Makamanda wa polisi washutumiwa kwa kuhoji watuhumiwa hadharani

Muktasari:

Katika miezi ya karibuni, makamanda wa polisi wa mikoa wanafanya zaidi ya utaratibu huo; wanawaonyesha na kuwahoji hadharani watuhumiwa na kuuliza maswali yanayoonyesha yanalenga kuwataka wakiri kuwa ni wahalifu au wavunja sheria kana kwamba wanaendesha kesi mahakamani.

Ni utaratibu wa Jeshi la Polisi kumuita mtu ambaye lina shaka kuwa amevunja sheria na kufanya naye mahojiano na baadaye kuchukua maelezo yake kama linaona kuna haja ya kuendelea na hatua nyingine.

Katika miezi ya karibuni, makamanda wa polisi wa mikoa wanafanya zaidi ya utaratibu huo; wanawaonyesha na kuwahoji hadharani watuhumiwa na kuuliza maswali yanayoonyesha yanalenga kuwataka wakiri kuwa ni wahalifu au wavunja sheria kana kwamba wanaendesha kesi mahakamani.

Lakini vitendo hivyo vinalalamikiwa na wadau wa sheria waliohojiwa na Mwananchi na wanasema ni ukiukwaji wa sheria na Katiba.

Video iliyoiibua mjadalam huo ni ile iliyosambaa katika mitandao ya kijamii siku kadhaa zilizopita ikimuonyesha kamanda wa polisi wa mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto akimuhoji mbele ya waandishi wa habari kijana aliyejichora mwilini maneno yasemayo “I Love You (nakupenda).

Kamanda Muroto alimuuliza kijana huyo umuhimu wa maneno hayo na kama watu wa kabila lake wanaweza kujua maana yake. Licha ya kijana huyo kumjibu kuwa hiyo ni sanaa, bado kamanda huyo alitaka kumuonyesha kuwa hayana maana yoyote na baadaye kudai ni mmoja wa wahalifu.

Kitendo kama hicho kimefanywa na makamanda wa mikoa tofauti na baadhi ya waliokamatwa walikiri, na wengine kutokubali kukiri, kama ilivyokuwa kwa Nabii Tito.

Katika kutafuta maoni kuhusu vitendo hivyo, Mwananchi ilihoji wadau ambao walisema ni ukiukwaji wa sheria na kwamba waliofanyiwa hivyo wanaweza kufungua kesi.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo mjini Dodoma, kwa kifupi Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba alijibu: “Nimesikia.”

Naye Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema mtu anayeona haridhishwi na utendaji wa jeshi hilo anaweza kufungua kesi mahakamani.

Mazungumzo kati ya mwandishi wa Mwananchi na Mwakalukwa yalikuwa ifuatavyo:

Swali: Tulitaka kufahamu utaratibu mnaoutumia mnapomkamata mtuhumiwa na jinsi mnavyotoa taarifa kwa umma kabla ya kumfikisha mahakamani.

Jibu: Sasa...nimeona clip (ya video) ya video ya kamanda wa Dodoma inatembea. Hebu niachie kwanza hilo, lakini mnaweza kumuuliza yeye kamanda wa Dodoma kwa kuwa ndiye msemaji wa mkoa huo na ukimuuliza yeye atakuwa na majibu.

Mimi ni msemaji wa jeshi zima, lakini kama kuna tatizo katika mkoa fulani, yeye ndiye anapaswa kuzungumza. Na mimi niko katika mitandao ninaona.

Swali: Asante kwa ufafanuzi huo, lakini turudi katika swali la awali, ni utaratibu upi unatumika kwa mtuhumiwa mkimkamata kabla ya kumfikisha mahakamani.

Jibu: Sasa sisi utaratibu wetu hatupaswi kuuongelea katika magazeti, upo utaratibu wa kufanya uchunguzi, kufanya mambo yetu... kama unaona kuna mambo hatuendi sawa, tunakosea nenda mahakamani kwani Jeshi la Polisi haliko juu ya sheria na unaweza kukata rufaa kwa waziri kama kuna utaratibu tumekiuka.

Lakini alipoulizwa, Kamanda Muroto aliiambia Mwananchi kuwa hana la kusema.

Katika video hiyo, Kamanda Muroto alimuhoji kijana huyo sababu ya kajiandika kifuani “I love u” na kutaka kujua kabila lake.

Alipojibiwa kuwa ni Mmakonde. alimuuliza kama Wamakonde wanafahamu lugha hiyo.

Mbali ya tukio hilo, Onesmo Machibya, ambaye anajiita Nabii Tito alikutana na maswali kama hayo mbele ya waandishi mkoani Dodoma. Kamanda Muroto aliwaambia waandishi makosa aliyodai ya mtuhumiwa huyo, lakini Nabii Tito hakukiri.

Katika tukio jingine la Machi 13, kamanda wa polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alizungumzia tuhuma dhidi ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo akiwa amemsimamisha mbele ya waandishi wa habari.

Kabla ya Mambosasa, kamanda wa Mkoa wa Iringa, Juma Bwire pia alitangaza makosa ya Nondo mbele ya waandishi wa habari.

Wanaweza kudai fidia

Lakini wadau waliohojiwa na Mwananchi walipinga vitendo hivyo.

“Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, pamoja na mambo mengine, inatamka ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa ana hatia ya kutenda kosa hilo, alisema wakili wa kujitegemea, Harold Sungusia.

Alisema kuwaita hadharani na kuwatangaza ni kama vile Jeshi la Polisi linakiuka sheria na ndiyo maana mtuhumiwa akiachiwa na mahakama anaweza kudai fidia ya kuchafuliwa jina.

Maoni ya Sungusia yanalingana na ya mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Vincesia Shule aliyesema kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao na hawatakiwi kufanya kazi ya kimahakama.

Dk Shule alitahadharisha kuwa sheria isipozingatiwa kuna siku watu watadai fidia kwa kudhalilishwa na jeshi hilo.

Hadhi ya mtu ilindwe

Mhadhiri mwingine wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, Dk Charles Kitima alisema: “Katika kulinda haki, hadhi na tunu ya mtu, inapaswa kulindwa. Hata kama polisi wanakuwa wanatekeleza wajibu wao, waheshimu utu wa mtu na kutokuonyesha uhalali wowote wa kumhukumu mtu kabla hajafikishwa mahakamani.

“Waandishi wa habari nao wanapaswa kuzingatia uhuru wa mtu. Si lazima kumwonyesha hadharani kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani. Wazingatie maadili waliyojifunza.”

Naye mwenyekiti wa zamani wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga alisema kumuweka hadharani mtuhumiwa, huifanya jamii kumchukulia kuwa ni mkosaji.

Mratibu wa Mtandao wa Wapigania Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa anasema moja ya jukumu la polisi ni kukamata wahalifu, kuchunguza na baada ya hapo ni kuwapeleka mahakamani. “Hawatakiwi kumuuliza mtuhumiwa umefanya kosa au hujafanya. Hilo linafanyika mahakamani na ndiyo maana siku ya kwanza unapofikishwa mahakamani hakimu anakuuliza unakiri au unakataa,” alisema Ole Ngurumwa.