Mambo matano yatikisa mjadala ofisi ya Rais

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika akitoa kauli serikali bungeni mjini Dodoma wiki iliyopita. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Kwa siku tatu kuanzia Jumatano wiki hii, wabunge wamekuwa wakijadili hotuba hiyo na wengi walizungumzia zaidi masuala ya utawala bora, vyama vya upinzani, upelekaji fedha kwa halmashauri, mgawanyo wa fedha kwa wakala za Serikali na masilahi ya madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa.

Mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais kwa mwaka wa fedha 2018/19 unahitimishwa kesho, huku mambo matano yakiwa yamezua mjadala zaidi.

Kwa siku tatu kuanzia Jumatano wiki hii, wabunge wamekuwa wakijadili hotuba hiyo na wengi walizungumzia zaidi masuala ya utawala bora, vyama vya upinzani, upelekaji fedha kwa halmashauri, mgawanyo wa fedha kwa wakala za Serikali na masilahi ya madiwani na wenyeviti wa Serikali za mitaa.

Ofisi ya Rais inahusisha wizara za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Akichangia suala la utawala bora, mbunge wa Hanang (CCM), Dk Mary Nagu alihoji uhalali wa kupelekwa polisi kwa agizo la mkuu wa wilaya hiyo, Sara Msafiri.

Dk Nagu alisema aliwekwa ndani kwa sababu yuko karibu na wananchi wa Hanang.

“Nawashukuru wananchi wa Hanang kwa kunisikia nilivyowaomba wasiandamane kuja kule (polisi). Naomba waendelee kushirikiana nami,” alisema.

Msafiri ameshaagiza mara mbili Dk Nagu kuhojiwa na polisi, lakini wawili hao wameshasuluhishwa na kumaliza tofauti zao.

Katika mchango wake, mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe aliitaka Serikali iwaeleze wananchi wa Kigoma alipo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko, Simon Kangue.

Alisema Kangue aliitwa kwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo alikokutana na ofisa usalama wa wilaya na tangu wakati huo hajulikani alipo, licha ya kufanyika jitihada za kumtafuta.

Naye mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga alisema haelewi mafunzo yaliyotolewa na Serikali ni ya nini kwa sababu watendaji hawatekelezi majukumu yao kwa kuzingatia utawala bora.

“Baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya wanaonekana wameshindwa. Mmepoteza bure fedha za Serikali kwa kuwapa mafunzo lakini wakirudi hawafanyi kile walichotakiwa kufanya,” alisema.

Vyama vya upinzani

Katika michango yao, baadhi ya wabunge wa CCM walijielekeza kukosoa vyama vya siasa vya upinzani.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Martha Mlata aliomba kupelekewa salamu Rais John Magufuli awasaidie kupata upinzani utakaoleta maendeleo, unaojitambua na ulio bora.

“Msajili wa Vyama vya Siasa uwapeleke wapinzani kwenye nchi zenye upinzani wa mfano ambao mataifa yao yameweza kusimama imara kwa sababu hapa Tanzania bado hatujawa na upinzani ulio imara utakaosaidia Taifa,” alisema.

Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliwataka wabunge wanaohoji utaratibu wa kurejesha mali za CCM warudi katika chama hicho ili waweze kufaidi mali ambazo walichangia wakiwa katika chama hicho.

“Hata katika michango ya harusi huiingii chumbani kwa sababu umechangia, unaishia mlangoni tu,” alisema.

Pia, alizungumzia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) iliyoonyesha udhaifu katika usimamizi wa fedha za Chadema, akiwataka wabunge wa upinzani kutoa boriti katika jicho lao kabla ya kutoa kibanzi kilichopo kwenye Serikali ya CCM.

Upelekaji fedha halmashauri

Mbali na hayo, suala la fedha za miradi kutotolewa lilizungumzwa na mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma.

Alisema katika mwaka wa fedha 2017/18 fedha zilizopelekwa ni asilimia 16 ya zilizotengwa kwa ajili ya miradi hiyo.

“Miradi yetu haiendi kwa sababu fedha haziendi katika halmashauri zetu. Naomba fedha za kutosha zitengwe na zipelekwe,” alisema.

Alisema mkuu wa Wilaya ya Mtwara alilazimika kwenda kukagua miradi ya mfuko wa jimbo baada ya inayotekelezwa na halmashauri kusimama kutokana na fedha kutopelekwa.

Akichangia hoja hiyo, mbunge wa Mkinga (CCM), Dustan Kitandula alisema licha ya kutengwa Sh11 bilioni kwa ajili ya masuala ya lishe, ni asilimia nane (Sh888 milioni) ndizo zimepelekwa hadi Februari mwaka huu.

“Tuna tatizo kubwa katika lishe. Asilimia 45 ya vifo vya watoto vinahusishwa na utapiamlo. Asilimia 57 wana upungufu wa damu halafu hotuba hazizungumzii jambo hili. Taarifa zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2025 tutakuwa tumepoteza nguvu kazi ya Sh28.8 trilioni,” alisema.

Wakala za Serikali

Wabunge wengi walitaka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) kuongezewa mgawo wa fedha za bajeti kwa kuwapa nusu ya fedha za Wakala wa Barabara (Tanroads) ili iweze kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Mbunge wa Lulindi (CCM), Jerome Bwanausi alisema Tarura haijaongezwa bajeti na pasipo hilo kufanyika itakuwa wakala isiyo na tija huku Nachuma akisema wataalamu wa Tarura wamekuwa kama miungu watu.

Alisema wakiombwa na wabunge au madiwani kutoa ufafanuzi juu ya ujenzi wa barabara, wamekuwa wakikaidi kufanya hivyo.

“Tunaomba kama ni kubadilisha sheria tufanye ili Tarura wasimamiwe na madiwani na wabunge kwa sababu wanahudumia wananchi,” alisema.

Masilahi ya madiwani

Mmoja wa wabunge waliozungumzia masilahi ya madiwani ni mbunge wa Nanyumbu (CCM), Abdallah Chikota aliyesema imefika wakati kwa Serikali kuwakumbuka madiwani ambao alisema wana majukumu mengi na makubwa katika serikali za mitaa.

“Madiwani wana malalamiko. (Waziri wa Tamisemi, Selemani) Jafo madiwani wana matumaini makubwa na wewe. Unda tume uangalie ukubwa wa kazi zao na si vibaya upitie upya posho zao kwa sababu kiwango wanacholipwa sasa kina miaka zaidi ya sita,” alisema.

Chikota, ambaye ni makamu mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac), alisema kumlipa (diwani) Sh350,000 kwa mwezi na kumtaka kusimamia miradi ya halmashauri kunaweza kusababisha rushwa kwa kuwa wakuu wa idara ambao wanawasimamia wanalipwa kiasi kikubwa cha fedha.

Katika hilo la posho, Nachuma alisema katika jimbo lake la Mtwara Mjini, mwenyekiti wa mtaa analipwa Sh20,000.