Walemavu wa akili na ombaomba waongezeka London-3

Muktasari:

  • Magari yanatwanga honi. Watu wawili, wenye mavazi machafu machafu, wamesimama katikati ya barabara wakimsubiri mbwa ajisaidie. Mwanamke, kabeba mkebe wa bia, mwenzake, mwanaume mkono mmoja umeshika myonyororo wa mbwa wake aliyechutama, mwingine kadhalika, kopo la pombe.

Unaongea katika simu, macho dirishani, ukiangaza nje.

Magari yanatwanga honi. Watu wawili, wenye mavazi machafu machafu, wamesimama katikati ya barabara wakimsubiri mbwa ajisaidie. Mwanamke, kabeba mkebe wa bia, mwenzake, mwanaume mkono mmoja umeshika myonyororo wa mbwa wake aliyechutama, mwingine kadhalika, kopo la pombe.

Uzunguni mbwa hawaruhusiwi kurandaranda ovyo. Shurti mkanda shingoni. Mkanda huwa na tarakimu la kusajiliwa- pale mnyama huyo akipotea, rahisi kutafutwa; au pia likitokea jambo fulani rahisi mnyama kukamatwa. Paka nao wameorodheshwa. Hakuna mbwa au paka koko wanaozurura zurura ovyo, kivurugu, bila wenyewe.

Sasa basi....

Huyo mbwa anayejisaidia ni wa Kijerumani - rangi nyeusi na kahawia...kabila “Rottweiler.” Vimikia vifupi. Wafugaji – wanawapenda. Kisa? Si waoga. Watulivu, waaminifu. Rahisi kuwafundisha ulinzi.

“Akikupenda ...hakuachii.”

Umewahi kumwona huyu jamaa, asiye na makazi. Mkasogoa.

Mzungu. Ana hasira sana. Si na walimwengu- kama alivyoimba marehemu Salum Abdallah miaka ile ya Sitini- bali na mkewe waliochana kipindi sasa.

Mji mwingine.

“Tulipooana wote tulifanya kazi. Mishahara mizuri. Tulikwenda matembezi Uturuki, Misri au Hispania siku za mapumziko watoto walipofunga shule. Ghafla nikaachishwa kazi. Si unakumbuka kasheshe za kiuchumi, 2008? Nikakaa sasa nyumbani na watoto. Kuwaogesha, kuwapeleka shule, kufua, kupika, nk. Bibiye akawa ndo’ mleta fedha. Akaanza kuniponda na mimi nikawa natafuta kazi – ila nlizopata zilikuwa mishahara koko. Bibie akabadilika ghafla. Utashangaa namna watu unaowajua huweza geuka kitabia. Nikaanza kunywa. Tukawa kila siku ugomvi. Mara tunalala vyumba tofauti. Hatukuwezana. Nikaja zangu London. Hapa si unapajua? Ghali! Kodi za nyumba juu. Nikaishia kuishi katika gari. Gari likanizidi gharama. Nikaliuza...”

Ndipo akampata mbwa, Bobby. Bobby na jamaa, jamaa na Bobby kila mahali, amoja. Kuna wakati ulimkuta amekaa pembe fulani akilia akakwambia Bobby wake alikufa. Akakauka, nusura afe. Majonzi. Ndipo akakutana na Suzy, huyu dada aliye naye sasa hivi. Naye aliachana na mumewe. Mume aliyemtandika mithili ya pia. Wamekutana. Wanapenda mbwa, sigara, pombe na bangi ikinunulika.

Baada ya muda akampata Rottweiler mwingine, jina Samson.

Ndiye huyu hapa anajisaidia.

Tofauti moja ya hawa walala nje, omba omba wasio na kazi na wenye mbwa na makazi yao, kuhusu mbwa. Wenye mbwa Uzunguni hutakiwa kufagia kinyesi kokote wanapokwenda nao. Hubeba mifuko ya plastiki kubebea mavi. Lakini ombaomba au wazururaji hawana nidhamu hiyo. Na ndiyo yanayojiri sasa hivi.

Gari inapiga honi weeee hadi mbwa anapomaliza.

Jamaa wanaondoka, bibie anamnyoshea kidole cha kati dereva - ishara ya matusi Majuu. Mwenzake hafagii kile kinyesi. Magurudumu ya magari yatafanya kazi hiyo.

Baadaye wanakwenda kanisa moja. Kila mchana hutolewa chakula bure kwa wasiojiweza. Baada ya kula wanaelekea makaburini.

Msomaji makaburi ya Ulaya huwa sehemu mahsusi ya wasio nyumba, kazi, hata wapenzi kupumzika. Wenzetu weupe hawana hisia au fikra inayofanana na zetu Waafrika kuhusu makaburi.

Hapo wanakaa wakipiga hadithi; sigara, pombe, wakivuta siku kando ya maua ya wakfu. Usiku watajua la kufanya. Mungu si Athumani.