Kuzuia makinikia kwashusha mapato Nyang’wale

Muktasari:

Wakati kipindi cha Januari hadi Juni 2016 halmashauri hiyo ilipokea zaidi ya Sh400 milioni ya malipo ya kodi ya ushuru wa huduma kutoka Bulyanhulu, kiwango hicho kilipungua hadi kufikia Sh226 milioni kwa kipindi kama hicho mwaka 2017.


Nyang’hwale. Uamuzi wa kuzuia mchanga wa dhahabu kusafirishwa nje ya nchi umeathiri mapato ya halmashauri za wilaya zenye migodi ya dhahabu baada ya kodi ya ushuru wa huduma kupungua.

Halmashauri ya wilaya ya Nyang’wale mkoani Geita ni kati ya maeneo yaliyoonja adha ya zuio hilo baada ya mapato kutokana na kodi ya ushuru wa huduma ya zaidi ya Sh700 milioni iliyokuwa ikilipwa na mgodi wa Bulyanhulu kwa mwaka, kupungua hadi Sh Sh301.6 milioni.

Wakati kipindi cha Januari hadi Juni 2016 halmashauri hiyo ilipokea zaidi ya Sh400 milioni ya malipo ya kodi ya ushuru wa huduma kutoka Bulyanhulu, kiwango hicho kilipungua hadi kufikia Sh226 milioni kwa kipindi kama hicho mwaka 2017.

Akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Kahama Agosti 2016, Rais John Magufuli aliagiza kusitishwa kwa usafirishaji nje wa mchanga wa dhahabu, amri aliyoirudia tena Machi 2, 2017 alipotembelea kiwanda cha Vigae cha Goodwill cha Mkuranga, Pwani.

Julai 2017, Bunge lilipitisha sheria mpya ya madini ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuzuia mchanga wa dhahabu kusafirishwa nje ya nchi.

Jana Februari 8, 2018 Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Nyang’wale, Carlos Gwamagobe amesema hali ni mbaya zaidi kwa malipo ya kati ya Julai hadi Desemba, 2017 kwa mapato hayo kupungua kwa asilimia 90 baada ya halmashauri kupokea Sh75.6 milioni kulinganisha na malipo ya Sh374.6 milioni kipindi kama hicho mwaka 2016.

Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea hundi kutoka mgodi wa Bulyanhulu unaomilikiwa na kampuni ya Acacia, Gwamagobe amesema kupungua kwa mapato hayo kutaathiri baadhi ya miradi ya maendeleo iliyopangwa kutekelezwa kwa fedha hizo.

Akikabidhi hundi hiyo, Meneja Mkuu wa mgodi wa Bulyanhulu, Benedict Busunzu amesema malipo hayo yamepungua kutokana na kupungua kwa shughuli za uzalishaji wa mgodini mwaka jana kulinganisha na mwaka 2016.

“Pamoja na shughuli kupungua, mgodi wa Bulyanhulu utaendelea kuwa mdau na mbia wa maendeleo kwa kuchangia gharama na kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi kwa kadri hali ya kifedha itakavyoruhusu,” alisema Busunzu.

Ameahidi kuwa mgodi huo kwa kushirikiana na serikali utatekeleza mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi halmashauri ya Msalala kwa gharama ya Sh4.5 bilioni.

“Mradi huu ambao mchakato wake unaendelea utanufaisha wananchi zaidi ya 100, 000 wa Msalala,” alisema Busunzu.

Katibu Tawala wa mkoa wa Geita, Celestina Gesimba aliyehudhuria hafla hiyo ameagiza fedha hizo zielekezwe kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo akitolea mfano kuwa zinatosha kununua vitanda 166 iwapo zitaelekezwa sekta ya afya au madawati 1, 316 na kunufaisha wanafunzi 3, 948 iwapo zitapelekwa sekta ya elimu.

Naye, Mkuu wa wilaya ya Nyang’wale, Hamimu Gwiyama aliutaka uongozi wa halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato kukabiliana na upungufu unaotokana na kupungua kwa malipo ya kodi ya ushuru wa huduma kutoka mgodi wa Bulyanhulu.