Mashirika ya ndege yabadili njia

Muktasari:

  • Taarifa hiyo ya Korea Kaskazini imekuja kutokana na onyo lililotolewa na Rais Donald Trump kuwa Marekani itaiangamiza Korea Kaskazini

Tokyo Japan. Mashirika matatu ya ndege ya barani Ulaya yamebadilisha njia kuu za ndege zao zinazosafiri kati ya Ulaya na Japani ili kukwepa kupita kwenye anga la Bahari ya Japani, kutokana na Korea Kaskazini kurusha makombora mengi kuelekea kwenye bahari hiyo.

Uamuzi wa mashirika hayo umefanywa katika muda sahihi kwani vyombo vya habari nchini Korea Kaskazini vimeripoti kuwa kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jong Un, ameahidi kuijibu Marekani kwa kufanya jaribio jingine la bomu la Hydrogen katika bahari ya Pasifiki.

Taarifa hiyo ya Korea Kaskazini imekuja kutokana na onyo lililotolewa na Rais Donald Trump kuwa Marekani itaiangamiza Korea Kaskazini iwapo italazimishwa kujilinda au kuwalinda washirika wake. Rais Trump aliyasema hayo Jumanne alipohutubia Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Kim ameilezea hotuba ya Trump kuwa sawa na kelele za mbwa mwoga anayebweka na kwamba ataendelea na mipango yake ya maendeleo ya nyuklia na makombora akidai hotuba ya Trump inadhihirisha kuwa Korea Kaskazini inafuata mwelekeo sahihi.

Mashirika ya ndege

Mashirika yaliyoamua kubadili njia ni Shirika la Ndege la Lufthansa la Ujerumani, Shirika la Ndege za Kimataifa la Uswisi na Shirika la Ndege la Scandinavia yaliyoanzisha njia mpya mwezi uliopita. Ndege za mashirika hayo kwa sasa zinapita sambamba na visiwa vya Japani katika anga la maeneo ya kaskazini ya Hokkaido na Tohoku wakati zinapokaribia jiji la Tokyo au vituo vingine nchini Japani.

Mashirika hayo ya ndege yamesema kuwa njia hizo mpya hazijasababisha mabadiliko makubwa katika umbali au muda ndege hizo zinaotumia kusafiri. Shirika la ndege la Lufthansa limesema kuwa lilifanya mabadiliko hayo kama hatua ya tahadhari na kuwa ni sehemu ya hatua endelevu za kuepuka majanga kufuatia urushwaji wa makombora unaofanywa na Korea Kaskazini.