Sura ngumu za askari wa Russia zilivyolainika

Monday July 9 2018

 

Jiji la Moscow limepokea mashabiki na wageni zaidi ya milioni moja kwa ajili ya fainali za Kombe la Dunia zinazotamatika wiki ijayo tu.

Mashabiki walikwenda Russia huku wengine wakijaza migahawa na hoteli wakipata vinywaji na chakula. Baadhi ya maeneo yalifurika mashabiki wakijipatia misosi mbalimbali.

Ujio wa mashabiki hao, wengine walitumia nafasi hiyo kutembelea mitaa mbalimbali ya Moscow na maeneo mengine yenye vivutio na iliwabidi wengine kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kuona timu zao kwa kuwa maeneo yao ni mbali.Baadhi ya miji katika vitongoji vya Russia kulikuwa na mabango ya mashabiki katika baadhi ya majengo na uzio kuonyesha kuwa wako hapo.

Mfano, huko Samara, watu wanaishi kwenye vibanda vya mbao na inaelezwa madirisha yake ni magumu kufunguka, lakini wanaishi kwa ajili ya timu zao zilizokuwa huko kwa Fainali za Kombe la Dunia. Yafuatayo ni mambo matano yaliyotikisa mji wa Moscow.

1. Furaha tu!

Tangu kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia, jiji la Moscow limechangamka. Ukifika Russia hasa Moscow utafurahi kwamba watu wa utamaduni mbalimbali wamekuwa wakifanya mambo yao, lakini kama unafurahi tu, Russia wana usemi wao kuwa ukifurahi tu kwa sababu unafuraha ni ujinga.

Wananchi wa Russia ni wakarimu, lakini wengi wana sura ngumu. Wengi si watu wa kuweka tabasamu huko Moscow. Sehemu kubwa ya mashabiki walikuwa wakipiga picha za selfie kwa ajili ya kumbukumbu zao kuwa walikuwa katika fainali hizo.

2. Kelele kwenye treni

Mara nyingi unapokuwa kwenye treni za abiria maarufu Metro huko Moscow, watu wote huwa kimya kila mmoja akitafakari yake. Ni matangazo ya maelekezo tu, lakini sasa hivi, ni kelele mtindo mmoja.

Hata masuala ya kibaguzi yanaonekana kumalizika kwenye treni hizo, kila mmoja anapiga stori kuzungumzia timu zao na wengine wakielezea mafanikio yao na kelele za furaha.

3. Rangi za bendera zatawala

Mashabiki maeneo mbalimbali wameenea kwenye miji ya Russia wakiwa na bendera za mataifa yao. Ni kama sehemu ya utambulisho wao. Siku za mechi, mashabiki wengi wanavaa jezi za mataifa yao na baadhi wakiwa na bendera ndogo.

Utambulisho wa mashabiki kwamba ni mwenzake ni uvaaji wa jezi na kushika ama kupeperusha bendera ndogo kwa pamoja.

4. Maeneo ya wazi yamejaa

Kabla ya fainali za Kombe la Dunia, maeneo ya wazi yalikuwa matupu, hakukuwa na watu, kwa kuwa polisi walipiga marufuku watu kukusanyika maeneo hayo kwani ndiyo maeneo yanayotokea vuguvugu za kisiasa, lakini kwa sasa kumejaa watu wa mataifa mbalimbali wakipumzika kubarizi.

Wengi badala ya kukaa hotelini, wanafika kwenye maeneo hayo kwa ajili ya kupumzika, kuangalia jiji la Moscow pamoja na kutafakari baada ya mechi za kwanza.

5. Polisi wapole kabisa

Huko Russia kwa kawaida, huwezi kumgusa askari, huwezi kumfikia wala huwezi kuzungumza na polisi. Utaanza vipi kushikana mkono na polisi utaanzaje kwanza.

Hapo hata yale mambo yetu sijui utayapenyeza vipi sijui. Polisi wenyewe wana sura ngumu na hapo ni kazi tu na uadilifu.

Katika fainali za mwaka huu, askari zaidi ya 30,000 walijiriwa kwa ajili ya fainali hizo, askari wanafuatwa kwa ajili ya kusaidia maelekezo, kwa ajili ya kutoa huduma na wengine wanafikia hatua wanapiga picha za selfie na askari, katika mazingira ya kawaida, askari gani utapiga naye selfie huko Russia!

Sasa swali kwa mashabiki na kila mmoja ni kwamba, haya mabadiliko katika jiji la Moscow wakati huu wa fainali, jee, mengine yataendelea ama ndiyo la?

Lakini kiukweli, imeshaelezwa kuwa baada ya fainali, askari wote wataendelea na majukumu yao na kila mmoja atarejea kwenye eneo lake, kazi kama kawaida.

Advertisement