Mambo 10 yaliyoitikisa nchi 2016

Basi la Kampuni ya New Force, lililokuwa likifanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Songea baada ya kuacha njia na kupinduka. Picha na maktaba

Muktasari:

Tangu mwaka uanze, kumekuwa na matukio mbalimbali yatokanayo na majanga ya asili, uhalifu, ya kisiasa na mengine mengi ya utendaji wa kila siku wa Serikali.

Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku 27 kumaliza mwaka 2016, wachambuzi wa uchumi, siasa na jamii wamebainisha mambo makuu 10 yaliyotikisa nchi huku wakiitaka Serikali kuyafanyia kazi katika mwaka 2017.

Tangu mwaka uanze, kumekuwa na matukio mbalimbali yatokanayo na majanga ya asili, uhalifu, ya kisiasa na mengine mengi ya utendaji wa kila siku wa Serikali.

Miongoni mwa mambo hayo ni tukio la tetemeko la ardhi lilioukumba Mkoa wa Kagera, ajali za barabarani, vita dhidi ya rushwa, mauaji ya kinyama yakiwamo ya askari polisi, mtikisiko wa uchumi, utumbuaji wa majipu, kesi za vigogo mbalimbali, bei kwa sukari na operesheni Ukuta.

Katika mjadala wake, Profesa wa elimu wa katika chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitila Mkumbo alisema pamoja na taifa kupitia katika matukio hayo makubwa yakiwamo yaliyosababisha kupoteza roho za Watanzania mwaka huu, kwake tukio kubwa ambalo limeacha historia katika Taifa ni kumpata Rais mpya, Serikali mpya na ajenda mpya.

Alisema mambo hayo mapya yamewawezesha Watanzania kuelewa ile dhana iliyokuwa ikipigiwa kelele miaka mingi kuwa madaraka ya Rais ni makubwa mno na yanapaswa kuangaliwa upya na kupunguzwa.

“Uamuzi wa Rais kuamua kuzuia Watanzania kufanya siasa ina maana vyama vya siasa vipo kifungoni, na hii ina maana kuwa yale malalamiko yetu kuwa Rais ana madaraka makubwa yaliyoonekana kuwa ni nadharia, sasa ametusaidia kuona kuwa kulikuwa na hoja,” alisema Profesa Mkumbo.

Katika uamuzi huo, vyama vya siasa vilizuiwa kufanya mikutano ya hadhara na wakati fulani hata ya ndani, jambo lililozaa mpango wa Chadema wa kupinga ilichoita udikteta (Ukuta) uliotikisha nchi kutokana na mabishano baina ya chama hicho na Jeshi la Polisi. Hata hivyo, baadaye mpango huo ulisitishwa kwa maelezo kwamba ungekuja kwa sura nyingine na bila taarifa.

Profesa Kitila aliongeza kuwa kutokana na madaraka makubwa aliyonayo Rais kama taasisi, siku moja akitokea mtu asiye na busara huenda akaipeleka nchi katika hatari na tukapata matatizo makubwa kama taifa.

Alisema Tanzania imekuwa na bahati ya kupata marais wenye busara ambao wameliongoza Taifa bila matatizo lakini endapo atatokea asiye na busara, hali inaweza kuwa mbaya.

Alisema ni kutokana na kuwa na viongozi wenye busara, ndiyo maana Watanzania hawakuona haja ya kuwapunguzia madaraka na wakati wote wamekuwa wakiishi kwa kutegemea huruma au roho nzuri ya Rais kufikia hatua fulani.

Akatolea mfano kuwa uamuzi wa kuamua kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya ulitokana na roho nzuri ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete lakini akasema sasa Watanzania waache kusubiri huruma na badala yake waamke na kuanza upya kudai Katiba Mpya ili pamoja na mambo mengine, madaraka ya Rais yaangaliwe upya na kuwekewa mipaka.

“Uwezo wetu wa kuhoji na kudai upo, natoa wito kwa wasomi, waandishi wa habari, wanaharakati, Rais Magufuli ameturahisishia na kutuwezesha kujua kuwa madaraka anayopewa ni makubwa na yanapaswa kuangaliwa upya,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema kutokana na hali inayoendelea katika Taifa, sasa hitaji la Katiba Mpya ni kubwa kuliko wakati wowote. “Ndiyo maana nasema, hakuna sababu yoyote ya kuacha hii ajenda, ipo haja ya kuifufua upya kudai Katiba Mpya itakayoyaangalia upya madaraka ya Rais,” alisema Profesa Mkumbo.

Tofauti na mawazo ya Profesa Kitila, msomi mwenzake wa uchumi, Profesa Haji Semboja alisema matukio makubwa yaliyoonekana kulitikisa Taifa miongoni mwake yapo nje ya mfumo wa kisiasa.

