Wapinzani DRC wajipiga ngwala kabla ya uchaguzi

Muktasari:

  • Idadi ya vyama vya siasa vilivyokubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa urais ni saba huku ikiwa ni miaka 18 ambayo Rais Kabila amekaa madarakani

Inawezekana ndoto za wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) bado ni za mchana na hilo huenda likawafanya washindwe kufuta nyayo za utawala wa Joseph Kabila anayejiandaa kuondoka madarakani.

Wengi wanaamini kuwa ndoto za usiku zina tija na mara zote zinaakisi uhalisia wa mambo yaliyotokea mchana.

Kwa mtazamo huo, wapinzani Congo kabla hata ya kunyanyua mguu kuelekea kwenye uwanja wa kampeni, tayari wameingia katika mgawanyiko tena siku moja tu baada ya kupitisha makubaliano mjini Geneva, Uswisi walikokubaliana kumsimamisha mgombea mmoja.

Ingawa vyama vyote saba vilivyohudhuria mkutano huo vilisaini makubaliano ya pamoja, hata hivyo, upepo umebadilika. Wameanza kulumbana na kukosoana hadharani wakitofautiana kuhusiana na makubaliano yalimpitisha Martin Fayulu kuwa mgombea pekee wa upinzani katika uchaguzi wa Desemba 23.

Fayulu wa chama cha ACD alikuwa amepitishwa na wapinzani hao kuwa ndiye kinara atakayekabiliana na mgombea mteule wa chama cha Kabila, Emmanuel Shadary ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani nchini humo.

Fayulu, mfanyabiashara ambaye aliingia ulingo wa siasa kwa mara ya kwanza mwaka 2006 alipochaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Kinshasa na baadaye mbunge wa taifa mwaka 2011, anatazamwa kama mtu mwenye ushawishi wa wastani kukabiliana na Shadary.

Akitazamwa kama mfanyabiashara zaidi, Fayulu alifaulu kubadilisha mitazamo ya wakosoaji wake pale aliposhiriki kikamilifu katika kampeni za mwaka 2011 kumnadi aliyekuwa mgombea wa upinzani, marehemu Ettiene Tshisekedi.

Uzoefu wake katika masuala ya biashara na hatimaye kufanikiwa kuzipamba siasa za Congo, ndiko kulikowapa msukumo wapinzani wenzake kuwa atakuwa chagua sahihi kukabiliana na mgombea anayeungwa mkono na serikali.

Elimu yake aliyoipata nchi za Marekani na Ufaransa ilimwezesha si tu kushamiri katika biashara bali kuwa na ujasiri wa kuanzisha chama cha upinzani na hata kufanikiwa kushinda kitu cha ubunge katika jiji la Kinshasa.

Alikuwa miongoni mwa wanasiasa wa upinzani waliojitokeza mstari wa mbele kukabiliana na Rais Kabila, wakimshinikiza kuondoka madarakani wakati muhula wake madarakani ulipofikia tamati Desemba 2016.

Miaka miwili baadaye, Rais Kabila amekubali kuwaaga Wacongo na kuingia katika historia ya marais wastaafu Afrika.

Felix Tshisekedi na Vital Kamerhe, viongozi wakuu wawili ambao walisaini mkataba wa uteuzi wa Fayulu wametangaza kujitoa kwenye makubaliano hayo wakiwalaumu wapinzani wenzao.

Wachambuzi wa mambo wanaona hatua hiyo ni kama wamejipiga ngwala na hivyo kumpa urahisi mgombea anayeunga mkono na Rais Kabila kuchanja mbuga.