Sunday, June 10, 2018

Sosopi: Kuzuia mikutano ya siasa kumeiongezea sapoti Chadema

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi

Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick Ole Sosopi akizungumza katika Ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata Relini jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Katibu Mwenezi,  Edward Simbeye. Said Khamis 

By Tausi Mbowe, Mwananchi

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema Taifa (Bavicha), Patrick ole Sosopi amesema matokeo ya kuzuia shughuli za kisiasa nchini kwa upande mwingine kuna manufaa kwa vyama vya upinzani kinyume na matarajio. Sosopi anasema hayo katika mahojiano maalumu alipotembelea ofisi za Mwananchi. Endelea...

Swali: Kuna mambo mengi yanayoendelea katika siasa nchini, hali ya Chadema ikoje kwa sasa?

Jibu: Chama chetu kipo imara kikipigania uhai wa demokrasia katika nchi, kupambania haki, kutekeleza dira, hatutegemei kuwa chama cha siasa au upinzani tu. Tunategemea kutawala nchi kwa ridhaa ya wananchi na ndiyo maana kila chaguzi zikifanyika tumekuwa tukishiriki na kuleta ushindani mkubwa kwa chama. Chadema tunatoa shukrani wa Watanzania kuendelea kukiamini chama chetu.

Awamu ya tano imeingia hali imekuwa tofauti tunakutana na utamaduni mpya wa siasa, huu si wa kikatiba au kisheria ni utamaduni wa mtu kuongoza anavyotaka. Shughuli za kisiasa zimepigwa marufuku na jambo hili haliathiri Chadema pekee yake japo sisi tumekuwa champions wa kupiga kelele na kupinga hayo yote na kuonyesha wajibu mkubwa wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo inaruhusu kila chama kinachopata usajili kufanya shughuli za kisiasa, kunadi sera, falsafa, dira na dhamira kwa watu mbalimbali.

Chama cha siasa hakiwezi kufanya shughuli zake kipindi cha uchaguzi tu, kuna vyama vinasajiliwa haina maana wasubiri mpaka katika uchaguzi. Unapoenda katika uchaguzi ni wakati ambao wananchi wanatakiwa wamefahamu sera zao.

Jambo hilo limeleta athari kubwa sana linaathiri mfumo mzima wa kuwaandaa vijana ili waje kuwa viongozi bora wa baadaye.

Je, kijana leo akitamani kuwa kiongozi wa siasa atumie njia gani kama hataruhusiwa kuona kwa vitendo namna siasa inavyofanya kazi. Tunaua vipaji vya vijana; lazima tupige kelele.

Swali: Baada ya kuteuliwa kuwa mwenyekiti Bavicha ulisema una deni kubwa. Je, umelimaliza, au umelipa kiasi gani?

Jibu: Kweli nilisema nina deni kutokana na hali ya kimazingira ya kisiasa ya nchi hii. Na deni ambalo ninaendelea nalo kulilipa kwa sababu kwa vijana wamejazwa hofu kubwa. Baada ya kuzuiwa mikutano wameamua kutumia mitandao ya kijamii na huko wanakutana na kitu kinaitwa cyber crime; tuna kesi zaidi ya 200 hadi 300 na vijana bila kujali itikadi zao, yaani wanapokosoa tu katika mtandao ni kosa. Nimekuwa sauti ya watu waliokosa sauti, kuwasemea vijana waliokosa mikopo na mazingira hayo yote.

Na sasa tumeona siasa zimeingia katika vyuo vikuu, Rais anapiga marufuku kufanya siasa lakini chama chake kinafanya. Pia, tumeendelea kusukuma ajenda yetu kuu ya kuanzisha Baraza Huru la Vijana Taifa kwani haijafika mwisho.

Na hoja hiyo iliwahi kuletwa na mbunge wa Kibamba, John Mnyika lakini Serikali iliamua kuichukua baadaye tukatoa maoni lakini mpaka sasa mchakato wake umefifia na hatujui umefikia wapi?

