Makonda atoa tamko la 12

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda

Muktasari:

  • Jana, Makonda aliwataka waajiri wote wenye wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha asilimia tatu ya wafanyakazi hao ni walemavu.

Dar es Salaam. Kauli ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuhusu waajiri kuhakikisha asilimia tatu ya wafanyakazi wao ni walemavu, inaongeza idadi ya matamko yanayotolewa na kiongozi huyo ambayo hadi sasa utekelezaji wake ama haujafanyika au umetekelezwa kwa kiasi kidogo.

Jana, Makonda aliwataka waajiri wote wenye wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha asilimia tatu ya wafanyakazi hao ni walemavu.

Makonda alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kuzingatia sheria za haki za walemavu ambazo Tanzania iliziridhia.

Siku chache baada ya kuapishwa 2016, Makonda alikutana na wenyeviti wa Serikali za mitaa na kuwaeleza mikakati yake tisa aliyopania kuifanya katika kulibadilisha Jiji la Dar es Salaam.

Wakati akiadhimisha mwaka mmoja tangu awe mkuu wa mkoa, Makonda alieleza mambo aliyoyatekeleza kwa kipindi hicho ambayo hayakuwamo kwenye orodha ya mikakati yake aliyopanga kuifanya.

Mambo hayo ni kampeni ya mti wangu, ujenzi wa wodi ya wagonjwa, vita ya dawa za kulevya, ujenzi wa ofisi ya Bakwata, kampeni ya uchangiaji wa damu, marufuku ya shisha na migogoro ya ardhi.

Kiongozi huyo amewahi kuahidi usafi wa jiji, ofisi za Serikali kutokuwa za chama, kutenga maeneo ya biashara, sensa ya nyumba kwa nyumba, usalama wa raia na mali zao, watumishi hewa, kurudisha hadhi ya watendaji wa Serikali za mitaa, elimu na barabara.

Kwenye suala la usafiri, Makonda aliahidi zawadi ya gari la Sh20 milioni au fedha taslimu kwa mwenyekiti ambaye mtaa wake utaongoza kwa usafiri na Sh5 milioni kwa kila mjumbe wa mtaa husika. Pia, alisema zawadi hiyo ambayo ingekuwa ikitolewa kila baada ya miezi mitatu, ingeanza Aprili Mosi, 2016.

Jana, Makonda aliongeza ahadi nyingine akiwataka waajiri kufuata matakwa ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu namba 9 ya mwaka 2010 kifungu cha 31, inayomtaka kila mwajiri aliyeajiri wafanyakazi zaidi ya 20 kuhakikisha asilimia tatu ni walemavu.

Alisema ajira kwa walemavu inakabiliwa na changamoto ikiwa ni pamoja na waajiri kutokuwa tayari kuwaajiri au kutoa fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo kwa walemavu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Dk Yahya Msigwa alisema walemavu wapewe ajira iwapo tu wamekidhi vigezo vya nafasi husika.

Alisema Serikali imeyapa kipaumbele makundi maalumu ambayo ni vijana, wanawake na walemavu. Alifafanua kuwa msisitizo kwa walemavu umekuwa mkubwa kutokana na hali yao.

“Lakini wasipewe kwa kupendelewa. Kwa mfano, mtu ana zahanati achukue tu mtu asiyekuwa na sifa kwa sababu ni mlemavu hapana, wapewe kulingana na uwezo wao.

“Kama wanafanya mahojiano kwa ajili ya kazi, kama ameshindana na wazima na kuwa na vigezo sawa, anapaswa kupewa kipaumbele kwa sababu ya zile asilimia tatu za kisheria,” alisema Dk Msigwa.

Katika maelezo yake ya jana, Makonda alisema, “Nawapa muda kuanzia mwezi huu hadi Januari mwakani, kila kampuni iwe kwenye sekta binafsi au ya umma iliyopo kwenye mkoa huu iwe imeajiri kulingana na matakwa ya Sheria ya Watu Wenye Ulemavu. Ikifika Januari tutafanya ukaguzi kwenye kampuni ili kubaini kama hilo limefanyika.”

Makonda alifafanua kuwa mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu kifungu cha 27, unazitaka nchi wanachama kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa fursa sawa ya ajira pasipo ubaguzi kwa misingi ya ulemavu wao.

