Rais Buhari, makamu wake kupambana 2019

Rais Muhammadu Buhari.

Muktasari:

  • Chama tawala cha All Progressive Party (APC), kimemthibitisha Rais Buhari kuwa mgombea katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwakani hivyo akawa anasubiri kumjua mpinzani wake mkuu kutoka Peoples Democratic Party (PDP).

Abuja, Nigeria. Rais Muhammadu Buhari na aliyewahi kuwa makamu wa rais Atiku Abubakar wanatarajiwa kupambana Februari 2019 kuwania kiti hicho cha uongozi wa juu baada ya kupitishwa na vyama vyao.

Chama tawala cha All Progressive Party (APC), Jumamosi kilimthibitisha Rais Buhari kuwa mgombea wake katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika mapema mwakani hivyo akawa anasubiri kumjua mpinzani wake mkuu kutoka Peoples Democratic Party (PDP) ambacho kilifanya mkutano wa uteuzi Jumapili.

Hii itakuwa mara ya pili kwa Buhari (76) kuwania urais katika nchi hiyo yenye watu wengi  na uchumi mkubwa barani Afrika. Katika mkutano huo wa Jumamosi alipitishwa bila kupingwa.

Mwishoni mwa upigaji kura katika kile APC ilisema mchujo, rais alipata kura 14.8 milioni katika mkutano huo uliofanyika ukumbi wa Eagle Square jijini Abuja.

"Kwa unyenyekevu mkubwa napenda kuthibitisha kukubali uteuzi uliofanywa na chama chetu, All Progressives Congress kwa kuniteua kuwa mgombea katika uchaguzi mkuu wa rais mwaka 2019," alisema Buhari katika hotuba yake ya kukubali.

"Ninawashukuru wote kwa kuniunga mkono na mwongozo, na kwa kubaki katika nia ya Ajenda ya Mabadiliko."

Wakati chama cha APC kilikutana kumthibitisha Buhari mjini Abuja, Jumapili chama kikuu cha upinzani cha PDP kilimfanya mkutano mkuu katika mji mkuu wa kusini wa Jimbo la Rivers State, Port Harcourt.

Waliojitokeza kuwania urais kwa tiketi ya PDP ni watu walewale waliohama APC miongoni mwao wakiwa Rais wa Seneti Bukola Saraki, makamu wa zamani wa rais Atiku Abubakar, Gavana wa Sokoto, Aminu Tambuwal na gavana wa zamani wa Kano, Mohammed Rabiu Kwankwaso.


Katika mkutano huo Atiku Abubakar (72) alipitishwa hivyo atakuwa anakabiliana na Buhari katika uchaguzi wa rais uliofanywa Februari 2019.

Atiku alipitishwa baada ya kupata kura 1,532 akifuatiwa na Tambuwal kura 693, Saraki 317, Kwankwaso 158 na Ahmed Dankwambo 111.

"PDP, asanteni kwa kunichagua. Huu ni ushindi kwetu sote. Kazi iliyo ya kuifanya Nigeria iwe thabiti inaanza sasa," alisema Atiku katika ujumbe wa twita muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mshindi.