Mambo mengi mazuri ya kujifunza kutoka Kenya

Muktasari:

Demokrasia ya Kenya imepiga hatua kubwa mno katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ukilinganisha yanayoendelea na kufanyika kwenye siasa za Tanzania na yanayoendelea Kenya utakubali kuwa wenzetu wako mbele yetu mara 100.

Pamoja na kwamba uchaguzi wa Kenya umefanyika salama huku ukiambatana na malalamiko ya msingi ya pande kuu zinazokinzana, Tanzania hawapaswi kujidai na kudhani kuwa Kenya inajikongoja. Kwa hakika, Kenya inapaswa kupongezwa na kuigwa kwa mambo mengi.

Demokrasia ya Kenya imepiga hatua kubwa mno katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ukilinganisha yanayoendelea na kufanyika kwenye siasa za Tanzania na yanayoendelea Kenya utakubali kuwa wenzetu wako mbele yetu mara 100.

Wametutangulia

Kenya imetutangulia kwenye masuala mengi. Wakati tunapata uhuru miaka ya 1960 uchumi wa Kenya ulikuwa karibu sawa na wa Tanzania, sarafu ya Kenya ilikuwa karibu sawa na ya Tanzania, n.k.

Miaka 50 baada ya uhuru wa nchi zetu uchumi wa Kenya uko mbele sana na hatutarajii kuifikia leo. Kenya wana viwanda vya uhakika vya kutosha na bidhaa nyingi zilizoko katika maduka yetu hapa Tanzania zinatoka China, Afrika Kusini na Kenya.

Sh1 ya Kenya leo hii ni sawa na Sh20 hadi Sh22 za Tanzania. Kwenye michezo ukifuatilia hata mashindano ya ubingwa wa dunia yanayoendelea hivi sasa pale London, Uingereza – Kenya ndiyo nchi ya pili kwa kuwa na medali nyingi, ikipitwa na Marekani tu.

Ukija kwenye utalii, sisi Tanzania tuna vivutio vingi vya utalii mara 10 kuishinda Kenya, lakini Kenya inaingiza fedha nyingi za utalii na kutuzunguka karibu mara 10.

Hata yale madini ya Tanzanite ambayo yanazalishwa Tanzania, iko miaka ambayo kwenye soko la dunia imerekodiwa kuwa Kenya ndiyo nchi iliyouza madini hayo kwa wingi kwenye soko hilo kuliko Tanzania.

Kama kuna Mtanzania anaweza kuthubutu kusema kuwa hatuna mambo muhimu ya kujifunza kutoka Kenya, kwa kweli itabidi ajishangae mwenyewe.

Demokrasia

Kwa sasa Kenya ni viongozi wa demokrasia katika ukanda wetu. Wamefanya mambo mengi makubwa katika sekta hiyo na Tanzania inapaswa kupelekwa shule. Msingi mkubwa wa demokrasia ya Kenya umetokana na Katiba yao ambayo ilipatikana kwa jasho na damu.

Hata kabla ya ujio wa Katiba ya sasa ya Kenya, demokrasia yao ilikuwa ya hali ya juu mno tangu Rais Daniel arap Moi alipoamua kuachana na uimla kwenye uongozi wake. Ndiyo maana haikuwa kazi kubwa kwa Mwai Kibaki kuingia madarakani mwaka 2002 kupitia muungano wa NARC ambao ulikisambaratisha chama kikongwe cha Kanu.

Na kama hiyo haitoshi Katiba ya Kenya imeweka misingi mingi muhimu ambayo inalifanya taifa hilo kuwa la kipekee katika ukanda wetu, kwenye masuala ya siasa.

Mathalan, nchini Tanzania mkuu wa nchi anaweza kuzuia shughuli za kisiasa za vyama vingine, hata kama yeye na chama chake wanaendelea nazo. Kenya, jambo hilo haliwezekani na huenda halitawezekana tena siku za mbele.

Wakenya wamejengwa katika misingi ya kusimamia yale yaliyomo kwenye Katiba yao, haki za wananchi wao, majukumu na wajibu wa Rais wao na mengineyo, hakuna wakati ambapo Rais wa Kenya atapoka mamlaka ya wananchi, haki zao na wajibu wao, na hakuna mahali ambapo Rais wa Kenya atasimamia mienendo sahihi ya vyama vingine vya siasa wakati na yeye anatoka kwenye chama cha siasa.

Mgawanyo wa madaraka

Mihimili ya dola nchini Kenya inafanya kazi zake kwa kiasi kikubwa bila kuingiliwa na mtu au chombo chochote na hali hiyo inaonekana tangu mwanzo wakati wawakilishi wa mihimili hiyo wakichaguliwa au kuteuliwa.

Mathalan, tazama jaji mkuu wa Kenya anavyoteuliwa, ni mchakato mrefu, wa wazi na unaihusisha jamii nzima. Nafasi ya jaji mkuu inatangazwa na wanaoitaka wanatuma maombi kisha wenye vigezo na sifa wanahojiwa na kamati maalumu iliyoundwa kwa mujibu wa Katiba.

