Masauni asisitiza onyo la maandamano

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Jumane Muliro (kushoto) wakati akitoka kukagua kituo kidogo cha polisi kinachohamishika, katika hafla ya kupoke vituo hivyo sita iliyofanyika katika viwanja vya Kituo cha Polisi Osterybay jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Masauni amesema watu wanaopanga kuandamana wasiijaribu Serikali la sivyo wataona kitakachowapata

 Siku chache baada ya Rais John Magufuli na waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba kuyazungumzia na kupiga marufuku yasifanyike maandamano, naibu waziri wa wizara hiyo, Yusuf Masauni naye amepigilia msumali.

Masauni amesema watu wanaopanga kuandamana wasiijaribu Serikali la sivyo wataona kitakachowapata.

Amesema hawatakubali kuruhusu watu wachache waitoe Serikali kwenye mstari wa maendeleo.

Naibu waziri huyo alisema hayo wakati akitoa akipokea vituo sita vya polisi vinavyohamishika kutoka katika kampuni ya vinywaji baridi ya CocaCola, hafla iliyofanyika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jana.

“Serikali imejitahidi kukabiliana na changamoto mbalimbali, lakini kuna baadhi ya watu wapo ndani ya nchi na wengine nje ni maadui wa mafanikio haya na wanataka kututoa katika ajenda,” alisema Masauni.

“Nasema nafasi hiyo hawana, kamwe Serikali na wizara hii hatutaruhusu mtu yeyote atutoe kwenye mstari.”

“Limeshasemwa. Mimi nasisitiza kama kuna wapuuzi wawili watatu wajaribu waone. Hatuwezi kuacha ajenda za msingi za maendeleo tukashughulika na vitu vya kipuuzi,” alisisitiza.

Mkuu wa operesheni na mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani alimhakikishia Masauni kuwa jeshi hilo liko imara na matukio ya uhalifu yamepungua.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Jumanne Murilo alisema vituo hivyo ni vya kisasa na vitakuwa na huduma zote muhimu kwa askari tofauti na vile vya awali.