Nimeendelea kutekeleza majukumu yangu ya mwenyekiti, lakini mimi pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama, hivyo tumeendelea kusimamia mameya wetu ambao wapo chini ya Chadema wanaendelea kutoa asilimia tano kwa vijana.

Swali: Ukitazama kwa upana inaonekana majukumu uliyonayo ndiyo hayo ya mwenyekiti wa taifa, je, majukumu ya Bavicha ni nini?

Jibu: Kikatiba ukizungumza ni kwa ujumla, ndiyo majukumu ni hayo. Mimi ni mwenyekiti, nipo hapa kutekeleza malengo ya Chadema kwa sababu hatuna malengo ya Bavicha, hivyo kazi yangu kubwa ni kuhamasisha ili chama kipate sapoti kubwa ya vijana. Nikisaidie kipate kuungwa mkono na kundi kubwa la vijana na sensa inaonyesha 2012 asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana kati ya miaka 18 mpaka 35.

Sisi tunahitaji nguvu kazi ya Taifa kwa hiyo ni lazima kila mahali tuingie, machinga tunaendelea nao, bodaboda tunadili nao wanapata changamoto na tunatafuta jinsi ya kuwasaidia, tunatoa elimu kwa ujasiriamali n.k.

Swali: Umefanikiwa kwa kiasi gani?

Jibu: Ni jambo ambalo tunaendelea nalo kwa sababu ni jambo endelevu. Haiwezi fika mahali tukasema sisi kama vijana wa Bavicha inatosha. Tunaendelea kufanya uhamasishaji, kukutana vijana kwa vikao vya siri, maana pale ikishakuwa ni kikao tu hata cha kikatiba, inakuwa shida kwelikweli. Mpaka sasa nataka kuwahakikishikia Watanzania kwamba tunaungwa mkono na vijana wengi.

Swali: Unajuaje kwamba mnaungwa mkono?

Jibu: Hili ukitaka kulipima na ulione, hakuna ukumbi utatosha pale itokee mkutano wa vyama vya siasa umeruhusiwa. Mtaona uwezo wetu, mtaona nguvu yetu. Mfano mdogo tu ulikuwa ni katika uchaguzi mdogo wa Kinondoni na sapoti kubwa tuliyoipata. Nilikuwepo na mimi ndiyo niliongoza timu ya mgombea, mlikiona na nini kilitokea mwenyekiti alipotoa tamko tunakwenda kufuata vitambulisho na viapo vya wagombea wetu. Siyo wazee wale waliotembea, wale walikuwa ni vijana

Swali: Hivi sasa mpo katika hatua za chini za uchaguzi wa ndani lakini jina la Freeman Mbowe linakuwa gumzo, hili limekaaje?

Jibu: Hizi kelele zinapigwa na watu ambao siyo wana Chadema, lakini nataka kuwahakikishia hiki ni chama cha demokrasia, tunafuata demokrasia. Mbowe kuwa mwenyekiti mpaka leo siyo kwa sababu yeye ametaka kuwa mwenyekiti ni kwa sababu anachaguliwa kuwa mwenyekiti.

Ni kweli tumeanza uchaguzi ngazi ya kata na kalenda yetu inaonyesha Desemba ndiyo tutamaliza uchaguzi, sisi Chadema hatugawani madaraka. Mbowe amepewa jukumu la kuhakikisha Chadema inashinda. Sasa kama atakuwa hajalimaliza wakati wake wa kutekeleza hilo, naamini wana chadema wataendelea kumchagua. Mbona sisi hatuzungumzi kuhusu CCM hawabadilishi mwenyekiti wa chama, sisi kila mtu anaweza kuwa mwenyekiti lakini ndani ya CCM hadi mtu akishakuwa Rais. Tunataka Mbowe atekeleze majukumu yake mpaka wana Chadema watakaposema inatosha.

Swali: Unawezaje kupima hali hiyo wakati chaguzi mnashindwa.