Mbali na matukio ya kiasili, profesa huyo alibainisha mambo mengine yanayohusu jinsi Serikali inavyobana matumizi na kuelekeza fedha kwenye miradi mikubwa ya maendeleo.

Alitolea mfano wa tetemeko la ardhi lililotokea katika mikoa mitatu lakini madhara makubwa yakionekana mkoani Kagera ambako watu 17 walifariki dunia, 252 walijeruhiwa huku nyumba za makazi 840 zikianguka na nyingine 1,264 kupata nyufa.

“Kwamba jambo hili limeshughulikiwaje, Serikali zilizopita hazikuweka mfumo kwamba yanapotokea maafa nini kifanyike, hakukuwa na mfumo. Hata Serikali ya sasa haikuja na suluhisho katika haya.

“Lakini ninaloliona jipya ni mfumo wa Serikali ambao ndiyo kwanza umeanza na uzuri mmoja ni muundo wa bajeti, na katika huu muundo tunauangalia kwenye hotuba ya bajeti, ambapo Serikali ilikuwa na bajeti nzuri, asilimia 40 zimeelekezwa kwenye maendeleo, ni muundo unaopunguza kula.”

Mategemeo ya wananchi ni uwezo wa Rais wa kusimamia wananchi waelekee kule walikoahidiwa ili wapate maisha bora, lakini matokeo yake siyo ya haraka.

Katika siku za karibuni, kimekuwapo kilio cha wananchi kukosa fedha wakihusisha hali hiyo na mikakati ya Serikali kurekebisha uchumi, lakini Profesa Semboja anasema hali hiyo ina sababu zake kiuchumi.

Msomi huyo alitolea mfano ujenzi wa barabara ya juu eneo la Tazara, akisema fedha zote zimeelekezwa katika maendeleo ya namna hiyo.

“Sasa utaona pesa yote ipo kule, tumefunga mkanda lakini matokeo yake huko mbele kila kitu kinakuwa kipo vizuri… Leo unajibana lakini kesho utakuwa vizuri, barabara zitafunguka viwanda vitajengwa na mambo yatakuwa mazuri,” alisema Profesa Semboja.

Katika ya mistari hiyohiyo, Profesa Samwel Wangwe alibainisha kuwa matukio mbalimbali yanayoonekana mapya katika kipindi cha mwaka 2016 yanatokana na mabadiliko ya uongozi uliopo sasa ambao unajaribu kupiga hatua kutoka moja kwenda nyingine.

Alisema ni wakati wa taasisi za Serikali kujipanga kuongeza kasi ya kufanya kazi kwa kufuata na kuzingatia misingi mipya ya kupinga rushwa na ufisadi, kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika vizuri na kuacha mtindo wa kuhujumu uchumi wa nchi.

Kutokana na kutokuona mabadiliko hayo, Rais Magufuli amekuwa ama akifukuza, kusimamisha au kutengua uteuzi, huku baadhi ya watumishi wakifikishwa kortini kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Profesa Wangwe alisema wananchi wanapaswa kuzingatia sheria zilizopo kwa kuongeza bidii na juhudi ili kuzalisha zaidi na kuondokana na malalamiko ya hali ngumu ya maisha.

“Serikali nayo iendelee kutoa sapoti kwa wananchi wake, iweke mazingira mazuri kwa wanaofanya kazi ili waweze kuzalisha na hiyo pesa inayodaiwa kupotea ipatikane,” alisema.

Ajali

Mbali na hayo yanayobainishwa na maprofesa hao, matukio mengine yanayoonekana kutikisa Taifa ni pamoja ajali za barabarani zilizopoteza maisha ya Watanzania wengi.

Ajali iliyotokea Julai 4, ikihusisha mabasi mawili ya kampuni ya City Boy katika Kijiji cha Maweni Wilaya ya Manyoni, Singida ilisababisha watu 29 kupoteza maisha papo hapo huku chanzo kikitajwa kuwa ni mwendo kasi na mbwembwe za madereva.

Ajali ingine ni ile iliyopoteza vifo vya watu 12 na wengine 30 kujeruhiwa vibaya wakati basi la kampuni ya New Force, linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Songea, Ruvuma kuacha njia na kupinduka.

Mauaji

Mwaka 2016 vilevile ulikithiri kwa matukio ya mauaji ya watu kinyama, wakiwamo askari polisi.

Miongoni mwa matukio hayo ni tukio la watu watatu kuchinjwa msikiti jijini Mwanza na watu wengine wanane wa familia tofauti kuchinjwa mkoani Tanga.

Kesi

Mwaka huu unamalizika huku kukiwa na kesi zilizotikisa ikiwamo ya mwenyekiti wa kampuni inayoshughulikia uwekezaji wa mitaji na dhamana (Egma), Harry Kitilya na waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya StanBic Tanzania, Sioi Sumari na Shose Sinare; watumishi wa waandamizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).