Mauzo soko la hisa DSE yapaa

Muktasari:

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Mwandamizi wa Masoko wa DSE, Mary Kinabo ilisema idadi ya mauzo hayo imeongezeka kutokana na kupanda kwa idadi za hisa zilizouzwa kutoka Sh1.6 bilioni  hadi kufikia  Sh2.2 bilioni.

Dar es Salaam. Idadi ya mauzo katika soko la hisa la Dar es salaam (DSE) imeongezeka kwa asilimia 57 na kufikia Sh3.3 bilioni kutoka Sh2.1 bilioni wiki iliyopita kutokana na ukubwa wa idadi ya mauzo.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Mwandamizi wa Masoko wa DSE, Mary Kinabo ilisema idadi ya mauzo hayo imeongezeka kutokana na kupanda kwa idadi za hisa zilizouzwa kutoka Sh1.6 bilioni  hadi kufikia  Sh2.2 bilioni.

Katika taarifa hiyo, Benki ya CRDB imeongoza kwa idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa kwa asilimia 49 ikifuatiwa na Soko la hisa DSE ikiwa na asilimia 43 na ya tatu ni Kampuni ya Bia nchini (TBL) yenye asilimia nne.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa ukubwa wa mtaji wa soko umepanda kwa asilimia 0.67 na kufikia Sh 23.4 trilioni kutoka Sh23.2 trilioni wiki iliyopita na ukubwa wa mtaji wa kampuni za ndani umebaki kuwa Sh8.4 trilioni. Ilisema kwamba licha ya mauzo kupanda, lakini viashiria vya soko katika sekta ya viwanda vimeshuka kwa alama 19.47.