Makandarasi wazalendo walamba dume reli ya kisasa

Muktasari:

  • Alisema unapojenga makaravati au mifereji kwenye mradi wa reli ya SGR ujenzi wake unakuwa kwenye kiwango cha kimataifa na viwango vyake viko wazi.

Kampuni inayojenga reli ya kisasa ya standard gauge (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, Yapi Merkhezi Construction imepanga kuzitumia kampuni za makandarasi wazalendo kujenga baadhi ya madaraja na mifereji kwenye mradi huo.

Akizungumza na wanachama wa Chama cha Makandarasi Wazalendo Tanzania (ACCT) waliotembelea ujenzi wa reli eneo la Soga, mhandisi mkuu wa kampuni hiyo, Mert Oz alisema uamuzi wa kuwatumia makandarasi wazalendo kujenga mifereji na makaravati unalenga kuwawezesha kupata uzoefu na kujifunza teknolojia mpya. “Ninaposema tutawapa makandarasi wazalendo kazi za kujenga baadhi ya mifereji na makaravati yawezekana baadhi ya watu wakadhani ni kazi za kiwango cha chini, hiyo sio kweli,” alisema.

Alisema unapojenga makaravati au mifereji kwenye mradi wa reli ya SGR ujenzi wake unakuwa kwenye kiwango cha kimataifa na viwango vyake viko wazi.

Licha ya kutoa kazi kwa makandarasi wazalendo, aliwataka kuhakikisha wanafanya kazi kwa viwango vya juu ili kupata uaminifu na sifa za kutekeleza miradi mikubwa. Pia, aliongeza kuwa reli hiyo itakuwa ya kimataifa na ni moja ya reli za kisasa duniani.

“Reli hii tunayojenga ni ya teknolojia ya kisasa kama zile zinazotumika Uturuki, Ujerumani na hata Marekani na nchi nyingine zilizoendelea,” alisema.

“Ubabaishaji hata chembe hautakiwi hapa na kama utafanya hivyo utaingia katika orodha ya kampuni duni zisizostahili kupata kandarasi za kimataifa.”

Kwa upande wake, mwenyekiti wa ACCT, mhandisi Milton Nyerere alisema ushiriki wao katika ujenzi wa baadhi ya miundombinu ya reli hiyo utatoa nafasi kwa makandarasi hao kujifunza ubora na viwango vya kimataifa vinavyopaswa kutekelezwa katika miradi mikubwa. Mkadiriaji gharama za ujenzi wa kampuni ya ukandarasi ya Nordic, Magdalena Richard alisema jambo kubwa alilojifunza ni namna Yapi Merkhezi Construction inavyosisitiza kumaliza kazi katika muda uliopangwa. Mradi wa ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ulioanza Mei unatarajia kukamilika mwaka 2019.