Serikali ya Marekani yafungwa

Muktasari:

Trump na wawakilishi wake wamelibatiza tukio hilo kuwa ni “Kufungwa kwa Schumer” wakimbeza Seneta kiongozi wa waliowachache Chuck Schumer wa chama cha Democratic kutoka New York lakini naye alijibu haraka kwamba ni "Kufungwa kwa Trump."

Washinton, Marekani. Kile kilichotokea mwaka 2013 wakati wa utawala wa Barack Obama kimejirudia kwamba Serikali ya Shirikisho la Marekani imefunga baadhi ya shughuli zake kuanzia mapema leo Jumamosi baada ya Baraza la Seneti kushindwa kupitisha mswaada wa matumizi ya Serikali.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali kufungwa wakati Baraza la Congress na Ikulu ya White House vyote vikidhibitiwa na chama kimoja na limetokea katika mkesha wa kutimiza mwaka mmoja tangu Rais Donald Trump aingie madarakani.

Punde baada ya tukio hilo Ikulu ya Trump ilitoa taarifa ikiwarushia lawama maseneta wa Democratic kwamba ndio wamesababisha serikali kufungwa.

"Usiku huu, wameweka siasa juu ya usalama wetu wa taifa, familia za kijeshi, watoto waishio katika mazingira magumu, na uwezo wa nchi yetu kuwahudumia Wamarekani wote," taarifa ya katibu wa mawasiliano wa Ikulu Sarah Sanders ilisema usiku wa manane. "Hatutajadiliana kuhusu hadhi ya wahamiaji haramu wakati Wademocrat wamewashika kama mateka raia watiifu kutokana na madai yao yasiyo na maana. Tabia hii ya kuzuia ni ya walioshindwa siyo wabunge.”

Trump na wawakilishi wake wamelibatiza tukio hilo kuwa ni “Kufungwa kwa Schumer” wakimbeza Seneta kiongozi wa waliowachache Chuck Schumer wa chama cha Democratic kutoka New York lakini naye alijibu haraka kwamba ni "Kufungwa kwa Trump."

"Kwa ujumla ni kama ulikuwa unajiandaa kwa tukio la kufungwa," alisema Schumer akiwa ndani ya Bunge. "Na sasa tutakuwa na moja. Na lawama hizi lazima Trump abebe mabegani mwake. Tukio hili litaitwa Kufungwa kwa Trump. Tukio hili litaitwa Kufungwa kwa Trump kwa sababu hakuna nyingine, hakuna, nani mwingine anastahili lawama kwa mazingira tunayojikuta tumo zaidi Rais Trump."

Maana yake

Matumizi ya serikali yalimalizika saa 6:00 usiku Ijumaa kwa saa za Marekani, hivyo shughuli zote zisizo za lazima zimesimamkishwa.

Japokuwa Rais Trump anawalaumu maseneta wa Democratic, hata baadhi ya maseneta wa chama tawala cha Republican waliungana na Wademocrat kupinga muswaada wa sheria ya matumizi ya serikali. Muswada huo ulikuwa unahitaji kura 60 kupita katika baraza hilo lenye wajumbe 100.

Baada ya kushindwa kufikia makubaliano Ijumaa maseneta hao sasa wanalazimika kuwa na majadiliano ya dharura ndani na nje ya Bunge ili waweze kuridhiana na hatimaye wapitishe matumizi ya serikali na suala la uhamiaji.

Wademocrat walijaribu kupata maridhiano na wenzao wa Republican, hasa nyongeza ya muda juu ya pgramu ya kuwahami wahamiaji wasirejeshwe makwao kwa vile muda wao unaisha Machi.

Katika hitoria ya Marekani hii si jambo geni shughuli za serikali kufungwa kwani hii ni mara nne katika kipindi cha miaka 25 na mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2013 ambapo ilifunga shughuli zake kwa siku 16.