Wanaume wajielekeze kutumia uzazi wa mpango kama walivyo wanawake

Muktasari:

  • Njia hizo za uzazi wa mpango zimeleta tija katika familia nyingi japo pia kama daktari nakiri kuwa bado elimu zaidi inahitajika kutolewa ili wazazi wapate uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa ujumla wake.

Tofauti na ilivyo miaka ya nyuma, utoaji wa mimba na uzazi holela umepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Njia hizo za uzazi wa mpango zimeleta tija katika familia nyingi japo pia kama daktari nakiri kuwa bado elimu zaidi inahitajika kutolewa ili wazazi wapate uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya njia za uzazi wa mpango kwa ujumla wake.

Hata hivyo, suala la matumizi ya njia za uzazi wa mpango linaweza kuibua maswali kadha wa kadha na kuleta mjadala kwenye jamii zetu, na maswali haya wakati mwingine huwa tunakutana nayo sisi wahudumu wa afya na baadhi ya maswali yanayoleta mjadala ni kama vile;

•Je matumizi ya njia hizi za uzazi wa mpango zinazingatia usawa wa kijinsia?

•Njia hizi za uzazi wa mpango ni rafiki kwa afya ya mtumiaji? (hasa mwanamke kama ilivyozoeleka)

Maswali mengi yanayohusiana na matumizi ya njia za kupanga uzazi huwa yanalenga maeneo haya mawili, lakini leo nitajikita kueleza kuhusiana na usawa wa kijinsia.

Tendo la ndoa na hasa linalofanywa bila kutumia kinga, mara nyingi linakuwa na matokeo mawili. Matokeo hayo ni magonjwa mbalimbali ya zinaa na mimba. Lakini hii haimaanishi kuwa kila washiriki wanapofanya tendo la ndoa bila kutumia kinga wanapata mambo haya kwa pamoja, hapana! Wanaweza wakapata moja tu ya mambo haya au wasipate kabisa. Itategemea tu wapo hatarini kiasi gani kupata moja ya mambo haya au yote kwa pamoja.

Suala la kujikinga au kuzuia magonjwa ya zinaa imezoeleka kuwa ni jukumu la wote wawili yaani mwanaume na mwanamke wake, lakini suala kuzuia mimba na kupanga uzazi wengi wanadhani kuwa ni jukumu la mwanamke.

Ndiyo maana inapofikia kwenye suala la kupanga uzazi mzigo wote wa kutumia njia mbalimbali za kupanga uzazi unabaki kwa mwanamke.

Hivyo nina imani wanaume kuanzia sasa mtaanza kuzingatia njia za uzazi wa mpango kwa lengo la kuwasaidia majukumu wanawake wenu kama nitakavyoeleza.

Kuchunga kalenda

Ni njia rahisi na ya asili ambayo mwanamke anaweza kuitumia katika kupanga uzazi, lakini njia haijaonekana kutumiwa na wanawake wengi kutokana na wanawake wengi kusema kuwa ni ngumu sana kuichunga kalenda na hivyo kuwasababishia kujisahau, hivyo wanawake wengi hutumia njia mbadala kama vile vidonge, vitanzi, sindano na vinginevyo. Kisayansi, pamoja utendaji kazi wa njia hizi, lakini bado zimeonekana kuleta madhara mengine ya kiafya na madhara haya yanaweza kuwa ya muda mfupi au ya kudumu.

Nadhani watu wanapaswa kujua kuwa, matumizi ya njia za uzazi wa mpango si jukumu la mwanamke pekee, ni jambo linalobeba usawa wa kijinsia.

Hata wanaume nao wana njia za uzazi wa mpango wanazoweza kuzitumia na kuwapunguzia wanawake majukumu haya na ikiwezekana kuwaondolea wanawake wao adha ya kupata matatizo ya kiafya yatokanayo na matumizi ya njia za uzazi wa mpango.

Baadhi ya njia za uzazi wa mpango ambazo mwanaume anaweza kuzitumia ambazo ni rafiki kwa jinsia ya kiume ni kama pamoja na matumizi ya kondomu, njia ya kutoa mbegu za kiume nje wakati mwanamke akiwa kwenye siku za kushika ujauzito, au ile inayohusisha upasuaji mdogo kwa lengo la kufunga mirija inayosafirisha mbegu za kiume kutoka kwenye korodani ili zisisafiri kwenda ukeni wakati wa tendo la ndoa. Njia hii kitaalamu inaitwa vasectomy.