Marekani yawataka raia wake waondoke Congo

Muktasari:

Hii inatokana na wasiwasi wa kuzuka machafuko ya kisiasa nchini humo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewaamuru raia wake wanaofanya kazi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuondoka nchini humo.

Hii inatokana na wasiwasi wa kuzuka machafuko ya kisiasa nchini humo.

Katika wiki za hivi karibuni, kumezuka vurugu zilizosababishwa na  maandamano ya wapinzani wanaopinga kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais.

Upinzani unasema hatua hiyo ni njama ya Rais Joseph Kabila, ambaye kwa mujibu wa katiba anafaa kuondoka madarakani mwezi Desemba, kuendelea kuongoza.

Takriban watu 50 wameuawa kwenye makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama mjini Kinshasa.

Maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo pia yamebaki kutokuwa salama, na serikali ya Rais Joseph Kabila imeshindwa kudhibiti hali katika maeneo mengi nje ya miji.

Alhamisi, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Mark Ayrault alinukuliwa akisema kwamba DR Congo imo hatarini ya kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa sababu rais aliyepo madarakani hataki kung'atuka.

CHANZO BBC