakazochukuliwa baada ya hiyo ziara na zaidi kama maoni ya wananchiyatazingatiwa.

Lakini, kwanza ni vizuri wajumbe wa sekretarieti wenyewe wajipime na kujitathmini na katika kuifanya kazi hiyo waangalie kama ina uwakilishi sawia wa pande mbili za Muungano.

Kama wajumbe wake hawatoi sura ya uwakilishi wa pande mbili za Muungano hata pakiwapo nia thabiti ya kufanya kazi kwa uadilifu basi hiyo nayo ni dosari.

Pia, ni muhimu milango ya kupokea maoni iwe wazi kwa watu wote bila kupangwa watu maalumu kama kundi la uwakilishi.

Wasiwasi uliopo unatokana na uzoefu wa hapa nchini wa kuunda tume, kamati maalumu, kamati ndogo na vikundi vya kuchunguza au kukusanya maoni na baadaye maamuzi yao kutozingatiwa au kuwekwa kabatini.

Kwa mfano, haya matatizo ya mfumo wa Muungano yameundiwa vyombo vya uchunguzi na kukusanya maoni zaidi ya mara tano tokea kuundwa kwa Muungano, lakini mapendekezo ya tume na kamati zote hizo yamebaki kabatini.

Tatizo kubwa na lilio wazi la hapa nchini ni kuwa hodari wa kuunda tume na kamati za uchunguzi au kukusanya maoni.

Lakini, zikishafanya hivyo mapendekezo yao hubaki kwenye mafaili kama vile zoezi la kutafuta maoni ya wananchi ni la kuwapa watu kazi ya kufanya na sio kuyafanyia kazi hayo waliyoyapata walipofanya uchunguzi.

Kwa kweli kuundwa tume, kamati au sekretarieti kuangalia masuala yanayolalamikiwa ndani ya Muungano baada ya kila kipindi imekuwa kama mtindo mpya wa mavazi, lakini mshono wa hiyo nguo ni uleule.

Hizi ni zama za ukweli na uwazi. Ni vizuri hiyo mijadala ya kukusanya maoni iwe wazi ili kila mwananchi awe na nafasi ya kuchangia na isiwe ya kimyakimya.

Kuweka mambo wazi kunasaidia kupunguza chokochoko zisizosaidia Muungano na kutawanyima nafasi wenye agenda za siri na za wazi za kuudhoofisha Muungano.

Tukumbuke kimya kingi huwa na mshindo mkubwa wenye kuleta hasara na kusababisha madhara.

Hapana haja ya kufanya utabiri. Tusubiri sekretarieti itagundua nini na itatoa mapendekezo gani na kama ushauri wao utafanyiwa kazi au utafungiwa kabatini kama ilivyotokea kwa matukio kama hayo ya siku za nyuma.