Jibu: Hakuna chaguzi tumeshindwa, chaguzi hizi tunapokwa, kwani nani ambaye hajaona Kinondoni boksi limeibwa limepelekwa huko lilipopelekwa na polisi wakasimamia wamerudi nalo na hakuna aliyelikagua. Na kinachoweza kutokea, CCM inaweza kushinda siyo kwa uhalali wa wapiga kura bali ni kutumia nguvu ya dola nguvu ya jeshi la polisi.

Swali: Kama hiyo imani haiwezi kuwasaidia katika chaguzi, itawasaidia wapi?

Jibu: Imani hiyo itatusaidia katika uchaguzi mkuu, na uchaguzi mdogo ni tofauti.

CCM inaweza kushinda kwa nguvu ya dola na ndiyo maana matokeo ya chaguzi ndogo wamekuwa wakitushinda, lakini tukienda katika Uchaguzi Mkuu hawatuwezi na jinsi hali ilivyofikia ni wazi kwamba tutawashinda kweupe.

Swali: Tumesikia sakata la kufutwa uchaguzi wa Serikali ya wanafunzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) ikidaiwa mliingiza vijana wenu kupitia jumuiya ya wanafunzi wanachama wa Chadema (Chaso), unafahamu nini juu ya hili?

Jibu: Nina ufahamu wa uwepo wa Chaso. Na Chaso iko matawi yote Tanzania vilipo vyuo vikuu, lakini sina ufahamu wa kinachoendelea katika serikali za wanafunzi. Na mtu anayesimamia Chaso bahati nzuri nimekuja naye ambaye ni katibu wangu mwenezi, kazi yake ni kusimamia Chaso katika shughuli za kichama.

Inapokuja kwenye uchaguzi wa serikali za wanafunzi tunajua sheria za nchi na sheria ndogo za vyuo haziruhusu. Kule wananadi masuala yanayowahusu wanafunzi, hakuna anayesema ‘peoples’ mle ndani.

Sasa kama wana Chaso hawaruhusiwi kugombea huko labda tupewe mwongozo na msimamo, kwamba mwana Chaso haruhusiwi kugombea nafasi yoyote kwenye serikali za wanafunzi.

Swali: Hivi Bavicha hamna ukomo wa umri katika uongozi, mbona kama wewe umri umekwenda?

Jibu: Ahaa ahaa, ni shida tu hizi mzee...Tuna ukomo. Baraza letu mtu anayepaswa kugombea anapaswa kuwa na umri wa miaka 18 mpaka 30, wanachama wetu wanapaswa kuwa kati ya miaka 18 hadi 35. Ukishakuwa 36 unakuwa si tena mwanachama.

Swali: Wewe mwenyewe hujafikia umri wa ukomo, je utagombea tena?

Jibu: Mimi bado niko ndani ya umri. Kuhusu kugombea hilo bado, tukifika tutaona, bado nimekikalia kiti sawasawa.

Swali: Bavicha iliwahi kukabiliwa na wimbi la usaliti, hali sasa ikoje?

Jibu: Kuwa chama cha upinzani, hasa Chadema ambacho ni hatari kwa uhai wa CCM, usitegemee hatutakuwa na watu wa namna hiyo. Kwa sababu CCM nao hawalali, na kwa sababu wanajua sisi ni hatari kwao, hawawezi kuacha kuchomeka watu wa namna hiyo.

Na wasaliti hawako Chadema pekee, wapo kila mahali. Hata hapa kwenu wapo, wanawapa taarifa au siri za humu ndani kwa washindani wenu. Hata Chadema wamo, lakini kila tunapowagundua hatuwezi kuwaacha.

Na Arusha juzi kama mlivyosikia tulifukuza wawili, kiongozi mmoja na mwanachama wa kawaida. Kilichotokea walikuwa na tatizo la kimaadili na tulifuata taratibu zote kwa haki tukafikia maamuzi.

Niliunda kamati maalumu kuchunguza, mmojawapo alikuwa naibu katibu mkuu , na siku walipoitwa, yule kiongozi akajiuzulu nafasi yake. Yaani kutuhumiwa tu yeye aliona ana hatia, akaamua kukimbia, lakini sisi tuliendelea na uchunguzi na alipoitwa kuhojia kama mwanachama wa kawaida, akagoma, sisi tunachukua maamuzi.