Mahojiano ya kila anayetaka nafasi hii nyeti yanafanywa mbele ya kamera za vyombo vya habari na yanarushwa mubashara kila raia anaona, taifa zima linashiriki mchakato wa kumpata jaji mkuu.

Jaji mkuu wa namna hii akishapatikana hawezi kuyumbishwa na Rais aliyeko madarakani, Jaji Mkuu wa namna hii atalinda masilahi ya taifa kuliko kitu chochote, na ndiyo maana mahakama za Kenya zinafanya kazi kwa weledi mkubwa, zimetuacha mbali na ziko huru kwelikweli.

Serikali ya Kenya

Serikali ni Rais, Baraza la Mawaziri na vyombo vingine vyote vinavyotumika chini yake. Ukitaka kupima ikiwa Serikali inafanya majukumu yake na kuheshimu mipaka iliyoweka na Katiba dhidi ya vyombo vingine, tazama mfano wa Kenya.

Mara kadhaa katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu tumemsikia Rais Uhuru Kenyatta akisisitiza kuwa ikiwa atashindwa kwenye uchaguzi atakabidhi Ikulu kwa njia ya amani.

Katika hotuba yake ya mwisho kama Rais wa Kenya aliyoitoa siku moja kabla ya upigaji kura aliwasisitiza wakenya kwenda vituoni “kuwachagua viongozi wanaowataka”, siyo rahisi kusikia maneno hayo kutoka kwa Rais wa nchi ya Afrika ambaye yuko madarakani na yuko kwenye uchaguzi wa kusaka kipindi cha pili cha uongozi.

Marais wa nchi nyingi za Afrika ambao wanagombea urais kipindi cha pili na kuendelea hawasemi kauli hizo. Hapa Tanzania Rais anayegombea kipindi cha pili hatoi kauli hizo, yeye ataapa kila mara kwamba “nitashinda uchaguzi na nitaendelea kuwa Rais wenu.”

Kwenye kauli za namna hiyo kuna ujumbe muhimu na wa wazi, kwamba marais wa namna hiyo hawako tayari kushindwa na ikitokea wanashindwa hawawezi kuachia Ikulu. Mchezo wa namna hiyo ulifanywa na Rais Mwai Kibaki mwaka 2007, lakini si rahisi ukatokea katika Kenya ya sasa.

Mamlaka ya Rais yamedhibitiwa

Nchini Kenya mamlaka ya Rais yamedhibitiwa vizuri, yako mambo hawezi kuyaingilia hata kidogo hata kama yamo serikalini na yale masuala ambayo yako kwenye mihimili mingine, Serikali haiyagusi kabisa na ikijaribu kufanya hivyo Kenya inaweza kuingia kwenye matatizo makubwa.

Mfano mzuri ni hivi karibuni ambapo mahakama ya juu nchini humo ilitoa uamuzi muhimu kabla ya uchaguzi wa sasa, kuhusu utendaji wa Tume ya Uchaguzi ya nchini humo, IEBC na uamuzi ule ukaiathiri Serikali ya Kenya moja kwa moja.

Rais Uhuru Kenyatta alipotoa maoni yake kulaumu uamuzi ule wa mahakama, Jaji Mkuu wa Kenya na majaji wengine wakaeleza kuwa wao hawaingiliwi na mtu yeyote.

Tanzania hilo haliwezi kutokea, nchini kwetu kila kitu ni cha Serikali na kiko chini ya Serikali, Bunge ni tawi la Serikali na Mahakama ni tawi la Sserikali. Kwa Tanzania Serikali inaweza kuliamrisha Bunge inavyotaka na Serikali inaweza kuiamrisha mahakama hadharani na watu wakawa kimya. Wenzetu wanapiga hatua muhimu sana, sisi tunajikongoja kwelikweli.

Ukabila

Jambo moja kubwa ambalo tumewashinda Kenya ni hilo. Ukabila wao uko damuni na taifa hilo lilijengwa kwa misingi hiyo tangu lilipopata uhuru. Letu pia likajengwa kwenye misingi ya umoja na mshikamano, ambao tunaubomoa taratibu.

Nina maana kuwa Kenya ilibomoa misingi yake ya umoja tangu ilipopata uhuru na ni ukweli usiopingika kuwa wanapiga hatua kubwa sana za kimaendeleo na kidemokrasia ndani na katikati ya migawanyiko yao na wanakwenda mbele kama taifa.

Pamoja na ukabila wao, sisi Watanzania ambao tunadhani tuna taifa lenye umoja na mshikamano tunayo mengi ya kujifunza kutoka Kenya. Umoja na mshikamano wetu hautakuwa na maana siku za usoni ikiwa tunashughulikiana ndani ya nchi yetu, tunaumizana, tunadhibitiana na kupeana wakati mgumu mno. Tuchukue katua na kuendelea kutafakari hali ya taifa letu.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, mtafiti na mwanasheria. Simu; +255787t536759/ Barua Pepe; [email protected]/ Tovuti; juliusmtatiro.com