Meneja wa kitengo cha utetezi na ushawishi wa masuala ya watu wenye ulemavu kutoka Hospitali ya CCBRT, Fredrick Msigalah aliiomba Serikali kuweka mkakati wa makusudi na kufuatilia utekelezaji wa sheria na mikataba inayolinda ajira kwa watu wenye ulemavu.

Alisema waajiri pia wanapaswa kulizingatia hilo kwa kuweka mazingira rafiki kwa walemavu katika maeneo yao ya kazi ili kuwawezesha kufanya kazi bila shida.

“Tunawaomba waajiri wawatumie wataalamu wa masuala ya walemavu kutoka CCBRT kupata mafunzo ya namna ya kuwajumuisha watu wenye ulemavu,” alisema Msigalah.

Alisema CCBRT kuna dawati linaloshughulikia ajira kwa walemavu lenye kanzi data ya wanaotafuta ajira.

“Kuna wataalamu wa fani mbalimbali wasomi wa astashahada na shahada,” alisema.

Msigalah alisema utafiti uliofanywa na CCBRT mwaka 2010 katika kampuni binafsi 126 za jijini Dar es Salaam zilizokuwa na wafanyakazi 25,446 ulionyesha asilimia 0.7 tu ya wafanyakazi hao walikuwa walemavu.

Alifafanua kuwa 2010 walifanya utafiti tena kwa kampuni 50 kwenye mikoa mitano ya Mwanza, Morogoro, Arusha, Tanga na Kilimanjaro ambao ulionyesha kuwa asilimia 0.4 ya wafanyakazi 20,566 waliofanyiwa utafiti, ndiyo waliokuwa na ulemavu.

“Hii ni kinyume cha Sheria ya Ajira kwa Walemavu, ipo haja ya Serikali kutilia mkazo usimamizi na utekelezaji wa sheria hiyo,” alisema Msigalah.

Kilio cha wenye ualbino

Watu wenye ualbino wamewataka waajiri kutochukulia hali zao kama kigezo cha kuwanyima ajira huku wakisisitiza kuwa nao wanastahili kuajiriwa.

Wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakitengwa kwenye mfumo wa ajira kwa dhana kwamba hawawezi kufanya kazi.

Hayo yalielezwa jana wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha watu wenye ualbino waliohitimu vyuo mbalimbali nchini.

Mhitimu wa shahada ya pili katika fani ya lugha, Mahenda Kulwa alisema licha ya wao kupata mwamko wa kusoma, inawawia vigumu kupata ajira.

Alisema hata pale inapotokea mtu wa kundi hilo akiwa na sifa za kuajiriwa, kuna dhana potofu zinatumika kama fimbo kwao.

“Utakuta mtu umesoma lakini unapoenda kuomba kazi na una sifa haupati kwa sababu tu una ualbino. Hadi sasa wapo wanaomini kumuajiri mtu mwenye ualbino kwenye kampuni au taasisi ni kuleta nuksi.”

Hoja kama hiyo ilitolewa na Nayla Omari ambaye pia ni mhitimu wa diploma lakini hana ajira.

Mkuu wa Idara ya Ushauri na Masuala ya Ajira wa Under the Same Sun, Josephat Igembe alisema changamoto hiyo inaendelea kukua.

Alisema hali hiyo imekuwa ikisabababisha vijana wengi wenye ualbino kuendelea kubaki mitaani bila ajira licha ya kupata fursa ya kusoma.

Kutokana na hilo, shirika lake limendaa programu maalumu ya kuwakutanisha wahitimu wenye ualbino na waajiri.

Alisema kupitia programu hiyo, wahitimu wenye ualbino wanafundishwa jinsi ya kuzipambania nafasi za ajira na kufanya kazi kwa ufanisi.

Alisema wakati umefika kwa jamii kuachana na dhana potofu, wawape nafasi za kazi watu hao.

Ahadi za makonda

1. Usafi wa jiji

2. Ofisi za Serikali kutokuwa za chama

3. Kutenga maeneo ya biashara

4. Sensa ya nyumba kwa nyumba

5. Usalama wa raia na mali zao

6. Watumishi hewa

7. Kurudisha hadhi ya watendaji wa Serikali za mitaa

8. Elimu

9. Barabara

10. Kupima wanaume saratani ya tezi dume

11. Kuwasaidia wanawake waliotelekezwa baada ya kuzalishwa na waume zao

12. Waajiri kuhakikisha asilimia tatu ya wafnayakazi wao ni walemavu