Marais watano wastaafu Marekani wawachangia waathirika wa vimbunga

Muktasari:

  • Rais Donald Trump alituma ujumbe katika tamasha la uchangiaji fedha.

 Marais watano wastaafu wa Marekani wamewezesha kuchangwa  Sh69 bilioni (Dola 31 milioni za Marekani) kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa vimbunga Harvey, Irma na Maria.

Marais hao Barack Obama, George W Bush, Bill Clinton, George HW Bush na Jimmy Carter walijumuika jana Jumamosi Oktoba 21,2017 katika tamasha lililolenga kuwachangia waathirika wa vimbunga hivyo vilivyotokea Agosti na Septemba mwaka huu.

“Kama marais wastaafu tunataka kusaidia Wamarekani wenzetu kurejea katika hali zao za kawaida,” amesema Obama.

Uchangiaji huo haukuhudhuriwa na Rais Donald Trump ambaye alituma ujumbe kupongeza juhudi hizo za watangulizi wake.

Marais hao walifika katika tamasha hilo na kuimba wimbo wa Taifa pamoja wakiwa jukwaani na baadaye  msanii wa kike Lady Gaga alitumbuiza.

Bill Clinton amesema suala hilo limewakutanisha wao kutoka vyama tofauti ili kusaidia matatizo yaliyotokea kwa wananchi walioathiriwa na vimbunga hivyo.

“Tufanye yale yanayotakiwa kufanywa kwa moyo, bila kujali rangi, dini wala vyama vya siasa hili ni kubwa kushinda hayo,” amesema Clinton.