UCHAMBUZI: Wabunge hamahama tamu au chungu kwa chama cha CCM?

Muktasari:

  • Chadema imekimbiwa na wabunge saba katika majimbo ya Ukonga, Siha, Babati Mjini, Serengeti, Ukerewe, Mon-duli na Simanjiro.
  • CUF imekimbiwa na wabunge watatu katika majimbo ya Kinondoni, Liwale na Temeke.

Duniani, maneno political migrants (wahamiaji wa kisiasa), tafsiri yake ni wanaohama nchi zao kutokana na migogoro ya kisiasa. Inawezekana sababu ikawa vita au sera za nchi zenye kubagua wengine, kundi lenye kubaguliwa linaamua kutafuta hifadhi katika mataifa mengine.

Tafsiri hiyo katika wigo wake ni kwamba wahamiaji wa kisiasa wanaweza kutokana na upinzani wa kisiasa. Walio madarakani wanawajengea hofu au kuwatisha wapinzani wao kiasi cha kujiona hawapo salama, hivyo kukimbia nchi ili kutafuta hifadhi.

Uhamaji wa kawaida kutoka chama kimoja kwenda kingine hautafsiriwi kuwa ni uhamiaji wa kisiasa. Bila shaka ni kwa sababu dunia haijawahi kushuhudia kokote yale yanayotokea Tanzania kwa sasa.

Ujio wa siasa mpya Tanzania, wimbi la wabunge na madiwani kuhama vyama vyao na kutimkia CCM, ni dhahiri kuwa tafsiri ya uhamiaji wa kisiasa imepanuliwa. Kwamba pamoja na migogoro ya kisiasa, mvuto wa kiongozi madarakani unaweza kuwa chanzo cha uhamiaji wa kisiasa.

Viongozi wenye dhamana ya wananchi, yaani wabunge na madiwani, waliochaguliwa kwa rasilimali fedha, watu, muda na kadhalika, wanaweza kuhama vyama vyao, kujiuzulu nyadhifa zao, hivyo kuliingizia taifa hasara kwa sababu ya kuvutiwa na kiongozi aliye madarakani.

Uhamiaji huo unafanyika kwenye nchi yenye changamoto lukuki. Huduma za kijamii zina utata. Mbunge ambaye jimbo lake wanafunzi wanaketi chini kwa kukosa madawati, wanafeli mitihani kwa sababu ya uhaba wa walimu na ukosefu wa vifaa vya kufundishia, anajiuzulu kuunga mkono juhudi za maendeleo yaletwayo na Serikali.

Mbunge ambaye wajawazito katika jimbo lake wanajifungua katika mazingira magumu, wastani wa vifo vya wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano ni mbaya, anajiuzulu ubunge, kisha anagombea tena kupitia CCM ili arudi bungeni, wakati gharama za uchaguzi zinatosha kujenga kituo bora cha afya.

Chama tawala ambacho kina mahitaji makubwa ya fedha, kinakabiliana na changamoto kubwa ya kibajeti ili kutimiza ahadi zake za uchaguzi, nacho badala ya kuogopa wimbi la wabunge na madiwani kujiuzulu na kuhama, kwamba linaongeza gharama kwa sababu fedha nyingi zinatumika kugharamia uchaguzi mdogo, ndiyo kwanza kinafurahia.

Chama tawala kinaamua kubadili mfumo wa kupata wagombea, kinawapa upendeleo wanaohama vyama ili wagombee na kutetea viti vyao walivyoviacha baada ya kujiuzulu. Chama tawala kinawapendelea wenye kuhama kuliko wanachama wake halisi kwa kuwapitisha bila kura za maoni.

Hizo ni siasa mpya Tanzania ambazo zinapaswa kuingizwa kwenye kamusi ya kisiasa ili kupanua tafsiri ya uhamiaji wa kisiasa. Wimbi la wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani kutimkia CCM kama inavyotokea hapa nchini kwa sasa, usipoita ni uhamiaji wa kisiasa, utatumia maneno mengine yapi yenye maana mahsusi?

Wabunge na madiwani wanatangaza wanahama ili kuunga mkono juhudi za Rais kuleta maendeleo. Ni sawa na kusema wao hawajiwezi katika kuwahudumia wananchi na kuwapa maendeleo. Hivyo, wameona Rais ndiye mwenye uwezo wa kufanikisha hili.

Dhahiri wabunge hao na madiwani hawana ubunifu wala maarifa ya kutoa matokeo chanya kwa wananchi. Wameona bora kupanda basi la Rais Magufuli ili maendeleo yakipatikana wajione ni sehemu ya waliyofanikisha. Kwa kifupi wameona bora wasafirie nyota.

CCM na Rais Magufuli wangeliona hilo vizuri wangebaini kuwa wabunge na madiwani wenye kuhama hawana kipya cha kuongeza kwenye basi la JPM la maendeleo. Kwa hivyo wangeweza kuwapokea lakini si kuwapa nafasi ya upendeleo ili wagombee tena ili kutetea nafasi zao. Maana hawana jipya.

Upande wa pili ni kuwa wanaohama wanagharimu fedha nyingi za uchaguzi. Je, haiwezi kuwa wanaohama wanatumika kumkwamisha Rais Magufuli? Kwamba wimbi la uhamaji ni kubwa, linateketeza fedha za umma. Hivyo basi, wanahama ili fedha ambazo zingetumika kuleta maendeleo, zigharamie uchaguzi. Hivyo uhamaji unapunguza kasi ya maendeleo.

Je, haiwezekani wanaohama shabaha yao ni kuichafua CCM ionekane inafanya siasa za dukani? Maana maneno ya wapinzani siku zote ni kwamba wabunge na madiwani wanaohama wanakuwa wamenunuliwa. Kadiri maneno yanavyotolewa ndivyo wimbi la uhamaji linavyokolea.

Je, wanaohama hawana lengo la kuivuruga CCM? Maana wanapewa nafasi ya kugombea kwa upendeleo. Je, wana CCM wazoefu wanafurahia hali hiyo? Isije ikawa mpango wa wanaohama ni kuwafanya wana CCM wazoefu kujiona hawathaminiki, hivyo wakasirike na kukiasi chama chao.

Wanaohama wanampenda kweli Magufuli na wanaungana naye kuleta maendeleo au wanajisalimisha baada ya kuona maisha yao ya kisiasa wakiwa upinzani yamejaa giza totoro?

Wanaona Uchaguzi Mkuu 2020 hawatashinda, kwa hiyo wanaamua kudanganya kumuunga mkono JPM kumbe wanajisalimisha wapate mbeleko 2020. JPM awaze hayo, isije ikawa ni chungu iliyopakwa tamu.