Mawakili wa Lema waomba kesi ipelekwe Mahakama ya Katiba

Mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema na mkewe Neema wakiwa  kwenye Mahakama ya Hakimu mkazi mkoani  Arusha jana. Picha na Musa Juma

Muktasari:

Wadai kesi hiyo inagusa haki za msingi zinazotolewa na Katiba

Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amepandishwa kizimbani akikabiliwa na kesi mbili; ya kutoa lugha ya kuudhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na kuhamasisha maandamano ya Ukuta ambayo mawakili wake wameomba ipelekwe Mahakama ya Katiba.

Katika kesi namba 352, Lema alipandishwa mbele ya Hakimu Bernard Ngaga akituhumiwa kati ya Agosti Mosi hadi 26 kuwa alitumia mtandao wa WhatsApp kuhamasisha watu kuandamana Septemba Mosi ilhali akijua ni kinyume cha sheria.

Hata hivyo, jana shahidi wa kwanza upande wa mashtaka ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Arusha, George Katabazi alitarajiwa kuanza kutoa ushahidi lakini mawakili wa utetezi, John Mallya na Sheck Mfinanga waliwasilisha hoja ya kusitishwa ushahidi.

Akisoma hoja hizo, Wakili Mallya alidai wanapinga kuendelea kusikilizwa ushahidi, kwani kuna masuala ya kikatiba hivyo ni vyema wapate ufafanuzi Mahakama ya Katiba ili kesi iweze kuendelea.

Alidai shauri linagusa haki zilizotolewa na Ibara ya 18 na 20 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inatoa uhuru wa watu kufanya mikutano na kuandamana na inaungwa mkono na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Katika kuonyesha haki za kisiasa ni muhimu, Wakili Mallya alitaja Ibara 46A(1) na (2)(b) ya Katiba inazungumzia kama Rais akikiuka haki hizo za kisiasa na Kikatiba anaweza kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Bunge, hivyo kuondolewa madarakani.

Jamhuri yapinga

Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Alice Mtenga alipinga hoja hiyo na kueleza kuwa kesi hiyo siyo ya Kikatiba na kuomba Mahakama kuendelea na shauri hilo.

Wakili Mtenga aliiomba Mahakama kuwapa muda wa kujibu hoja za utetezi kwa tarehe nyingine ambayo itapangwa.

Hata hivyo, Wakili Mallya alidai upande wa utetezi haujasema kesi hiyo ni ya kikatiba, bali kuna maswali ya Kikatiba ambayo shahidi wa mashtaka hawezi kuyajibu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Hakimu Ngaga alisema haoni sababu ya kutoa muda zaidi kwa upande wa mashtaka kujibu hoja za utetezi, kwani tayari wamejibu. Alisema atatoa uamuzi wa shauri hilo Februari 8.

Kesi ya lugha ya kuudhi RC

Katika kesi namba 351, Lema na mkewe, Neema wanatuhumiwa kumtumia Gambo ujumbe wa kuudhi.

Katika maelezo hayo yaliyosomwa na Wakili Mtenga mbele ya Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa Arusha, Nestory Baro, alidai Lema (40) alikamatwa na kufikishwa mahakamani Agosti 29 mwaka jana kwa kosa la kumtumia ujumbe wa kuudhi Gambo.

Alidai kukamatwa kwakwe kulitokana na kosa alilotenda Agosti 20, Agosti mwaka jana kupitia simu inayodaiwa kumilikiwa na mke wake.

Alidai ujumbe huo ulisomeka: “Karibu Arusha tutakudhibiti kama mashoga wanavyodhibitiwa Uarabuni.”

Hata hivyo, Lema na mkewe walikana mashtaka na kudai tarehe iliyoandikwa kuwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani haikuwa sahihi.

“Nilipandishwa mahakamani kweli Agosti 29, lakini sikukamatwa na kupandishwa mahakamani siku hiyo moja,” alidai Lema.

Wakili Mallya licha ya kuwasilisha notisi ya kupinga maelezo hayo, aliomba hoja hizo zisikilizwe kwa njia ya mdomo siyo maandishi. Hakimu Baro alipanga Februari 3 kuanza kusikiliza mapingamizi hayo.