Mrembo anayetumia makovu kama fursa

Muktasari:

  • Huyu ni mrembo mwenye umri wa miaka 22 sasa aliyegeuza makovu yake makubwa ya majeraha ya kuugua kwa mafuta ya moto kuwa fursa ya kujiajiri kwenye fani ya urembo ambayo imempa umaarufu mkubwa kimataifa.

Shalom Blac haliwezi kuwa jina geni kwa wapenzi wa masuala ya urembo hasa vipodozi.

Huyu ni mrembo mwenye umri wa miaka 22 sasa aliyegeuza makovu yake makubwa ya majeraha ya kuugua kwa mafuta ya moto kuwa fursa ya kujiajiri kwenye fani ya urembo ambayo imempa umaarufu mkubwa kimataifa.

Akaunti yake ya Youtube ina watazamaji zaidi ya milioni tisa ambao hufuatilia habari zake pamoja na elimu ya urembo ambayo amekuwa akiitoa kupitia mwonekano wake wenye makovu ya majeraha hayo.

Kupitia akaunti yake, Shalom anaelezea mkasa huo wa kuungua ulimpata akiwa na miaka tisa wakati akiwa anamkimbia paka baada ya umeme kukatika nyumbani kwao.

Anasema kutokana na kumuogopa mnyama huyo aliamua kwenda kumfuata mama yake jikoni na hakuona chombo kilichokuwa na mafuta na kujikuta anajigonga na kuangukia humo.

“Majereha niliyopata yalisababisha kupoteza uwezo wa nywele kuota tena, yaliacha makovu makubwa ambayo yalisababisha kudhihakiwa kwa majina mabaya ikiwamo kuitwa sura mbili, sura ya makovu na kadhalika,” anasema Shalom.

Majeraha hayo anasema yalisababisha alazwe hospitali kwa muda wa miezi minne na baadaye shangazi yake aishie Marekani alipata taarifa hizo ambapo aliwachukua na mama yake ili kuhakikisha anamsaidia kupata matibabu zaidi ya majeraha yake.

Kutamani kujiua

Shalom anaeleza kuwa makovu yalimkosesha amani na wakati mwingi alilazimika kujifunika kujaribu kuyaficha ili kuepuka kufedheheshwa kwa majina mabaya.

“Nakumbuka siku moja nilichukua kisu na kuingia bafuni, nikajiangalia na kushangaa kwa nini watu hawanipendi wananiona mimi kuwa ni mzimu.

“Nikatafakari maisha yangu ya kufedheheka kila siku, hata nikienda matembezi watu wananishangaa nawasikia wakihoji nini kimenipata usoni kwangu,” anasema.

Baada ya kutafakari, aliamua kutafuta kazi ya kumsaidia binafsi akijaribu kuuona uzuri wake na hii ni baada ya kujipodoa taratibu na wakati huo kichwani akivaa kofia za nywele bandia (hair wig) za aina mbalimbali.

Wakati kwa makovu yaliyopo kwenye mabega yake anasema alikuwa anavaa nguo za mikono mirefu ili kuyafunika, hata hivyo baada ya muda aliamua kwenda kuchorwa ‘tattoo’.

Shalom ambaye anaonekana kuwa na tabia ya ucheshi anaamini kwamba ‘tatoo’ hizo kwa kiasi zimepunguza mwonekano wa ngozi na kuficha kovu lake, kwa kuwa amechorwa maua.

Hivi karibuni aliamua kurusha video mtandaoni inayoonyesha akifutwa vipodozi usoni mwake na kuvuliwa wigi na rafiki yake wa kiume.

Kwa sasa Shalom amekuwa bingwa wa kujipamba na kupamba watu wengine. Jambo ambalo limemwezesha baadhi ya kampuni za vipodozi kumtumia katika matangazo ya bidhaa zao.