Tuko kwenye boti katikati ya bahari, wewe mwenzetu unatoa mtumbwi tuzame wote halafu tukuache? Makosa waliyokutwa nao ni utovu wa nidhamu. Usaliti ndilo kosa kubwa ndani ya Chadema kuliko kosa jingine lolote. Usaliti waliofanya ni kwenda kinyume na maamuzi ya vikao vya chama. Na kwa katiba yetu, ukishafukuzwa uanachama Bavicha, ndio umefukuzwa Chadema.

Swali: Uligombea uenyekiti Kanda ya Nyasa, kitu gani kilitokea mkakorogana na Mchungaji Peter Msigwa?

Jibu: Sijawahi kukorogana na Msigwa. Kilichotokea, kwanza nilikuwa na sifa za kugombea mwenyekiti wa kanda. Kwanza natoka Mkoa wa Iringa uliopo katika Kanda ya Nyasa, nilikuwa makamu mwenyekiti wa Bavicha, nilipima dhamira yangu na uhitaji wa kanda nikaona nafaa. Kama mnavyojua chaguzi zina ushindani. Sikuwahi kutamka popote kwamba nataka uenyekiti wa kanda, lakini zilikuwapo oya oya nyingi mtaani, lakini mimi sikuwa sehemu ya hizo oya oya. Kama watu waliamua kunipigania, labda waliona ninafaa lakini mimi sikuwatuma. Msigwa alinukuliwa mara kadhaa akijibu hizo oya oya kwa mtazamo wake.

Tulipokwenda kwenye usahili, chama kilipima kwa mtazamo wake, kikaniambia nikae pembeni. Si kwa kujitoa mimi, lakini kikaona labda Msigwa anafaa zaidi kuliko mimi.

Kamati Kuu ilikuwa na uwezo wa kuchagua kutushindanisha ndani ya sanduku la kura, lakini waliona Msigwa ni bora zaidi wakampitisha, nami niliheshimu maamuzi ya chama. Lakini nayaona kwamba ilikuwa ni bahati yangu, maana amekuja kuondoka Patrobas Katambi nikawa mwenyekiti Bavicha. Na sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu, ulifungwa mlango ule na Mungu alinifungulia mlango mwingine.

Ulikuwa ni uamuzi mzuri wa chama, huenda walijua au hawakujua, lakini mwisho wa siku nimekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, nafasi ambayo ni kubwa kuliko mwenyekiti wa kanda.

Na kama chama kisingekuwa kinaniamini, nisingekuwa mwenyekiti wa Bavicha, lakini baadaye walinipitisha. Hili lilinipa funzo kubwa kwamba tunapaswa kuwa wavumilivu, na hatupaswi kutoka kwenye reli.

Swali: Bado unalimezea mate jimbo la Isimani?

Jibu: Naomba Mungu asinichukue kabla sijawa mbunge wa jimbo la Isimani. Si tu nina ndoto ya kuwa mbunge wa Isimani, bali pia ninatamani pia kuwa rais wa nchi hii, lakini kwanza niwe mbunge.

Mwaka 2015 nilipata kura 16,000 dhidi ya 21,000 za waziri William Lukuvi. Na ilikuwa kwa mara ya kwanza nagombea, nimetoka chuo kikuu, nilikuwa kijana mdogo, propaganda nyingine kwamba huyu bado mdogo zilikuwa nyingi, wapo watu wazima walioamini kuwa mimi bado, na masuala ya kikabila kule.

Na mshindani wangu alikuwa anazungumza kampeni za kikabila, na kura nilipata zaidi ya nusu. Sasa naendelea kujenga jimbo, kufanya kazi na kuna hofu kubwa sana. Mimi nikitembelea kule lazima Defender (gari la polisi) inifuatilie kule. Unajua Isimani ni jimbo lisilofahamika nchini na maskini sana, kwa kuwa mbunge wake huwa halizungumzii, yeye ni maarufu kuliko jimbo.

-->